Home Mchanganyiko SERIKALI YA JPM YAZIBANA KAMPUNI ZINAZOUMIZA WATUMISHI NA WASTAAFU KWA KUTOZA RIBA...

SERIKALI YA JPM YAZIBANA KAMPUNI ZINAZOUMIZA WATUMISHI NA WASTAAFU KWA KUTOZA RIBA KUBWA

0

Mkuu wa Mkoa wa Singida (RC) Dkt Rehema Nchimbi
akimkabidhi Mwalimu Mstaafu kutoka
Wilaya ya Singida  Amosi Njoghomi kiasi cha shilingi milioni 18.8 zilizookolewa kutoka kwa mmoja wa wakopeshaji wa ‘Riba Umiza.’ Mwalimu Njoghomi
alikopa shilingi milioni 2, lakini mkopeshaji alimtaka arejeshe fedha taslimu
shilingi milioni 31 hadi serikali ilipoingilia kati na kumsaidia. 

Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Singida,
Suzan Shesha (kulia) akishuhudia tukio la Mwalimu Njoghomi kukabidhiwa pesa
zilizookolewa. Kushoto ni Mwenyekiti Mstaafu wa CWT mkoa wa Singida, Aran Jumbe.

Familia ya Mwalimu Mstaafu Albert Mpahi ikipokea
kiasi cha shilingi milioni 2 zilizookolewa kutoka kwa moja ya Kampuni za Mikopo
zisizofuata utaratibu. Mwalimu Mpahi alikopa shilingi milioni 7.2 na mkopeshaji
wake akamtaka arejeshe fedha taslimu Shilingi Milioni 17 hadi serikali
ilipoingilia kati.

RC Nchimbi akimkabidhi Mwalimu Mstaafu kutoka Wilaya ya Ikungi  Gerase Mshumbusi kiasi cha shilingi milioni 13 zilizookolewa
kutoka kwa mmoja wa wakopeshaji
wa ‘Riba Umiza.’ Mwalimu Mshumbusi alikopa shilingi milioni 3.5, lakini
mkopeshaji alimtaka arejeshe fedha taslimu shilingi milioni 17 hadi serikali ilipoingilia
kati na kumsaidia.

Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Singida
Suzan Shesha (kushoto) akishuhudia tukio la Mwalimu Gerase Mshumbusi
kukabidhiwa pesa zilizookolewa. Kulia ni Mwenyekiti Mstaafu wa CWT mkoa wa
Singida, Aran Jumbe.

RC Nchimbi akizungumza na wadau mbalimbali
kutoka kwenye mabenki, Taasisi, Maafisa Utumishi, watu binafsi na Kampuni za
Mikopo kutoka mkoa wa Singida kabla ya zoezi la kurudisha fedha zilizookolewa.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Adili
Elinipenda, akitoa taarifa ya fedha zilizookolewa kutokana na Riba Umiza kwa
kipindi cha Julai hadi Oktoba 2020.

Wadau wakifuatilia mkutano huo .

Mkutano ukiendelea.

Maombi na Dua maalumu kupitia mkutano huo vikifanyika
kwa lengo la kuliombea Taifa la Tanzania na watu wake.

Maombi yakiendelea.

Familia ya Mwalimu mstaafu Albert Mpahi muda
mfupi baada ya kukabidhiwa shilingi milioni 2 zilizookolewa na serikali.

 Na
Godwin Myovela, Singida

 

RAIS John Magufuli amewafuta machozi walimu,
wastaafu na baadhi ya wananchi mkoani hapa kwa kuokoa na hatimaye kuwakabidhi
mali na fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 82 walizokuwa wametapeliwa
kupitia Kampuni za Mikopo zinazoendesha shughuli zake kinyume na utaratibu.

Mkuu wa Mkoa Dk Rehema Nchimbi, kwa niaba ya Rais, amewakabidhi
kiasi hicho cha fedha waathirika wote waliopitiwa na wimbi hilo, maarufu ‘Mikopo
Umiza,’ ofisini kwake leo.

“Ni Serikali hii ya Magufuli ndio iliyofanikisha
kuwabana hawa wakopeshaji haramu na hatimaye leo walimu wangu na ninyi
watumishi wenzangu mnakabidhiwa haki yenu iliyokuwa imeporwa, tuendelee
kumshukuru Rais kwa mema haya anayoendelea kutufanyia,” alisema Nchimbi na
kuongeza:

“Rais Magufuli mda mrefu alishakampeniwa na Mwenyezi
Mungu mwenyewe kupitia Corona, kama Mungu alipitishia kwake ile neema, maono na
uwezo ule wa kusimama bila kutetereka, mimi Rehema Nchimbi ni nani hata
nisiendelee kumsifu?” alihoji.

Akiwasilisha
taarifa ya fedha zilizookolewa kutokana na Riba Umiza katika kipindi cha Julai
hadi Oktoba mwaka huu, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, alisema takribani shilingi
milioni 82.8 pamoja na mali nyingine vimeokolewa na kurejeshwa kwa wahusika.
 

Alisema
matokeo ya ufuatiliaji na udhibiti huo umebaini kuwa baadhi ya wakopeshaji
binafsi wanafanya shughuli hiyo bila ya vibali halali, hali inayosababisha
kukwepa kodi na hivyo kuikosesha serikali mapato na kujipatia fedha isivyo
halali.

Pamoja
na mambo mengine, alisema udhibiti umebaini kuwepo kwa utozaji mkubwa wa riba
zisizovumilika za zaidi ya asilimia 100 kinyume na viwango vilivyowekwa na
kuainishwa na Benki Kuu, sanjari na wakopeshaji kukaa na kadi za benki za
wakopeshwaji kwa lengo la kuchukua fedha kila ifikapo mwisho wa mwezi.
 

Aidha,
kupitia ripoti hiyo iliyowasilishwa na Takukuru, imeelezwa baadhi ya
wakopeshaji hawaandai mikataba ya ukopeshaji, hivyo wakopeshwaji hawana nakala
za mikataba, na hata iliyopo kwa baadhi ya kampuni hizo haikidhi sifa na
vigezo.

“Baadhi
ya kampuni hizi za mikopo hazina hata wataalamu wa mahesabu hali inayowafanya
kutoza riba zenye mkanganyiko, na hivyo kujikuta wakimbambikiza riba kubwa
mkopeshwaji,” ilieleza sehemu ya ripoti hiyo.

Hata
hivyo, Afisa wa Takukuru mkoani hapa, Shemu Mgaya, pamoja na mambo mengine
alisema kuna uvujaji mkubwa wa taarifa za watumishi wanaostaafu. Mathalani
mafao ya mstaafu yanapokuwa yameingizwa benki wakopeshaji wanakuwa wa kwanza
kupata taarifa kabla ya mhusika.
 

“Tumebaini
kwa baadhi ya mabenki kuna ukiukwaji mkubwa wa taratibu za kibenki kupitia
maafisa wao, kwa eneo la kuwezesha kutolewa fedha kutoka akaunti ya mteja
kwenda akaunti ya mkopeshaji bila mwenye akaunti kuwepo,” alisema Mgaya na
kuongeza:
 

“Udhibiti
pia umebaini hata Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imekuwa ikichelewesha mafao kwa
wastaafu hali ambayo inasababisha baadhi ya wastaafu kujikuta wakiingia katika
hii mikopo umiza (mikopo yenye riba kubwa).”
 

Ofisi
hiyo ya Takukuru, hata hivyo inasisistiza kuwa endapo matokeo hayo ya udhibiti
na mapendekezo yatatekelezwa basi ni dhahiri yataleta ustawi kwa wazee na
wastaafu wa Tanzania ikizingatiwa wastaafu ndio ‘Hazina ya Taifa.’

FUATILIA HAPA CHINI TAARIFA ALIYOPOKEA
MKUU WA MKOA KWA NIABA YA RAIS YA KAZI KUBWA YA ILIYOFANYWA NA TAKUKURU KUWABANA
WAKOPESHAJI HARAMU NA KULINDA MASLAHI YA WANYONGE KWENYE WILAYA ZA SINGIDA,
IRAMBA, IKUNGI NA MANYONI KUFUATIA AGIZO LA HIVI KARIBUNI 

 

26
Oktoba, 2020

 

TAARIFA YA FEDHA ZILIZOOKOLEWA NA TAKUKURU
MKOA WA SINGIDA KUTOKANA NA RIBA UMIZA KIPINDI CHA JULAI HADI OKTOBA,2020

MKOA WA SINGIDA.

  1. WILAYA
    YA SINGIDA

a.
Wilaya
ya Singida tumefanikiwa kuokoa kiasi cha Tshs. 18,800,000/= kutoka kwa
Mkopeshaji BISEKO MUNGETA KAZUNGU ambaye alimkopesha Mwalimu Mstaafu AMOSI
NJOGHOMI fedha kiasi cha Tshs.2,000,000/= na kumtaka kurejesha fedha kiasi cha
Tshs. 31,000,000/=.Tunaomba leo Fedha hizi Tshs.
18,800,000/=
uzikabidhi kwa  AMOSI NJOGHOMI.

b.
Wilaya
ya Singida tumefanikiwa kuokoa kiasi cha Tshs. 700,000/= kutoka kwa Mkopeshaji CHARLES
WAWA ambaye alimkopesha Mtumishi Mmoja wa serikali (Jina limehifadhiwa) fedha
kiasi cha Tshs.500,000/= na kumtaka kurejesha fedha kiasi cha
Tshs.1,900,000/=.Fedha hizi zimekabidhiwa kwa mhusika kupitia Akaunti yake huku
tukiendelea kufuatilia fedha iliyosalia.

c.
Wilaya
ya Singida tumefanikiwa kuokoa kiasi cha Tshs. 2,000,000/= kutoka kwa Kampuni
ya BOMANG MICROFINANCE ambayo ilimkopesha Mwalimu Mstaafu ALBERT SUNGI MPAHI
fedha kiasi cha Tshs.7,200,000/= na kumtaka kurejesha fedha kiasi cha
Tshs.17,000,000/=. Tunaomba leo Fedha hizi Tshs.
2,000,000/=
uzikabidhi kwa  ALBERT SUNGI MPAHI, TAKUKURU inaendelea
kufuatilia fedha zilizosalia.

IKUNGI

a.
Katika
 Wilaya ya IKUNGI tumefanikiwa kuokoa
kiasi cha Tshs.17,000,000/= kutoka
kwa mkopeshaji , kampuni ya MAGIREI COMPANY LTD (MICRO CREDIT) ya Singida
mjini. Kampuni hii ilimkopesha Mwalimu Mstaafu GERASE KAJUNA MSHUMBUSI Tsh.3,500,000/=
mwaka 2015 na kulipa Tsh.17,000,000/=
mwaka 2017. Baada ya Ofisi ya TAKUKURU kufanya ufuatiliaji iliitaka
kampuni hii imrejeshee jumla ya Tshs.17,000,000/=. BWANA GERASE KAJUNA
MSHUMBUSI alirejeshewa kupitia kwenye akaunti yake namba 50802500415 iliyopo
katika Benki ya NMB kiasi cha Tsh.4,000,000/=
kati ya tarehe 02/07/2020 na tarehe 03/08/2020. Tunaomba leo Fedha
iliyosalia kiasi cha Tshs. 13,000,000/= uzikabidhi kwa Mwalimu
Mstaafu GERASE KAJUNA MSHUMBUSI .

b.
Kampuni
iitwayo WIDOP COMPANY LTD ilimkopesha kiasi cha Tsh.1,700,000/= Bi. LUCIA PETRO
NYIKA Muuguzi Mstaafu na kurejesha kiasi cha Tsh.5,100,000/=  .Baada ya TAKUKURU kufuatilia Bi. LUCIA PETRO
NYIKA amerejeshewa Tshs.2,400,000/=  tarehe 15/10/2020, na fedha nyingine
zilizobaki zipo kwenye utaratibu wa kurejeshwa TAKUKURU Wilaya ya Ikungi na
mara tu zitakaporejeshwa atakabidhiwa Bi. LUCIA PETRO NYIKA.

IRAMBA       

a.
TAKUKURU (W) ya
IRAMBA imeweza kuokoa fedha  kiasi
cha Tsh.3,500,000/= zilizokuwa zimechukuliwa na kampuni ya ANGELVA FINANCIAL
LTD kinyume na utaratibu wa Kibenki. Ambapo
siku ya  tarehe 26/06/2020 Ofisi
ya TAKUKURU (W) IRAMBA ilimkabidhi MAGRETH
BUSONGO fedha  kiasi cha
Tsh.3,500,000/=.

Awali
ilipokelewa taarifa ya  kulipishwa riba
kubwa katika mkopo aliokopa kutoka kwa kampuni ya ANGELVA FINANCIAL LTD ya
Kiomboi Iramba kiasi cha Tsh.1,000,000/= mwezi agosti mwaka 2019  na kulipa marejesho ya Tsh.9,250,000/= mwezi
February mwaka 2020 sawa na riba ya asilimia 925 baada ya kupata fedha za mafao
ya kustaafu.

 

MANYONI

a. TAKUKURU(W)
YA  MANYONI imeweza kuokoa fedha  kiasi cha Tsh.360,000/= zilizokuwa
zimechukuliwa na kampuni ya MWITA CREDITORS kinyume na utaratibu wa Kibenki
.Mtumishi Mstaafu Bw. CHRISTOPHER MWALUKO KABUDI alizidishiwa riba kwenye mkopo
wake na alikuwa amelipa fedha nyingi kuliko alivyotakiwa kurejesha.Baada
Takukuru kufuatilia ilibainika kwamba kiasi cha shilingi laki tatu na sitini (360,000/=) zilikua zimerejeshwa na
mlalamikaji baada ya mkopo kumalizika.Hivyo wahusika walipohojiwa walikiri kosa
na kuzirejesha fedha hizo kiasi cha Tshs. 360,000/=. TAKUKURU(W) ya Manyoni
imerejesha fedha hizo kwa CHRISTOPHER MWALUKO KABUDI.

b.
TAKUKURU (W) MANYONI imeweza kuokoa fedha  kiasi cha Tsh.200,000/= zilizokuwa

zimechukuliwa na ALPHONCE NJALIKE kinyume na utaratibu wa Kibenki. Bi.PAULINA
JOSEPH alikopa kwa ALPHONCE NJALIKE kiasi cha shilingi laki mbili na wakati wa
marejesho alishindwa kurejesha waliuza vitu vyake vya ndani yakiwemo
makochi.Baada ya ofisi kuingilia kati iligundua kwamba mkopeshaji hakuwa na
leseni ya ukopeshaji na pia taratibu za uuzwaji wa makochi yake
haukufuatwa.Baada ya mlalamikiwa kuhojiwa na ofisi aliomba kulipa gharama za
makochi hayo kiasi cha shilingi laki mbili (200,000/=) na hivyo kufutwa kwa
deni husika na mlalamikaji kupata haki yake.

c.
TAKUKURU (W) MANYONI ilifanya
ufuatiliaji kwa ISSA KIULA BAKARI ni Mwalimu mstaafu na alitozwa riba kubwa
na  HAMIS ISSA ambae awali alikuwa
mfanyakazi wa MRITHOS CREDITORS. Alikopa kiasi cha shilingi milioni tisa (Tshs.
9,000,000) pamoja na riba na wakati wa marejesho mlalamikiwa alikua na kadi
pamoja na namba ya siri ya mlalamikaji.

Kutokana
na hivyo mlalamikiwa alichukua kiasi cha shilingi milioni kumi na nane kwenye
akaunti ya mlalamikaji. Baada ya mlalamikaji kumfuata alikubali kulipa shilingi
milioni tatu.Takukuru ilifanya ufuatiliaji na mlalamikiwa nae alikiri kuwa na
kiasi cha shilingi milioni tano na laki tano (Tshs.5,500,000/=) za mlalamikaji.
Aliomba kuzilipa fedha hizo ndani ya mwezi mmoja na tayari ameshalipa shilingi
milioni nne (Tshs.4,000,000/=) ambazo
mlalamikaji ISSA KIULA BAKARI alikabidhiwa na Katibu Tawala wa Wilaya Manyoni. .Fedha zilizobaki zitawasilishwa
TAKUKURU na mdaiwa tarehe 29 mwezi huu wa Oktoba 2020.

TAKUKURU (M) inazidi Kutoa
rai kwa wananchi wote kwa ujumla kujiepusha na vitendo vya Rushwa na kushiriki
kikamilifu kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa kwa kufika ofisi zetu za
TAKUKURU (M) na Wilaya au kupiga simu namba 113, kwa kutumia TAKUKURU APP wanapobaini kutokea/kutaka
kutokea kwa vitendo vya Rushwa na kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi na
kushiriki kutoa ushahidi Mahakamani.

Imetolewa
na:

 

ADILI ELINIPENDA

MKUU WA TAKUKURU (M)

SINGIDA