Home Mchanganyiko KAMATI YA AMANI YA VIONGOZI WA DINI MWANZA YAANIKA MAZITO UCHAGUZI MKUU

KAMATI YA AMANI YA VIONGOZI WA DINI MWANZA YAANIKA MAZITO UCHAGUZI MKUU

0
NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA
KAMATI ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza,kuelekea uchaguzi mkuu imetoa tamko zito ikiwataka Watanzania kuzingatia mambo 10 yatakayowezesha uchaguzi huo kufanyika kwa amani.

Tamko hilo hilo lilitolewa jana kwa waandishi wa habari na Wenyeviti Wenza wa Kamati hiyo Askofu Dk. Charles Sekelwa na Sheikh Hasani Kabeke.

Walisema Watanzania wote kila mmoja kwa nafasi yake bila kujali imani na itikadi ya vyama wahakikishe wanatunza amani ili uchaguzi huo ufanyika kwa amani, uhuru na haki kwa sababu haki na amani havitengamani.

Mwenyekiti Mwenza wa kamati hiyo Sheikh Kebeke alisema yapo mambo yanayoendelea nchini kuwa patachimbika, yanawapa hofu wananchi na ni dalili za maandalizi ya vurugu kwenye uchaguzi hata katika matokeo pia kuna changamoto ya baadhi ya wagombea kutokukubali kushindwa.

“Lazima tutazame maslahi ya umma si binafsi,mamlaka hutoka kwa Mungu na humpa amtakaye,maana nchi hii tumeipokea kutoka kwa wazazi ikiwa na amani, vijana nao wasikubali kutumiwa na wanasiasa,amani ikivunjika wahanga ni ndugu zetu na mwisho wa hayo ni Oktoba 28,baada ya uchaguzi,”alisema Kabeke na kuongeza viongozi wa dini hawataki yatokee hayo.

Akisoma tamko la Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza, Mwenyekiti Mwenza Askofu Dk.Charles Sekelwa,alisema kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na madiwani, kamati hiyo inaawasa Watanzania bila kujali vyama vyao wahakikishe wanatunza amani kwa sababu maisha yapo baada ya uchaguzi.

Alisema amani ikitoweka watu wote bila kujali mwanzilishi, mhamasishaji na atakayeivunja hakuna shughuli za kiuchumi, kijamii na maendeleo zitakazofanyika (biashara,elimu,afya na usafiri).

“Tunawaomba kuelekea uchaguzi mkuu Watanzania kutunza amani ili uchumi uimarike kwani amani ikivunjika hakuna chochote kitakachofanyika, shughuli zote za biashara,elimu,ibada,matibabu na usafiri zitaathirika,”alisema Dk. Sekelwa kwenye tamkoa hilo.

Pia kwenye tamko hilo wazazi na walezi wameshauriwa kuwakanya na kuwaeleza vijana athari za kujiingiza kwenye mambo ya kisiasa yanayoweza kuleta vurugu na kusababisha uvunjifu wa amani, wajizuie kweye mambo hayo.

Mwenyekiti Mwenza huyo aliwaasa viongozi wa dini zote waache na wajiepeshe kuwaeleza watu wachaguane kwa mlengo wa kidini bali wachague mtu ama kiongozi atakayewaletea maendeleo badala ya kuchaguana kwa imani za dini.

“Sisi viongozi wa kiroho,waumini wote wanaochagua na kuchaguliwa ni wetu a jukumu letu kubwa ni kuhakikisha tunawaongoza kutenda mema na kuacha maovu.Pia viongozi wa vyama vya siasa na wanasiasa waache na wajiepushe kutoa maneno ya uchochezi yanayoweza kuvunja amani mfano ya kitanuka, tutaibiwa kura, hatutokubali matokeo na tutaingia barabarani endapo watashindwa kwenye uchaguzi,”alisema Dk. Sekelwa.

Pia wananchi Oktoba 28, mwaka huu wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura kuwachagua viongozi wanaowataka bila bughudha na baada ya kupiga kura warejee nyumbani kusubiri matokeo yatangazwe na mamkala husika kisheria.

“Haya matamko ya zilindeni kura zenu, msitoke vituoni mkarudini nyumbani je,wafuasi wa vyama vyote wakikaa kituoni si ndio mwanzo wa vurugu?Mkipiga kura rudini nyumbani msubiri matokeo,”alisistiza Dk. Sekelwa.

Aidha kwenye tamkoa hilo kamati hiyo ya amani iliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusimamia haki kwa wagombea wa vyama vyote na ilipo haki na amani inakuwepo, pia itangaze matokeo baada ya kura kuhesabiwa na mshindi kupatikana kwani ucheleweshaji wa kutangaza mshindi kunaweza kuwatumbukiza watu kwenye hisia za mbaya na kuzusha vurugu.

Kamati hiyo iliishauri NEC kutoa fursa kwa makundi yenye mahitaji maalum na kuhakikisha vifaa vyote muhimu vya uchaguzi vinakuwepo kwenye vituo vya kupigia kura na vinafunguliwa mapema.

Kwa mujibu wa tamko hilo la kamati ya amani ya viongozi wa dini,wagombea na wafuasi wao (wananchi) wakubali matokeo yatakapotangazwa na NEC kwani katika ushindani lazima apatikane mshindi na mshindwa,hivyo asitokee mtu wa kujitangaza kabla ya tume.

Dk. Sekelwa alisema jeshi la polisi kufanya vizuri hivyo liendelee kutenda na kudumisha amani,lijizuie kutumia nguvu na lisisite kutumia nguvu mahali panapohitajika na kuviasa vyombo vya habari kutumia kalamu zao kwa weledi,vipate taarifa kutoka vyanzo sahihi.

“Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza, inawaomba viongozi wa dini kusimama kwenye nafasi zetu na wananchi bila kujali dini na madhehebu yetu tuendelee kuliombea taifa letu muda wote,”alisema Mwenyekiti Mwenza huyo.