Home Burudani RC IBUGE AHIMIZA VIVUTIO VYA UTALII KUSINI VITANGAZWE KWA NGUVU ZOTE

RC IBUGE AHIMIZA VIVUTIO VYA UTALII KUSINI VITANGAZWE KWA NGUVU ZOTE

0

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akicheza ngoma ya Lizombe katika uwanja wa Majimaji mjini Songea siku ya kufunga Tamasha la Majimaji Selebuka ambalo limefanyika kwa siku nane

Mkuu wa Mkoa wa Lindi mheshimiwa Zainabu Telaki akiwa na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakibadilishana mawazo na Chifu wa Tano wa Kabila ya Wangoni Chifu Imanuel Zulu mara baada ya kufungwa Tamasha la Majimaji Selebuka katika uwanja wa Majimaji mjini Songea

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akikagua moja ya mabanda ya maonesha kwenye tamasha la Majimaji Selebuka mjini Songea

……………………………………………………………..

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ametoa rai kwa wadau wa watalii kuvitangaza vivutio vilivyopo ukanda wa kusini ili kufungua milango ya uwekezaji.

Ametoa rai hiyo wakati anafunga tamasha la  Majimaji Selebuka ambalo limefanyika kwa siku nane kwenye uwanja wa michezo wa Majimaji mjini Songea.

“Tumezoea sana kutangaza vivutio kutoka kaskazini na  fukwe zilizopo Mashariki mwa nchi yetu, uwekezaji kusini unahitaji juhudi za pamoja wadau na wananchi wa Kusini ili  Southern Circuit yaanik Mzunguko wa Kusini kwa hakika utangazwe vema’’,alisisitiza  RC Ibuge.

Amesema kinachotafutwa hivi sasa ni kuongeza mapato kupitia sekta ya utalii na kuhakikisha kuna uendelevu wa kutambulisha vivutio vya kusini Duniani.

Brigedia Jenerali Ibuge amesema kuna soko kubwa la sekta ya utalii hivyo  juhudi kubwa katika kutangaza vivutio vya utalii zinaweza kuongeza uthaminishaji wa maliasili zilizopo na kuongeza kipato kwa wabunifu na wananchi.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kulitendea haki tamasha la Majimaji Selebuka mwaka huu ambapo ameagiza kuongeza juhudi zaidi katika kuhakikisha matamasha yajayo  yanakuwa na ushiriki mkubwa na kuongeza vikundi vya ushiriki kutoka mikoa ya Ruvuma,Lindi na Mtwara.

Katika Hatua nyingine RC Ibuge amewakumbusha wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na UVIKO 19 kwa kuzingatia maelekezo yote yanayotolewa na wataalam wa afya.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mheshimiwa Zainabu Telaki akizungumza kwenye tamasha hilo  ametoa rai kwa wadau wa utalii kuhakikisha kuwa vivutio vyote vilivyopo kwenye mikoa mitatu ya kusini vinatangazwa kwenye luninga zote zilizopo nchini ili kufungua fursa za utalii kusini.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema akizungumza kwenye tamasha hilo amesisitiza vivutio adimu vya utalii vilivyopo kusini  ambavyo havipatikani sehemu nyingine duniani  vitangazwe kitaifa na kimataifa kuvutia wawekezaji.

Mgema ametoa rai kwa Bodi ya Utalii Tanzania kuhakikisha kuwa vivutio vya kusini vinakuwa sehemu ya vivutio vinavyotangazwa ili watalii wengi waweze kufika mikoa ya kusini kuangalia vivutio hivyo.

Amesema serikali tayari imeimarisha miumbombonu katika mikoa ya kusini hivyo watalii wanaweza kufika kusini kwa kutumia usafiri wa anga,barabara na majini.