Home Mchanganyiko RPC SINGIDA ASISITIZA UMUHIMU WA MABASI YA MASAFA MAREFU KUWA NA MADEREVA...

RPC SINGIDA ASISITIZA UMUHIMU WA MABASI YA MASAFA MAREFU KUWA NA MADEREVA WAWILI

0

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stella Mutabihirwa    akiwa ndani ya moja ya mabasi alilolikagua akitoa elimu kwa abiria juu ya haki na wajibu wao Stendi Kuu ya Misuna mjini hapa juzi. kabla ya kuendelea na safari yake 

 

Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Singida , akielekea kwenye moja ya mabasi eneo la Stendi Kuu Misuna ili kwenda kulikagua.

 

Na Abby Nkungu, Singida

 

KAMANDA wa polisi mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi Stella Mutabihirwa amewataka wamiliki wa mabasi yanayofanya safari za masafa marefu ndani na nje ya nchi kuhakikisha kila gari linakuwa na madereva wawili ili kupunguza idadi ya ajali za barabarani zisizokuwa za lazima.

Kamanda Mutabihirwa alitoa agizo hilo wakati wa mwendelezo wa  kila mwezi wa jeshi hilo kukagua magari ya abiria  eneo la Kituo kikuu cha mabasi Misuna mjini hapa unaolenga kubaini matatizo mbalimbali na kuyarekebisha kwa manufaa ya usalama wa abiria na mustakabali wa Sheria za usalama barabarani. 

“Dereva ni binadamu na binadamu huchoka na kupoteza uwezo wake wa kumudu vyema gari; hasa anapoendesha kwa muda mrefu bila kupumzika, mwisho analiangusha. Ili kuepuka ajali za aina hii, wamiliki lazima waajiri madereva wawili kwa kila gari linaloenda masafa marefu kwa ajili ya kupokezana njiani” alieleza na kutoa angalizo; 

Kwa ninyi madereva, nawakumbusha Singida ndio Kituo cha kupokezana usukani. Tutakuwa tukikagua kuona iwapo mnazingatia agizo hili. Endesheni kwa kufuata alama za barabarani na kumbukeni mnabeba roho za watu; hivyo hakuna sababu ya kufukuzana njiani ili kumpita mwenzako”. 

Aidha, Kamanda huyo aliwaagiza wamiliki hao kuyapeleka mabasi yao Kituo cha polisi kilicho karibu kwa ajili ya kukaguliwa kabla ya kuanza safari yoyote ili kuingia barabarani yakiwa katika ubora unaokubalika kisheria. 

Baadhi ya madereva waliohojiwa walitoa mwito kwa mamlaka zinazohusika kurejesha alama zote za barabarani zilizong’olewa, kuharibiwa au kuibwa na watu wasio waaminifu ili kuzuia ajali zinazoweza kuepukika. 

Nao wengi wa abiria wameipongeza hatua ya polisi kukagua mabasi katika Stendi kuu hiyo kisha kutoa elimu kwa madereva kabla ya kuwaruhusu kuendelea na safari zao wakisema hiyo itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa madhara yanayoweza kujitokeza barabarani.

“Wanachofanya polisi hapa Singida ni kutukumbusha wajibu wetu tukiwa barabarani. Kwa kweli ni jambo jema sana. Tunachoomba, alama zote muhimu za barabarani ambazo zimeondolewa na watu wenye nia mbaya zirudishwe kwa manufaa ya watumiaji wote wa barabara zetu” alisema dereva Mussa Shikobe.

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi wa mkoa, jumla ya mabasi na malori 1,900 yamekaguliwa katika kipindi cha mwezi mmoja, 223 yalikamatwa na wahusika kupewa onyo, baadhi yao kufikishwa mahakamani huku magari 15 yakifungiwa baada ya kubaini yakiwa na matatizo makubwa ambayo yangeweza kusababisha ajali.