Home Mchanganyiko RC DKT. SENGATI AONYA WATUMISHI WATAKAO ZOROTESHA MAENDELEO SHINYANGA

RC DKT. SENGATI AONYA WATUMISHI WATAKAO ZOROTESHA MAENDELEO SHINYANGA

0

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga katikati akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wapya wa Wilaya waliofika ofisini kwake jana kwa lengo la kujitambulisha na kuanza kazi katika vituo vyao vipya vya kazi.

Sehemu ya wadau wa Mkoa wa Shinyanga waliofika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kushiriki makaribisho ya Wakuu wa Wilaya wapya wa Wilaya zinazounda Mkoa wa Shinyanga.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akiongea na  wadau wa Mkoa wa Shinyanga waliofika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kushiriki makaribisho ya Wakuu wa Wilaya wapya wa Wilaya zinazounda Mkoa wa Shinyanga.

…………………………………………………………………………

Na Anthony Ishengoma -Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati amesema hatakuwa mvumilivu kwa viongozi na watumishi wa umma watakaoshindwa kusimamia na kusababisha kuzorota kwa maendeleo ndani ya Mkoa wa Shinyanga.

Dkt. Sengati alisema hayo jana wakati akiwakaribisha viongozi Wakuu wa Wilaya wapya wa Wilaya za Kishapu na Kahama waliofika katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa kujitambulisha mbele yake lakini pia pia mbele ya wadau mbalimbali wa walioko mkoa wa Shinyanga.

‘’Sitavumilia, nitahakikisha natumia mbinu zote kuhakikisha wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria taratibu na kanuni za kiutumishi lakini pia hatua za kinidhamu kwasababu watanzania ni wengi wenye uwezo wa kuwahudumia wananchi.’’Alisisitiza Dkt. Sengati Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Aidha Dkt. Sengati aliwataka Wakuu wa Wilaya wapya kufanya tathimini ya kina ili kuja na mikakati ya kuendeleza Shinyanga kama mkoa wa kimkakati na inayoendana na Tanzania ya uchumi wa kati lakini pia ulimwengu wa kidijitali ili kudhibitisha kuwa wao ni viongozi wa karne hii ya Sayansi ya na Teknolojia.

‘’Napenda kuona mahusiano makubwa ya utajiri wa Mkoa wetu na ubora wa maisha ya wana Shinyanga, natamani kilimo,madini na mifugo takribani milioni nne, biashara kubwa na uwekezaji ulioko Shinyanga uhakisiwe katika ubora wa maisha ya watu wa Shinyanga.’’ Alisisitiza Dkt. Sengati.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu aliyemaliza muda wake Bi. Nyamaganga Taraba akitoa maoni yake wakati wa kuaga wajumbe wa mbalimbali waliohudhuria afla hiyo fupi alisema ukiona umeteuliwa ujue kuna kazi unayoenda kufanya na ukiona umetenguliwa ujue kuna kazi umekamilisha.

Bi. Taraba alisema kuwa kazi waliyotumwa wameikamilisha kwani wameiacha Shinyanga ambayo sio jangwa tena, wamepunguza tatizo la mimba na ndoa za utotoni lakini pia ujenzi wa vyumba vya madarasa na kuwaomba viongozi wapya kuendeleza yale mazuri waliyoyaacha na kuwataka kuendana na watu washinyanga ambao ni wasikivu wanaotoka kuendana nao sawa.

Wakati huo Mkuu mpya wa Wilaya ya Kahama Bw. Festo Kiswaga amehaidi kuja na mkakati wa kupunguza umasikini kwa watu wenye maisha duni na kuweka mikakati itayowainua maisha yao ili waweze ujiona na wao wana nguvu ya kuendana na soko la kiushindani lililopo.

‘’Unapomwondoa mtu katika umasikini maana yake unataka naye awe sehemu ya nguvu ya soko na awe na uwezo wa kununua na hivyo aweze kuchangia katika ujenzi wa uchumi tunataka Kahama inayokuwa na nguvu kubwa ambayo kila mmoja anaweza kuingia sokoni. Hivi karibuni Serikali ya awamu ya Sita imefanya mabadiliko katika uongozi wa Wilaya mbalimbali nchini na katika mabadiliko hayo Mkoa wa Shinyanga ulibata madiliko ya viongozi hao kwa Wilaya zake mbili za Kishapu pamoja na Kahama.