Home Mchanganyiko UPUNGUFU WA WATUMISHI WASABABISHA MRUNDIKANO WA KESI SONGWE

UPUNGUFU WA WATUMISHI WASABABISHA MRUNDIKANO WA KESI SONGWE

0

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geofrey Mizengo Pinda (aliyevaa suti nyeusi) akikagua ramani ya ujenzi wa Mahakama ya Mkoa wa Songwe inayojengwa katika kijiji cha Nselewa Wilayani Mbozi katika ziara yake ya siku mbili mkoani hapa.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Omary Tebweta Mgumba akizungumza na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geofrey Mizengo Pinda (aliyevaa suti nyeusi) kabla ya kuanza ziara yake ya siku mbili mkoani hapa.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geofrey Mizengo Pinda (aliyevaa suti nyeusi) akisalimia wajumbe wa kamati ya ulizni na usalama Mkoa wa Songwe kabla ya kuanza ziara yake ya siku mbili mkoani hapa.

………………………………………………………………

Na Grace Gwamagobe

Upungufu wa watumishi katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali kwa Mkoa wa Songwe umepelekea mrundikano wa kesi hali inayoweza kusababisha ongezeko la uhalifu.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Omary Tebweta Mgumba ameyasema hayo jana wakati akizungumza na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geofrey Mizengo Pinda alipofanya ziara ya siku mbili Mkoani hapa.

“Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkoa wa Songwe inao watumishi wawili kati ya kumi wanaotakiwa kuwepo na hao wawili tu wanahudumia wilaya zote nne za Mkoa wetu, hawa lazima waelemewe na hivyo kupelekea kesi nyingi kuchelewa kukamilika, tunaomba mtutazame kwenye hilo.”, amesema  Mhe. Mgumba.

Ameongeza kuwa kuna changamoto ya ukosefu wa Mahakama za Wilaya ambapo kwa Mkoa wa Songwe ni Wilaya ya Mbozi pekee yenye mahakama huku Wilaya tatu zilizobaki zikitumia majengo ya kupangisha.

Mhe Mgumba pia amemueleza Naibu Waziri Pinda kuwa kuna ukosefu wa vifaa ikiwa ni pamoja na magari ambayo hutumika katika kusafirishia wafungwa pamoja na miundombinu ya maji katika magereza kutojitosheleza.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geofrey Mizengo Pinda amesema kuhusu changamoto ya watumishi serikali imeendelea kutoa vibali vya ajira ili kuongeza idadi ya watumishi lakini Mkoa unapaswa kuangalia kesi ambazo sio za Msingi zifutwe ili kupunguza mrundikano wa kesi na mahabusu.

Naibu Waziri Pinda ameongeza kuwa kesi nyingine zinaingiza hasara serikali kwani zinakuwa hazina msingi lakini pia kwa kesi ndogondogo mahakimu waangalie namna ya kutoa vifungo vya nje ili kuipunguzia serikali mzigo wa kutunza wafungwa.

Pia amemsisitiza Mkuu wa Mkoa kuendelea kusimamia maadili ya mahakimu kwakuwa yeye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Mahakama kwa ngazi ya Mkoa.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geofrey Mizengo Pinda amefanya ziara ya Siku mbili mkoani Songwe ambapo ametembelea majengo ya mahakama, Mahabusu na Magereza.