Home Mchanganyiko Upasuaji kuondoa uvimbe wa saratani bila kuondoa titi lote waleta ahueni kwa...

Upasuaji kuondoa uvimbe wa saratani bila kuondoa titi lote waleta ahueni kwa wagonjwa

0

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga za Saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk. Crispin Kahesa akizungumza jambo katika semina ya siku moja kwa mashujaa wa saratani ya matiti mapema hii leo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dk. Julius Mwaiselage akizungumza na mashujaa hao

Mashujaa (wanawake waliotibiwa na kupona saratani ya matiti) na wale wanaoendelea na matibabu dhidi ya saratani hiyo, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dk. Julius Mwaiselage na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa ORCI, Dk. Crispin Kahesa wakiinua mkono juu kama ishara ya kuishinda saratani hiyo kwa matibabu.

Mashujaa (wanawake waliotibiwa na kupona saratani ya matiti) na wale wanaoendelea na matibabu dhidi ya ugonjw huo wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza

*********************************

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

Upasuaji wa kisasa wa kuondoa uvimbe wa saratani pasipo kuondoa titi lote lililoathirika umeleta ahueni kwa wagonjwa na kupunguza unyanyapaa nchini.

Yameelezwa hayo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Julius Mwaiselage alipozungumza na waandishi wa habari katika mahojiano maalum, kuhusu mwezi Oktoba ambao ni maalum Kidunia kwa ajili ya uelimishaji, uhamasishaji, uchunguzi na matibabu ya saratani hiyo.

Amesema wastani wa wanawake 100 wanaogundulika na saratani hiyo ikiwa katika hatua za awali, huondolewa uvimbe kwa njia ya upasuaji pasipo kung’olewa titi lote lililoathiriwa, kila mwaka.

Amesema huduma hiyo ilianza kutolewa rasmi mwaka 2016 nchini na wataalamu wa ORCI wakishirikiana na wenzao wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH- Mloganzila).

Dk. Mwaiselage amebainisha kwamba ORCI kila mwaka huona wagonjwa wa saratani ya matiti kati ya 600 hadi 700 ambapo hao 100 ambao ni sawa na asilimia 30 hutibiwa kwa kuondoa uvimbe pasipo kung’oa titi lote.

“Zamani kwa kuwa hatukuwa na mashine za kisasa za tiba mionzi, matibabu yalikuwa ni lazima kuondoa titi lote, changamoto nyingine tuliyokuwa tunakabiliana nayo ni wagonjwa hawa kuchelewa kuja hospitalini, walikuja ugonjwa ukiwa umefikia hatua za juu mno, haikuwa rahisi kupata matokeo mazuri ya tiba.

“Lakini kutokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali kwa kutumia mashine hii ya ‘Linear accelerator’, tunao uwezo wa kuchunguza na kutibu kwa kuondoa ule uvimbe tu na kuliacha titi, baada ya upasuaji huo mgonjwa anaendelea na matibabu ya mionzi kupitia mashine ya kisasa tuliyonayo hapa ORCI,” amesisitiza.

Amesema hata wale waliofanyiwa upasuaji na kuondolewa katika titi lote jitihada zinafanyika ambapo tayari wataalamu wapo nchini China wakijifunza jinsi ya kufanya upasuaji wa kupandikiza matiti.

“Corona imetuchelewesha, walikuwa wawe wameshamaliza masomo yao na kurejea nchini tayari kuanzisha huduma hii,” amebainisha.

Amesema Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kila mwaka Tanzania kuna wagonjwa wapya 42,000 wa saratani aina zote, saratani ya matiti inaongoza duniani kote kwa kuathiri wanawake kwa asilimia 99, wanaume asilimia moja.

“Tanzania saratani ya matiti inashika nafasi ya pili kwa idadi kubwa ya wagonjwa, miaka 10 iliyopita ilikuwa inashika nafasi ya nne, tunaona inaongezeka kwa kasi,” amebainisha.

Amesema changamoto ambayo wanaiona hivi sasa kwenye jamii ni wimbi la taarifa potofu zilizopo kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya wagonjwa hushawishiwa kwenda kupata dawa za kienyeji ambazo hata hazijafanyiwa utafiti na hivyo huacha tiba za hospitalini.