Home Michezo Ikulu yatinga nusu fainali netibali

Ikulu yatinga nusu fainali netibali

0

*************************************

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

MABINGWA watetezi wa mchezo wa netiboli, timu ya Ofisi ya Rais Ikulu imetinga kwa kishindo hatua ya nusu fainali kwa kuwa timu pekee iliyoshinda michezo yake yote mine kwa makundi yote mawili ya michezo ya michuano ya Kombe la Mei Mosi inayofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

Mbali na pointi hizo pia Ikulu imemaliza ikiwa na magoli mengi 166 ya kufunga; ambapo wamefuatiwa na Uchukuzi wenye pointi sita na magoli 124 ikiwa nayo imeingia hatua ya nusu fainali wote wakiwa kwenye kundi A; wakati timu za kundi B zilizofuzu hatua hiyo ni Wizara ya Mambo ya Ndani ikiwa na pointi sita na magoli 128 wakifuatiwa na Tanesco yenye pointi nne na magoli 118.

Kutokana na matokeo hayo sasa Ikulu itakutana na Tanesco; huku Mambo ya Ndani watacheza na Uchukuzi katika hatua hiyo itakayofanyika tarehe 27 April, 2021.

Kwa upande wa soka timu za Tanesco na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wametinga hatua hiyo wakimaliza kundi A wakiwa wote wanapointi tisa, lakini wanatofautiana katika magoli ya kufungwa pekee; huku kundi B zimefuzu timu za Uchukuzi na TPDC wote wakiwa na pointi 10 lakini wanazidiana katika magoli ya kufunga na kufungwa.

Katika michezo iliyochezwa leo kwa upande wa soka NCAA waliwafunga MWAUWASA magoli 19-0 yaliyofungwa na Emmanuel Kabanyama manne; huku Regan Peter na Tumainiel Sandemu kila mmoja alifunga magoli matatu, nao Liberatus Rwechungura, Detrum Mwakyalaba na Brown David kila mmoja alifunga magoli mawili, pia Vicent Ngowo, Jacob Panga na Aidan Frank walifunga goli moja kila mmoja.

Nayo Tanesco walifungwa na RAS Mwanza kwa magoli 3-2. Magoli ya RAS yalifungwa na Fuma Kapeji mawili na Peter Mumbar goli moja, na ya Tanesco wamefunga na Ibrahim Said na Kurwa Mangara.

Katika michezo iliyofanyika uwanja wa Nyamagana, Uchukuzi iliendeleza wimbi la ushindi kwa kuwafunga Mwanza Jiji kwa magoli 4-0, yaliyofungwa na Joseph Paul, Rahim Ayesh, Mrisho Harambe na Idrisa Bahatisha. Nao TPDC waliwashinda Wizara ya Kilimo kwa magoli 2-0 yaliyofungwa na Barnabas Mwashambwa na Daruweshi Shija.

Katika netiboli timu ya Uchukuzi iliwashinda TPDC kwa magoli 36-25. Hadi mapumziko washindi walikuwa na magoli 20-0; nayo Wizara ya Mambo ya Nje iliwafunga MWAUWASA kwa magoli 16-6, yaliyofungwa na Patricia Kiswaga 12 na Jureck Mbise manne, wakati Salome Emmanuel na Neema Maleko kila mmoja alifunga sita kwa MWAUWASA.

Michezo ya kuvuta Kamba wanaume NCAA waliwashinda Wizara ya Habari (2-0); huku Chuo cha Mipango na Wizara ya Kilimo walitoka sare ya 1-1; Tanesco walipata ushindi wa chee dhidi ya PSSSF; nayo Habari walishindwa mbele ya Ukaguzi (2-0) na Mipango waliwavuta Nje (2-0); wakati kwa upande wa wanawake Taasisi ya Saratani Ocean Road waliwashinda Tanesco (2-0); TPDC waliwavuta NCAA (2-0); Wizara ya Habari waliwavuta MWAUWASA (2-0); TPDC wakawashinda Habari (2-0) na Tanesco wakapoteza tena kwa Mipango (2-0).

Michuano hiyo itaendelea kesho kwa michezo yam bio za kilometa 15 kwa wanaume na kilometa nane wakawake zitakazoanzia Igoma Stendi ya Magu hadi Sabasaba; pia kutakuwa na michezo ya bao, karata, na draft