************************************
RUNGWE
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema inaona kuna fursa kubwa ya kuwajengea uwezo wafugaji katika maeneo mbalimbali ili kujua uendelezaji wa malisho bora ambayo yatamuhakikishia mfugaji kuwa na afya bora lakini pia kuongeza kipato cha kaya.
Hayo yamesemwa wilayani Rungwe mkoani Mbeya na Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo, na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angelo Mwilawa wakati akizungumza na SUA Media
Dkt. Mwilawa amesema kuwa hatua hiyo ya kuwaendeleza wakulima imekuwa ni muendelezo wa maagizo kutoka kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Mashimba Ndaki ambaye amekuwa akitaka kuhakikisha Wizara anayoongoza inatoa elimu ya kutosha kwa wakulima
Akizungumzia malisho ya nyasi aina ya Brachiaria ambazo zimefanyiwa utafiti na watafiti kutoka Mradi wa Innove Afrika ulio chini ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dkt. Mwilawa amesema ni Mradi wenye mafanikio makubwa na kuwataka wafugaji katika wilaya hiyo na kote nchini kuhakikisha wanaendeleza teknolojia hiyo kwa kupanda na kustawisha nyasi hizo
“Na hili ambalo tumeliona, aina hii ya malisho ya Brachiaria ni moja ya aina ya nyasi za malisho ambazo zimefanyiwa utafiti nchini lakini kwa sasa tumeona aina hii ya malisho ina ubora mkubwa katika kuleta lishe bora kwa mifugo”, amesema Dkt. Mwilawa
Naye mmoja wa watafiti katika Mradi huyo Dkt. Ismail Suleiman amesema kuwa teknolojia hiyo imepokewa vizuri na wafugaji wengi wilayani Rungwe mkoani Mbeya kwani kwa sasa wafugaji wameamka na kuanza kupanda malisho hayo
Amesema mradi ulianza na wafugaji wachache lakini kwa sasa idadi imekuwa ikiongezeka siku hadi siku kiasi kwamba wapo wafugaji waliamua kupanda malisho hayo wakati wa kiangazi na kumwagilia kwa maji ili kuhakikisha wanakuwa na malisho hayo
Mmoja wa wanufaika ambaye aliamua kupanda wakati wa kiangazi Bw. Anyabwile Asa Mwakosya amesema awali alikuwa akichukua nyasi porini na kwa kiasi kikubwa zilileta madhara kwa mifugo yake
“Awali nilikuwa nikikata majani porini na wakati mwingine ng’ombe alipokula mimba ilikuwa na uwezo wa kutoka na hata sikujua kwa nini, lakini kwa sasa tangu nianze kutumia nyasi hizo wanyama wangu mimba huenda kwa wakati muafaka pasipo kuvurugwa”, amesema Mwakosya
Mradi wa Innove Afrika unajumuisha nchi sita barani Afrika zikiwemo nchi za Tanzania na Kenya.
Nacho Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimesema kinajivunia kwa kiasi kikubwa kuwa mshiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ile inayonyanyua na kuboresha maisha ya watu moja kwa moja kwa kuinua kipato na kuongeza afya kwa watanzania
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam Prof. Esron Karimuribo ambaye amemwakilisha Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA upande wa Taaluma Prof. Maulid Mwatawala wakati akifungua warsha ya siku moja iliyofanyika April 14, 2021 ya kisera katika kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa chakula, Mradi ujulikanao kwa jina la ‘INNOVE AFRICA’
Prof. Karimuribo amesema ushiriki wa SUA katika Mradi huu unasaidia kufanikisha malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mkakati namba mbili wa kidunia katika kuhakikisha inaondoa baa la njaa hadi ifikapo mwaka 2030
“Mradi huu ulijikita katika kuhakikisha unapanua kilimo hiki cha nyasi hizi za Brachiaria kama njia mbadala ya kuweza kupata malisho bora ambayo yataongeza uzalishaji wa maziwa yenye ubora zaidi na kwa hivyo kupitia uzalishaji huo basi mfugaji anapouza maziwa anaongeza kipato lakini pia yakitumiwa na wanajamii yanaongeza lishe”, amesema Prof. Karimuribo
Akizungumzia matokeo ya utafiti huo ambao ulikuwa unaangalia namna bora ya kukuza nyasi aina ya Brachiaria ili kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini, Mradi unaofanyika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya Mratibu wa Mradi huo Prof. Dismas Mwaseba amesema wao kama watafiti wameona mbegu aina ya Brachiaria inastawi zaidi katika Ukanda huo wa Nyanda za Juu Kusini na kwa kiasi kikubwa unaweza kuwa msaada kwa wafugaji katika eneo hilo
Aidha amesema kuwa kupitia Jukwaa la Ubunifu na Jukwaa la Wafugaji wa ng’ombe kama litatumiwa vizuri lina uwezo wa kueneza kilimo hiki chenye manufaa makubwa kwa wafugaji na hasa katika kuhakikisha kilimo kinaendelea kikiwemo kilimo cha nyasi
Nao wakulima mbalimbali wanaoshiriki katika Mradi huu wamesema kwa sasa wanaona manufaa ya mradi huo na hasa baada ya ongezeko la uzalishaji wa maziwa na upatikanaji wa nyasi hizo tofauti na awali
Mfugaji Bibi Mehne Mwasumbi na Stanley Salingo wamesema tangu walipopanda nyasi hizi wamekuwa na raha wakati wote kwani kwa upande wa Mwasumbi hata kama mumewe hayupo hutoka tu nje ya nyumba yao na kukata nyasi na kulisha ng’ombe lakini pia anaona tofauti ya maziwa ambapo kwa sasa ubora wake umeongezeka kwa kiasi kikubwa