Home Mchanganyiko BILIONI 24 KUINUA KIWANGO CHA HUDUMA YA MAJI MTWARA VIJIJINI

BILIONI 24 KUINUA KIWANGO CHA HUDUMA YA MAJI MTWARA VIJIJINI

0

Wataalam wa Wizara ya Maji wakikagua maendeleo ya kazi ya ya uboreshaji wa Chanzo cha Maji cha Mbwinji katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara.

Mhandisi Joshua Lawrence wa Wizara ya Maji akikagua baadhi ya mashine zinazotumika katika Chanzo cha Maji cha Mitema katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara.

Kiongozi wa Timu ya Wataalam wa Wizara ya Maji, Mkurugenzi Philipo Chandy (aliyekaa) akiwa pamoja na Timu ya Wataalam ya Wizara ya Maji katika Chanzo cha Maji cha Mbwinji katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wizara ya Maji, Prisca Henjewele akitoa elimu kwa msimamizi wa miongoni mwa vituo vya kuchotea maji vya Mradi wa Maji wa Lukuledi unaotoa huduma kwa wakazi 17,060 katika vijiji 5 vya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara.

Miongoni mwa vituo vya Mradi wa Maji wa Lukuledi vikitoa huduma katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara.

Ujenzi wa tenki la Mradi wa Maji wa Mnolela ukiendelea katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara.

…………………………………………………………………………..

Serikali imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 24 kwa ajili ya kazi ya ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji 205 ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa ahadi ya kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa maeneo ya vijijini mkoani Mtwara, ambao kati yao asilimia 60.1 wanapata huduma.

Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Mtwara, Mhandisi Mbaraka Ally amesema fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 31 itakayonufaisha wakazi zaidi ya 300,000 katika vijiji 205 kwa mwaka huu wa fedha wakati akitoa taarifa kwa Wataalam wa Wizara ya Maji wakiwa katika ufuatiliaji na kutathmini ujenzi wa miradi ya maji ya Kilidu Mnui na Mnolela katika Wilaya ya Newala.

“Kati ya Sh. bilioni 24 zilizotengwa, tumeshapokea Sh. bilioni 8 na zimeanza kutumika kwenye ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kilidu Mnui ambao umeshakamilika kwa gharama ya zaidi ya Sh. bilioni 1.4, ukiongeza lita 720,000 kwa siku na kuhudumia wanachi 60,000 wa Newala mjini na vijiji jirani, changamoto iliyopo ni umeme ambapo tayari tumeshachukua hatua ya kubadilisha mita ya LUKU na baada ya muda mfupi mradi utaanza kutoa huduma’’, alisema Mhandisi Ally.

“Vilevile Mradi wa Maji wa Mnonela umefikia asilimia 45 na utakamilika mwezi Disemba, 2020 kwa gharama ya zaidi ya Sh. milioni 400 na kuhudumia wakazi 2,805 wa vijiji vya Dodoma, Mkunjo, Mtanda na Mnonela katika Halmshauri ya Wilaya ya Newala inayopata huduma ya maji kwa asilimia 55”, alifafanua Mhandisi Ally.

Aidha, wakazi 17,060 wa vijiji vya Lukuledi, Nasindi, Polapola, Kalinga na Napata wameanza kupata huduma ya majisafi na salama mara baada ya Mradi wa Maji wa Lukuledi kukamilika kwa asilimia 95 kwa kiasi cha zaidi ya Sh. milioni 600 na kumaliza kilio cha muda mrefu.

Mkurugenzi wa Huduma ya Ubora wa Maji, Philipo Chandy ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Masasi-Nachingwea (MANAWASA) kwa kazi ya uboreshaji wa Chanzo cha Maji cha Mbwinji katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi.

Amesema kuwa maendeleo ya ujenzi ni mazuri na utakapokamilika utaimarisha zaidi huduma ya maji kwa wananchi waishio katika wilaya za Masasi mkoani Mtwara, Nachingwea na Ruangwa mkoani Lindi.