Home Mchanganyiko PSSSF NA BENKI YA AZANIA ZAZINDUA HUDUMA YA KUWAWEZESHA WANANCHI KUMILIKI NYUMBA...

PSSSF NA BENKI YA AZANIA ZAZINDUA HUDUMA YA KUWAWEZESHA WANANCHI KUMILIKI NYUMBA NA VIWANJA KWA GHARAMA NAFUU

0

 NA
KHALFAN SAID

MFUKO
wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Benki ya Azania, wamezindua
huduma ya kuwawezesha wanachama wa Mfuko huo na wananchi kwa ujumla kuweza
kumiliki nyumba kwa kulipa kidogokidogo.

Uzinduzi
huo umefanyika jijini Dar es Salaam Juni 21, 2021 ambapo taasisi hizo mbili
kupitia Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba na Mkurugenzi Mtendaji wa
benki ya Azania Bw. Charles Itembe walisaini makubaliano yatakayowawezesha
wananchama na wananchi kukopa kutoka benki hiyo kupitia mikopo ya makazi yaani (Mortgage
loan) ili kununua nyumba na viwanja vinavyomilikiwa na PSSSF  kupitia uwekezaji iliyoweka sehemu mbalimbali
nchini.

CPA.
Kashimba alisema mradi wa nyumba za gharama nafuu upo Dar es Salaam, Morogoro,
Shinyanga, Tabora, Mtwara na Iringa na mradi wa viwanja vya gharama nafuu viko
katika mikoa ya Ruvuma, Kagera, Tabora, Iringa, Katavi, Morogoro, Dar es
Salaam, Rukwa, Lindi na Mtwara.

“Kupitia
makubaliano haya, wanachama wa Mfuko pamoja na wananachi wengine watafaidika
kwa kukopeshwa nyumba na viwanja kwa riba ndogo ya asilimia 10% kwa mwaka na
hivyo kuimarisha na kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kwenye maeneo hayo
ili wawe na makazi bora na kutimiza kauli mbiu ya serikali ya nyumba bora kwa
wananchi wote inawezekana.” Alibainisha CPA, Kashimba.

Akifafanua
zaidi kuhusu masharti ya kukopa nyumba na viwanja Mkurugenzi Mkuu huyo alisema,
mteja atalazimika kuweka rehani ya asilimia 10% ya thamani ya mkopo au mali ya
thamani hiyo kwa dhamana ya mkopo na kiwango cha juu kabisa ambacho mteja
anaweza kukopwa na benki ni asilimia 90% ya thamani yote ya nhyumba au kiwanja.

“Mteja
atakapokamilisha malipo yake atakabidhiwa hati yake ya nyumba au kiwanja na
benki ya Azania na muda wa marejesho ya mkopo ni kipindi kisichozidi miaka 15
kwa mkopo wa nyumba na miaka miwili kwa mkopo wa kiwanja.” Alifafanua CPA.
Kashimba.

Alisema
katika makubaliano hayo jumla ya nyumba 192 na viwanja 886 vyenye hati vitakuwa
sokoni na vitauzwa kwa mkopo wenye riba nafuu kwa wanachama na wananchi  kwa kuzingatia vigezo na masharti mepesi
yaliyowekwa na waitaji watapata fursa ya kutembelea na kuona viwanja hivyo.

Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Azania, Bw. Charles Itembe,
ameupongeza Mfuko wa PSSSF kwa kubuni mradi huo mkubwa wenye tija kubwa kwa
taifa kwa Wanachama na wasio wananchama wa PSSSF.

“Kama
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii umeonyesha nia njema inayolenga kumuinua mwananchi kwa
vitendo na sio kwa maneno tu.” Alisema,

Alisema
Benki ya Azania inaona faraja kuwa sehemu ya mradi kwani ina uzoefu wa miaka mingi wa ukopeshaji wa nyumba Tanzania.

“Benki imeanza
kutoa mikopo hiyo toka mwaka 2005 wakati huo mabenki mengine yalikuwa bado
hayajaanza kufanya kazi hiyo.” Alisema.

Alisema
ushirikiano huo benki na PSSSF sio jambo la kwenda kuiga kwani ni jambo ambalo
wameshawahi kulifanya na kutoa manufaa makubwa kwa watu wengi na kujenga
heshima kubwa sana huko mtaani.

“Napenda
niwahakikishgie watanzania wanaokuja kuomba mikopo ya nyumba au viwanja, tuko
tayari kuwahudumia na mikopo hii inatolewa kwa asilimia 10%, hakika ni riba
ambayo ni ndogo sana.” Aliwahakikishia wahitaji.

Akifafanua
zaidi alisema mtu atakayekopa atakuwa na muda mrefu wa kutosha kulipa
kidogokidogo na anaweza kuwa tayari anakaa kwenye nyumba yake huku akiendelea
kulipia.

“Mkopo
huu utakuwa na bima ya mkopo kupitia huduma ya bank assurance inayotolewa na
benki ya Azania, kwa hivyo nyumba yako itakuwa salama kwa majanga mbalimbali
yanayoweza kusababishwa na moto au mafuriko.” Alisema Bw. Itembe.

 

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba(kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Azania Bw. Charles Itembe wakionyesha mikataba hiyo baada ya kusaini

 

 

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba(kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Azania Bw. Charles Itembe wakisaini makubaliano ya kuwawezesha wananchi kumiliki nyumba na viwanja kwa gharama nafuu.

 

 

Baadhi ya wakurugenzi wa PSSSF na benki ya Azania walioshuhudia uzinduzi huo.

 

 

 

 

Mkurugenzi wa Uwekezaji mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, Bw. Fortunatus Magambo 

 

 

 

Mkurugenzi wa Uwekezaji mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, Bw. Fortunatus Magambo (aliyesimama) akitoa neno la utangulizi. Wengine kutoka kulia ni CPA. Kashimba, Bw. Itembe na Meneja Mwandamizi wa Wateja  Binafsi Bw. Jackson Lolai 

 

 

Picha ya pamoja