Home Mchanganyiko WAZIRI MKUU AKIPONGEZA KIWANDA CHA AFRICAB KWA UWEKEZAJI BORA

WAZIRI MKUU AKIPONGEZA KIWANDA CHA AFRICAB KWA UWEKEZAJI BORA

0

***********************************

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameupongeza uongozi wa kiwanda cha kuzalisha vifaa mbalimbali vya umeme cha AFRICAB kutokana na uwekezaji wake kwenye sekta ya nishati na kusisitiza umuhimu wa mamlaka za Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo alipofanya ziara ya kukitembelea  kiwanda kwa lengo la kuangalia uzalishaji wake ambapo pamoja na mambo mengine alisema uwepo wa kiwanda hicho nchini imeisaidia Serikali kuondokana na gharama kubwa za uagizaji wa vifaa  vya umeme kutoka nje ya nchi ambazo zikiigharimu Serikali.

Alisema uwekezaji wa kiwanda hicho, mbali na kuipunguzia Serikali mzigo wa gharama, pia umesaidia kuharakishwa kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme nchini ikiwemo ya REA hatua inayoendelea kuliletea maendeleo Taifa na hivyo kusisitiza haja ya wawekezaji hao kuendelea kuthaminiwa.

“Zamani fedha nyingi zilikuwa zinatumika katika kuagiza vifaa mbalimbali vya umeme kutoka nje ya nchi, kwa sasa vifaa vingi vinazalishwa hapa hapa nchini zikiwemo zinazozalishwa na kiwanda hiki, naami kadri siku zinavyokwenda uwekezaji huu utakuwa  hivyo kuzidi kulilete tija taifa, kikubwa mamlaka zinazosimamia suala zima la uwekezaji kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wenye nia ya kutaka kuwekeza hapa nchini” alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Alisema miradi mingi ya umeme inayoendelea kutekelezwa hivi sasa hapa nchini imekuwa ikitumia transfoma  pamoja na nyaya zinazozalishwa na kiwanda hicho cha AFRICAB suala alilosema kuwa limekuwa faraja kwa Serikali kutokana na kiwanda hicho kuiunga mkono Serikali katika jitihada zake za kujiletea maendeleo.

Aidha mbali na uwekezaji huo, Majaliwa pia aliupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kuwa  mmoja wa walipakodi wazuri kwa Serikali  kwa kubainisha kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikilipa kodi kiasi cha Sh Bilioni 2 kila mwaka huku kikitoa ajira rasmi kwa watu zaidi ya 1000  walioajiliwa katika maeneo tofauti.

“Serikali inawapongeza kwa hatua hii nzuri iliyotokana na uwekezaji huu na zaidi inawakaribisha wawekezaji wote wenye nia ya kutaka kuja kuwekeza hapa nchini  hasa kutokana na uwepo wa mazingira mazuri yanayofaa kwa uwekezaji” aliongeza Majaliwa.

Kwa upande wake Meneja masoko wa AFRICAB David Tarimo uongozi  wa kiwanda hicho umepokea lwa furaha ziara ya Waziri Mkuu Majaliwa mahali hapo kwa kuwa kutaendelea kukiongezea chachu kiwanda hicho kuongeza nguvu ya uzalishaji.

Alisema wao kama wawekezaji wazalendo  hapa nchini jukumu lao ni kuhakikisha wanaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha sekta ya nishati nchini inakuwa yenye tija kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora zitakawawezesha wananchi kuzitumia kwa muda mrefu.

Alisema changamoto wanayokabiliana nayo ni baadhi ya wananchi kuendelea kuamini bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi ambazo nyingi zimekuwa zikiingizwa kwa njia ya ‘panya’ na zaidi zikikosa ubora ikilinganishwa na bidhaa zinazozalishwa nchini hususani kutoka katika kiwanda hicho.