Home Mchanganyiko SERIKALI YAWATAKA WASIMAMIZI WA SHULE NA VYUO KUZINGATIA MUONGOZO WA KUJIKINGA NA...

SERIKALI YAWATAKA WASIMAMIZI WA SHULE NA VYUO KUZINGATIA MUONGOZO WA KUJIKINGA NA CORONA,KUANZISHA KIWANDA CHA CHANJO YA CORONA

0

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi akizungumza na Waandishi wa Habari Leo Julai 4,2021 jijini Dodoma  wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 kwenye shule na Taasisi za Vyuo zinazotarajiwa kufunguliwa hapo kesho kulia Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Prof. Carolyne Nombo

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Prof. Carolyne Nombo akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari jijini Dodoma leo wakati wa kutoa tamko la Serikali kuhusu kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 kwenye shule na Taasisi za Vyuo zinazotarajiwa kufunguliwa hapo kesho kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi

………………………………………………………..

Na.Alex Sonna,Dodoma.

SERIKALI imewataka  viongozi na wasimamizi wa shule na Vyuo kuzingatia mwongozo wa kudhibiti ugonjwa wa UVIKO 19 ili kujikinga bila kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi huku ikianza mchakato wa kutengeneza chanjo ya Virusi vya Corona  hapa nchini

Hayo yamesemwa leo Julai 4,2021 jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Prof.Abel Makubi amesema  kuwa wasimamizi wote wanapaswa kuuzingatia muongozo huo na kuutekeleza ipasavyo ikiwemo kuweka vyombo maeneo mbalimbali ili wanafunzi waweze kunawa kwa maji tiririka na sabuni lakini kuhimiza matumizi ya barakoa kwa wanafunzi.

“Mwaka jana tulitoa muongozo huu ,inawezekana ,matumizi ya vifaa hivi yalipungua au yalisitishwa kabisa ,sasa tunaagiza miundombinu ya maji ya kunawa irudishwe na itumike kama kawaida,wanafunzi wawe na barakoa angalau mbili au tatu ambazo zitamwezesha kufua na kubadilisha.’amesema Prof.Makubi

Prof. Makubi amesema Serikali inalazimika kuwakumbusha viongozi wa shule na Taasisi za Elimu kuimarisha mifumo ya malezi kwenye mabweni, kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara kuhusu afya za wanafunzi.

“Mambo muhimu ni viongozi wa shule na vyuo kuandaa miundombinu ya maji na upatikanaji wa barakoa kama ilivyokuwa mwaka jana na kuchukua hatua stahiki iwapo kutagundulika kuna maambukizi bila hofu wala taharuki” amesema  Prof. Makubi.

Aidha, Prof. Makubi amesisitiza elimu ya kujikinga na ugonjwa huo iendelee kutolewa kwenye maeneo mbalimbali hasa nyumba za ibada, shuleni na vyuoni.

Prof.Makubi amewataka viongozi wote wa mikoa na wilaya kuongeza kasi ya udhibiti na kuhakikisha barakoa zinavaliwa wakati wote watu wanapoingia kwenye taasisi za Serikali .

Pia amewataka viongozi wa dini kuendelea kuelimisha waumini wao katika nyumba za ibada kuhusu kujikinga na ugonjwa huo na kufuata taratibu zote za kujikinga kwa mujibu wa miongozo ambayo imeshatolewa na serikali .

Aidha Prof.Makubi amesema kuwa serikali imeanza mchakato wa kutengeneza chanjo ya Virusi vya Corona  hapa nchini ili kupunguza gharama ya kuagiza nje ya nchi  na kuzifanya ziwe karibu na wananchi.

“Wataalamu tunao wengi na kiwanda hicho hakitatengeneza chanjo ya UVIKO 19 pekee, hata ikiisha tutaendelea kuzalisha chanjo nchini” amesema Prof. Makubi.

Aidha, Prof. Makubi amesema Serikali haina mpango wa kuwauzia wananchi chanjo ya ugonjwa UVIKO 19 wala kuruhusu mtu yeyote kuingiza chanjo hiyo kinyume na utaratibu utakaowekwa.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Elimu Prof. Carolyne  Nombo amesema Wizara kwa kushirikiana na Tamisemi itasimamia miongozo hiyo iliyotolewa na Wizara ya Afya. 

“Miundombinu yote ifufuliwe ikiwemo matumizi ya vitakasa mikono, barakoa asilia na maji yanayotiririka” amesisitiza Prof. Carolyne.