………………………………………………………………………………

UJENZI wa Jengo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma ambalo limegharimu zaidi ya shilingi bilioni mbili limekamilika na kuanza kutumika.

Akitoa taarifa hiyo ofisini kwake Mhandisi wa Halmashauri hiyo Ludger Nchimbi  amesema  ujenzi wa jengo hilo, ulianza rasmi mwaka 2017  na kwamba mradi umejengwa kwa awamu tatu.

 Amesema katika awamu ya kwanza mkataba  ulikuwa unatekelezwa na Mkandarasi Wakala wa Majengo Tanzania TBA,ambao uligharimu zaidi ya shilingi milioni 493,awamu ya pili ni mkataba wa zaidi ya bilioni mbili na  awamu ya tatu ujenzi umefanyika kwa force akaunti kwa ajili ya umaliziaji  wa mradi huo. 

“Tulipokea fedha kutoka serikali kuu Bilioni tatu ambazo zimetumika kutoka mapato ya ndani, fedha iliyotumika mpaka kukamilika Jengo shilingi zaidi ya shilingi bilioni mbili’’,alisema.

Hata hivyo Mhandisi amesema Mkandarasi TBA alisimamishwa kuendelea na kazi ya ujenzi  na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina  Mndeme Juni 6 mwaka huu,baada ya Mkandarasi huyo kupata changamoto ya kufungiwa akaunti zake zote na kushindwa kuendelea na kazi,hali iliyosababisha Halmashauri kutumia force akaunti kukamilisha mradi huo.

Amesema mradi wa jengo hilo kwa sasa limekamilika na tayari  limeanza kutumika kuanzia Oktoba 21, 2020.