Naibu Waziri Mhandisi Maryprisca Mahundi akikagua ujenzi wa mradi. Nyuma yake ni Katibu Umoja wa Vijana CCM, Kenani Kihongosi. Mbele yao ni Meneja RUWASA wilaya ya Chunya Mhandisi Ismail Ismail.
miundombinu ya mradi wa maji Matwiga
………………………………………………………………..
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema mradi wa maji wa Matwiga uliopo Wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya unatekelezwa kwa awamu tatu, na awamu ya kwanza itatumia kiasi cha shilingi bilioni 2.3.
Ameyasema hayo wakati wa ukaguzi wa mradi huo unaotarajiwa kuanza kutoa huduma mwezi Agosti 2021, na unatekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Amesema serikali itaendela kutoa fedha ili mradi huo ukamilike kwa awamu zote tatu kwa wakati, na kuainisha kuwa mradi huo ni miongoni mwa miradi ambayo serikali imedhamiria kuikwamua baada ya kukwama kwa muda mrefu.
“Tumeamua kufanya mageuzi katika sekta ya maji. Jukumu moja kubwa katika mageuzi haya ni pamoja na kukwamua miradi yote ambayo imekwama kwa muda mrefu. Niwashukuru viongozi wote wa Wizara kuanzia kwa Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso, Katibu Mkuu wa Wizara Mhandisi Anthony Sanga. Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Nadhifa Kemikimba pamoja na watumishi wote wa Wizara. Wanajituma kila siku kuhakikisha malengo ya serikali yanafikiwa.” Naibu Waziri Mahundi amesema.
Ameongeza mradi huo ulikwama tangu mwaka 2012 lakini kwa sasa umeanza na hautasimama.
Mradi wa maji wa Matwiga chanzo cha maji yake ni bwawa la asili na unatekelezwa kwa kutumia wataalam wa Wizara ya Maji.
Naibu Waziri Mahundi katika ukaguzi huo aliambatana na Katibu wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya Taifa, Ndugu Kenani Kihongosi, ambaye ameishukuru serikali kwa kufanya uamuzi wa kujenga mradi huo.
Kihongosi amesema nia ya serikali ni kuhakikisha wananchi wa Chunya wanapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza kama ilivyoahidiwa ndani ya ilani ya uchaguzi ya CCM
Amewataka wananchi kuhakikisha wanalinda miundombinu ya mradi huo ili kupata huduma endelevu.
Awali akitoa taarifa ya Mradi Meneja wa RUWASA wilaya ya Chunya Mhandisi Ismail Ismail amesema mradi huo unalenga kuhudumia jumla ya vijiji 16 vyenye zaidi ya wakazi elfu 74, ambapo awamu ya kwanza imefikia asilimia 80.
“Awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi ni miundombinu kwa ajili ya vijiji vya Matwiga na Isangawana ambapo watu 18,000 watapata huduma ya majisafi na salama. Kwa sasa mradi umefikia asilimia 80 na tunatarajia kukamilisha ifikapo Agosti 30, 2021. Aidha mradi huu utasaidia kuongeza kiwango cha upatikanaji maji wilayani Chunya kwa asilimia 37 na hivyo kufanya kiwango cha upatikanaji maji kufikia asilimia 65.” Mhandisi Ismail amesema.