Home Mchanganyiko CHAURU YATARAJIA KUPATA MAPATO YA SH.MIL.478.9 MSIMU 2020/2021

CHAURU YATARAJIA KUPATA MAPATO YA SH.MIL.478.9 MSIMU 2020/2021

0

*************************************

MWAMVUA MWINYI, RUVU
CHAMA Cha Ushirika wa Wakulima wa Umwagiliaji Ruvu (CHAURU) Ltd kinachomiliki shamba la mpunga cha Ruvu ,Chalinze wilayani Bagamoyo ,Pwani kinatarajia kupata mapato ya sh.milioni 478.9 katika msimu wa kilimo wa mwaka 2020/2021.
Hayo yalisemwa Mlandizi wilayani humo na meneja wa Chauru ,Victoria Ulotu wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho ambapo fedha hizo zitatokana na vyanzo mbalimbali toka kwa wakulima wa shamba hilo la mpunga.
Alieleza, fedha hizo zinatokana na vyanzo vya mapato ikiwa ni pamoja na ada,shamba na uvunaji,umwagiliaji, matunzo ya ya mifereji na matuta,uchakataji wa mpunga,uendeshaji zana na karakana,mauzo ya pembejeo za kilimo, na ukodishaji .
“Katika mapato hayo tunatarajia kutumia kiasi cha sh.milioni 312.5 kama gharama za uendeshaji ikiwa ni pamoja na utawala, miashara na posho kwa wafanyakazi, gharama za watumishi, gharama za ofisi, gharama za mawasiliano, gharama za usafiri, gharama ustawi wa jamii, gharama za mikutano na vikao,gharama za kisheria na nyinginezo,”alisema Ulotu.
Alisema kuwa chama kitabaki na ziada ya shilingi milioni 166.4 baada ya kutoa gharama zote za uendeshaji chama kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2020/2021 ambao unaanza mwezi Oktoba.
“Lengo letu ni kuhakikisha eneo lote la Chauru linalimwa kwani kwa sasa linalimwa sehemu tu hivyo tunaomba watu wajitokeze kujiunga na chama ambacho kwa sasa kinajijenga upya na kuwa na mwelekeo wa kibiahara ili kuleta faida kwa wanachama wake,”alisema Ulotu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chauru Chacha Sadala alisema kuwa chama chao kimefanikiwa sana baada ya kupita kwenye mabaliko ikiwa ni pamoja na kushika nafasi ya 52 kati ya vyama bora vya ushirika dunia baada ya kushindaniwa na vyama vingine 354 kupitia taasisi ya agriterra juu ya taarifa za ukaguzi.
Sadala alisema ,chama hicho kilikuwa na changamoto nyingi lakini kwa kinakwenda vizuri tangu walivyokabidhiwa kutoka lilikuwa shirika la chakula Nafco ambapo miundombinu yake mingi ilikuwa imekufa kutokana na uchakavu kwani ilijengwa miaka ya 60.
Alisema kuwa moja ya changamoto zilizopo ni madeni ya kilimo ambapo baadhi ya wanachama na watu wanaokodisha mashamba wamekuwa hawalipi fedha zote unapofika msimu kwani hulipa kidogo na kusema kuwa wangelipa lakini wanalimbikiza madeni na kukifanya chama kidai wakulima.
Naye mmoja wa wanachama wa umoja huo Hussein Dilunga alisema kuwa kutokana na wakulima kuvuna mazao mengi maghala yamejaa mpunga hivyo mpunga wao kuwa nje.
Dilunga alisema kuwa kutokana na hali hiyo kuna haja ya kujenga maghala ili kuhifadhi mpunga wao kwani endapo mvua itanyesha mpunga unaweza kuharibika.      
Chama hicho kina jumla ya wanachama 894 ambapo eneo lao lina ukubwa wa hekari 3,209 ,u zinazolimwa ni hekari 1,800 na wakulima wako wa aina mbili wanachama na wengine hukodisha mashamba na ni moja ya mashamba yanayozalisha mpunga kwa wingi hapa nchini.