Home Mchanganyiko Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Wapewa Mafunzo ya Mfumo...

Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Wapewa Mafunzo ya Mfumo wa MadeniMIS Wilayani Busega

0

Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu kutoka Wilaya ya Busega Wakiwa tayari kupata Mafunzo ya MadeniMIS

********************************

Watumishi wa kada ya Ualimu Wilayani Busega wapewa mafunzo ya Mfumo wa Madeni ya Watumishi Serikalini ujulikanao kama MADENI MANAGEMENT INFORMATION SYSTEM (MadeniMIS) wenye lengo la kuhakiki na kuthibitisha madeni ya Watumishi wa Serikali yasiyo ya mshahara.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa siku mbili kwa Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu, na Wasaidizi wao pamoja na Waratibu wa Elimu ngazi ya Kata, ambapo yameanza kutolewa kuanzia tarehe 02 hadi 03 Oktoba, 2020 katika ukumbi wa Silsos, Nyashimo.

Mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha watumishi wa serikali kuweza kuanzisha uingizaji wa madai yao kwenye mfumo ili baadae Walimu Wakuu na Wakuu wa shule waweze kuhakiki na kupitisha madai kwa ajili hatua za kubaini madeni ya Watumishi wa Serikali.

Awali Afisa Utumishi wa Wilaya ya Busega, Bw. Mussa Mmbyana amewataka Walimu kuwa makini wakati wa mafunzo hayo ili kufanikisha lengo la mafunzo hayo. Mafunzo ya MadeniMIS yanawezeshwa na Maafisa TEHAMA kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Busega.

Mfumo wa madeni ya Watumishi Serikalini, MadeniMIS una lengo la kuratibu madeni na madai ya Watumishi wa Serikali yasiyo ya mshahara nchi nzima lakini kwa kuanzia utaanza na madeni ya Walimu. Aidha mfumo huu utapunguza malalamiko ya madai na madeni ya Watumishi wa Serikali.