Home Mchanganyiko SERIKALI IMETOA ZAIDI YA BILIONI TATU KWA TAASISI MBALIMBALI ZA UTAFITI

SERIKALI IMETOA ZAIDI YA BILIONI TATU KWA TAASISI MBALIMBALI ZA UTAFITI

0

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari, Dkt Stella Bitanyi wakiangalia moja ya sampuli ya chanjo bora ya mifugo katika Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) alipokwenda kukagua vifaa vilivyonunuliwa na fedha zilizotolewa na Wizara

Mmoja wa wataalamu wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) akimweleza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako matumizi ya moja ya vifaa vilivyonunuliwa na Wizara ya Elimu kwa ajili ya utafiti

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akijaribu kutumia moja ya kifaa cha upimaji sampuli ya chanjo bora katika Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) wakati alipokwenda kukagua vifaa vilivyonunuliwa na fedha zilizotolewa na Wizara hiyo kupitia COSTECH.

………………………………………………………..

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa Taasisi mbalimbali zinazofanya utafiti katika masuala ya Kilimo, Viwanda, Afya na Mifungo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako leo Julai 3, 2021 wilayani Kibaha wakati alipotembelea na kufanya ukaguzi wa namna fedha shilingi milioni 400 zilizopelekwa katika Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) zilivyotumika.

Profesa Ndalichako amesema fedha hizo zilipelekwa katika Taasisi hiyo kwa lengo la kuiwezesha kupata vifaa muhimu vinavyotumika katika uthibiti ubora wa chanjo zinazozalishwa nchini pamoja na kufadhili mradi unaolenga kupata mbegu kuu ya chanjo ya magonjwa ya Homa ya Mapafu ya Mbuzi.

“Taasisi hii ni kati ya taasisi zilizopatiwa fedha na Wizara kupitia COSTECH ili kuwezesha kufanya utafiti katika eneo lao la mifugo, ninayo furaha kuona fedha walizopata wamezitumia kununulia vifaa muhimu pamoja na kuwapeleka mafunzo wataalamu wao ili kuongeza ujuzi na weledi katika kazi” amesema Waziri Ndalichako.

Waziri huyo amesema ufadhali huo umesaidia sana katika kuongeza tija katika taasisi hiyo, hivyo Wizara yake itaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya utafiti ambayo inaendana na malengo ya Maendeleo ya Taifa.

Amesema fedha hiyo siyo fedha nyingi katika utafiti lakini imesaidia kwani ni muhimu kama Taifa kuwa na madawa na chanjo zake yenyewe ambazo zinaaminika.

Aidha ameridhishwa na namna Wizara ya Mifugo ilivyoweza kusimamia Taasisi yake katika kuhakikisha fedha ambazo wamepata inatumika kama ilivyokusudiwa na kuleta matunda kwa Taifa.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini Dkt.Stella Bitanyi ameishukuru Wizara ya Elimu kwa ufadhili huo ambao umesaidia Taasisi yake kuongeza ufanisi katika kuzalisha chanjo na kuongeza kiwango cha uzalishaji ambapo mwanzo walikuwa wakizalisha dose milioni 40 lakini baada ya ufadhili imefikia dose milioni 60.

Batinyi ameendelea kueleza kuwa ufadhili huo pia umewezesha Taasisi hiyo kuzalisha chanjo za kimkakati zinazotumia teknolojia ya cell culture. Hivyo Wizara ya Elimu imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha sekta ya Mifigo nchini hususan katika kudhibiti magonjwa ya mifugo kupitia chanjo bora zinazoendelea kuzalishwa ambazo hatima yake ni kuwa na mazao mifugo iliyo bora ambayo pia itatoa mazao bora.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt. Amos Nungu amesema kuwa ufadhili unaotolewa kwa ajili ya utafiti unaangalia tafiti ambazo zinaendana na ajenda za maendeleo za Kitaifa. Hivyo utafiti huu pia ni muhimu na unaendana ajenda za maendeleo kupitia Sekta ya Mifugo.