Home Mchanganyiko WAZIRI MKENDA AZINDUA MRADI WA AGRI CONNECT JIJINI MBEYA WENYE THAMANI YA...

WAZIRI MKENDA AZINDUA MRADI WA AGRI CONNECT JIJINI MBEYA WENYE THAMANI YA BILIONI 277

0

 

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akizungumza wakati akizindua Programu ya AGRI CONNECT iliyofanyika katika ukumbi wa Highland Hotel Jijini Mbeya, tarehe 21 Juni 2021. (Picha Zote Na Mathias Canal)

 

 

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akizindua Programu ya AGRI CONNECT iliyofanyika katika ukumbi wa Highland Hotel Jijini Mbeya, tarehe 21 Juni 2021. wengine pichani wakishuhudia tukio hilo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji Mhe Dkt. Christine Ishengoma na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe Omary Mgumba.

 

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akijadili jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Juma Homera wakati wa hafla ya uzinduzi wa Programu ya AGRI CONNECT iliyofanyika katika ukumbi wa Highland Hotel Jijini Mbeya, tarehe 21 Juni 2021.

 

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda (Kushoto) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Juma Homera (Katikati) mara baada ya kuwasili Ofisini kwake Jijini Mbeya akiwa katika ziara ya kikazi, Tarehe 21 Juni 2021. Mwingine pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe Omary Mgumba (Kulia).

 

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Juma Homera akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Programu ya AGRI CONNECT iliyofanyika katika ukumbi wa Highland Hotel Jijini Mbeya, tarehe 21 Juni 2021 ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda.

 

Sehemu ya washiriki wa mkutano wa AGRI CONNECT wakisikiliza kwa makini hotuba ya mgeni rasmi-Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda wakati akizindua Programu ya AGRI CONNECT iliyofanyika katika ukumbi wa Highland Hotel Jijini Mbeya, tarehe 21 Juni 2021.

 

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akizungumza wakati akizindua Programu ya AGRI CONNECT iliyofanyika katika ukumbi wa Highland Hotel Jijini Mbeya, tarehe 21 Juni 2021.
 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mbeya

 

Shabaha ya serikali ni kuhakikisha utafiti wa mbegu bora unaimarishwa, kuongeza uzalishaji wa mbegu lakini pia kuboresha utoaji wa huduma za ugani.

 

Katika mpango huo, maeneo mengine yatakayoangaliwa ni pamoja na kilimo cha umwagiliaji hususani katika uzalishaji wa mbegu ili kuweza kujitosheleza kwa mbegu mwaka mzima; kuimarisha upatikanaji wa suluhu katika masoko ya mazao ya kilimo; kuimarisha Kilimo Anga ili kudhibiti visumbufu vihamavyo pamoja na kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa mitaji na ugharamiaji wa sekta ya kilimo.

 

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 21 Juni 2021 wakati akizindua Programu ya AGRI CONNECT uliofanyika Jijini Mbeya.

 

Itakumbukwa kuwa Mwaka 2018, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilisaini Mkataba wa Ugharamiaji (Financing Agreement) na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya wa utekelezaji wa Programu ya AGRI-CONNECT wenye thamani ya Euro milioni 100 sawa na takribani Shilingi bilioni 277 ambazo ni ruzuku (grant) kutoka Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.

 

Aidha, kiasi cha Euro milioni 3.5 sawa na Shilingi bilioni 9.6 zimechangiwa na wadau wanaotekeleza programu hii ya AGRI-CONNECT na kufanya mahitaji ya rasilimali kuwa Euro milioni 103.5 sawa takribani bilioni 287 kwa kipindi cha miaka miaka minne kuanzia mwaka 2019/2020 hadi 2023/2024 ambapo utekelezaji wake ulianza Februari, 2019 kwa hatua za awali.

 

AGRI-CONNECT imechagua maeneo machache ya kipaumbele yenye kugusa watu wengi kwa kuzingatia mnyororo wa thamani (agricultural value chain) wa mazao ya kahawa, chai na mazao ya Bustani ambapo wakulima wadogo wapatao 150,000 wa mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe, Katavi, Iringa na Ruvuma watanufaika.

Waziri Mkenda ameitaka AGRI-CONNECT ijikite katika kuongeza uzalishaji na tija kwenye mazao haya iliojiwekea kuwa ni ya kipaumbele na kutafuta suluhu ya tatizo la masoko. Kama itatekeleza vizuri AGRI-CONNECT, kuwa uzalishaji wa mazao utaongezeka.

 

Kuhusu ujenzi wa miundombinu, hususani ya usafiri. Waziri Mkenda ameutaka Wakala wa Ujenzi wa Miundombinu ya Barabara Vijijini (TARURA) kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara za vijijini hususani barabara zinazounganisha maeneo ya uzalishaji na masoko.

Kadhalika Waziri Mkenda ametoa mwito kwa sekta binafsi kuhakikisha AGRI-CONNECT inatekelezwa. “Serikali ni lazima ishirikiane na Sekta binafsi. Hivyo basi, mamlaka zote za mikoa ya nyanda za juu kusini na Mamlaka zingine zote husika zishirikiane na Sekta binafsi kwenye mnyororo wa thamani wa mazao yote ya kilimo hususan Kahawa, Chai na mazao ya bustani. Katika mazao haya kuna fursa nyingi ambazo sekta binafsi inaweza kunufaika nazo, ikiwa ni pamoja na kujenga viwanda” Amekaririwa Prof Mkenda

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Juma Homera amesema kuwa mradi huo wa AGRI CONNECT unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya ni muhimu hapa nchini kwani itakuwa sehemu ya kupambana na utapiamlo na udumavu ambao kiwango chake ni kikubwa.

“Kiwango cha udumavu na utapiamlo ni kikubwa sana hapa nchini ambapo mkoa wa Ruvuma ni asilimia 41%, Iringa 47.1%, Mbeya 33.8%, Njombe 53.6%, Songwe 43.3% na Katavi 73.7% hivyo tunaamini mradi huu utamaliza kama sio kupunguza tatizo hilo” Amesisitiza Rc Homera

Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe Omary Mgumba amesema kuwa Mkoa wa Songwe unashika nafasi ya tatu kwa kilimo cha kahawa nafasi ya tatu katika uzalishaji wa mazao ya chakula.

Amesema pia pamoja na kushika nafasi hizo nzuri za kiuongozi katika sekta ya chakula lakini bado mkoa huo upo katika nafasi mbaya kwa kuongoza kwa wananchi kuwa na utapiamlo pamoja na udumavu.

“Hivyo mradi huu unakuja kuwasaidia wakulima wenzangu hususani wa kahawa kwani jinsi mpango ulivyo utaimarisha sekta mbalimbali ikiwemo barabara kwa ajili ya kuboresha urahisi wa kuyafikia masoko ya mazao ya wakulima” Amekaririwa Mhe Mgumba

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe Dkt. Christine Ishengoma (Mb) amesema kuwa mradi huo utakaotengeneza barabara za vijijini utarahisisha usafirishaji wa mazao ya wakulima nchini.

Amesema kuwa ni matarajio makubwa kwa bunge na serikali kwa ajira zitakazotolewa kwa vijana na kina mama kwa ajili ya kujikimu katika mahitaji yao katika familia zao.