Home Mchanganyiko AG FELESHI AWATAKA WAKUU WA DIVISHENI NA VITENGO KUWEKA MALENGO YA KAZI

AG FELESHI AWATAKA WAKUU WA DIVISHENI NA VITENGO KUWEKA MALENGO YA KAZI

0

Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliezer Feleshi akizungumza na  wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi ( hawapo Pichani)  katika kikao cha Baraza  hilo kinachofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jengo la TMDA Mkoani Mwanza.  Moja ya mambo aliyoyasisitiza ni pamoja na uboreshaji wa  maslahi ya  watumishi wa  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu  wa Serikali na Taasisi zake
**********************

Na Mwandishi Maalum

Mwanza

Wakuu wa Idara na Vitengo  katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wametakiwa kuweka malengo  pamoja  na kuwa na  miongozo ya ndani itakayoainisha  shabaha na muda wa kutekeleza kila kazi.

Ametoa wito huo katika siku ya kwanza ya mkutano wa siku mbili wa Baraza la Wafanyakazi la  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali unaofanyika  Jijini Mwanza.

Dkt. Feleshi amesema,  Kupitia kikao  hicho cha Baraza  angependa  kukitumia kukumbushana  mambo machache kuhusu  utendaji kazi wetu  wa kila siku katika  maeneo kadhaa.

Eneo la kwanza ambalo  Mwanasheria Mkuu   amewakumbusha wakuu hao wa Divisheni na Vitengo  na watumishi wote wa ujumla,   ni kuhusu majukumu yetu ya kazi ambapo  amesisitiza kwamba ni wajibu   wa  kila mtumishi kuzitambua na kuzianisha kazi,  kuzielewa na kuzitekeleza kwa weledi.

Kwa mujibu wa Mwanasheria  Mkuu wa Serikali anasema  Uzoefu unaonyesha kuwa watumishi  katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu  wa Serikali wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea.

Eneo la pili ambalo  Dkt. Feleshi  amelikumbusha ni kwa wakuu  Divisheni na Vitengo   kuweka malengo ya kazi.

“Ninatoa  wito kwa Wakuu wa  Divisheni na Vitengo kuweka malengo, kuwa na miongozo ya ndani kwa kuanisha shabaha na muda wa kutekeleza kila kazi kwa ufanisi na kwa wakati.” Amesisitiza Dkt. Feleshi.

Aidha amebainisha  kuwa , Wakuu wa Divisheni na Vitengo wanatakiwa kuhakikisha uwepo wa mambo matatu wakati wa kutekeleza mpango kazi wa Ofisi.

Ameyataja mambo hayo kuwa ni; kueleweka kwa  majukumu ( clarity), kwamba kiongozi  ahakikishe kazi inayotolewa  maelekezo na aliyempa kufanya kazi hiyo anaelewa nini anatakiwa  kufanya.

Jambo la pili  ambalo ameelekeza kwa wakuu wa divisheni na  vitengo kuzingatia ni; uwezo au umahiri( competence) kwamba, mtumishi anayepewa kazi anao uwezo wa kuielewa na kuitekeleza kazi hiyo kwa ukamilifu pasipo makosa.

“Jambo la tatu ni mazingira wezeshi ( Climate) kwamba, pawepo na mazingira wezeshi na yenye kumwezesha mtumishi kufanya kazi zake kwa ufasaha na kufikia malengo yaliyokusudiwa hii ni pamoja na kuwepo kwa vitendea kazi” amebainisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Eneo la  Tatu ambalo  amewakumbusha Wakuu wa   Divisheni na Vitengo  pamoja na watumishi wote ni  suala la uadilifu ambapo  pamoja na kutilia mkazo  kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, lakini  amehimiza kutumiwa kwa njia  ya kuelimishana na kuchuka hatua stahiki mapema kwa watumishi wenye viashiria vya  kutekeleza majukumu yao kinyume na maadili.

“Ofisi iwe ni sehemu ya malezi na siyo kusubiri kutibu tatizo, aidha uzingatiaji wa uadilifu tuuhimize pia kwa Taasisi ambazo ni wadau  wetu wa ndani ya nje ambao tunafanya nao kazi” akasema.

Aidha Mwanasheria Mkuu wa Serikali pia amesisitiza haja na umuhimu wa kujenga uwazi katika mifumo yetu ya kutekeleza majukumu na vilevile kuomba mrejesho kutoka kwa wadau.

Kuhusu Maslahi ya Watumishi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali  ameeleza kwamba, amekwisha kutoa maelekezo kwa Menejimenti  ya Ofisi  kuandaa andiko la kujenga hoja ili Bajeti ya Ofisi  yetu na Taasisi zake ziweze kuongezwa na  kuwezesha kutatua changamoto zilizopo katika  maeneo ya ununuzi wa vitendea kazi, kuboresha maslahi kwa watumishi na mafunzo  kwa watumishi.

“Hivyo natoa wito kwa Idara zinazohusika na kazi hiyo kukamilisha kazi hiyo ambayo pia iliridhiwa na kikao cha ( Government Legal Team) kilichofanyika Novemba 22, 2021 ili tuweze kuwasilisha andiko hilo kwenye mamlaka husika” amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akielezea zaidi kuhusu  maslahi ya watumishi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa na haya ya kusema

“Kulingana na  hali ya kifedha tunayopokea katika Ofisi, hatuna budi tuendelee kutoa kipaumbele  kulipa stahiki za watumishi, kwani kwa kulipa madai na stahiki zao mbalimbali kwa wakati tutakuwa tunatekeleza matakwa ya kisheria”

Katika  siku ya kwanza ya Baraza , wajumbe walipata nafasi ya  kupokea   taarifa mbalimbali  na kisha kuzijadili na pia kutolewa ufafanuzi Makamu Mwenyekiti wa Baraza  Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Longopa na Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo na  Wasimamizi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kutoka mikoa Tisa ambako Ofisi hizo zipo.