Home Mchanganyiko Hasunga Atoa Siku 5 Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Kukamilisha Malipo...

Hasunga Atoa Siku 5 Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Kukamilisha Malipo ya Wakulima wa Korosho Kibiti na Mkuranga

0


Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga(Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na wakulima wa Korosho, Maafisa Ugani, na wadau mbalimbali wa Kilimo katika Wilaya ya Mkuranga akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Pwani. (Picha Zote Na Innocent Natai)

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga(Mb) akizungumza na moja ya
Wakulima wa Korosho Wilayani Mkuranga Mkoani Pwani, Jana Tarehe 13 Agosti 2020. 

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga(Mb) akisalimiana na viongozi
wa kamati ya ulinzi na usalama  Wilayani Kibiti Mkoani Pwani. 
Jana Tarehe 13 Agosti 2020. 

Na Innocent Natai, Pwani

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ametoa siku
Tano kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania(CPB), Viongozi wa Vyama
vya Ushirika pamoja na Benki ya Kilimo, kuhakikisha wanakutana na wakulima wa
Korosho Wilayani Mkuranga Mkoani Pwani ambao fedha zao za mauzo ya Korosho
hazijalipwa mpaka sasa ili kuwalipa haraka iwezekanavyo.

Amewataka kukagua taarifa zao na kuwalipa
fedha zao mara moja kwani serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania Dkt
John Pombe Magufuli ilishatoa fedha zote kwa ajili ya kufanyika kwa malipo hayo, “Nasikitika kwanini mpaka sasa malipo hayajakamilika” Aliuliza Waziri Hasunga

Akizungumza mbele ya Wakulima na Maafisa ugani Waziri Hasunga amesema kuwa inasikitisha kuona bado kuna wakulima wanaidai serikali
angali serikali kupitia kwa Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli imekwisha kutoa
fedha kwa ajili ya kuwalipa kwa muda mrefu kitendo kinachowafanya wakulima
kuichukia serikali na kukata taama ya kufanya kilimo.

Amesema kuwa kumekuwa na kisingizio cha muda mrefu kuwa baadhi ya wakulima taarifa
zao za kibenki zina makosa hivyo kusababisha kushindwa kufanyiwa malipo kwa
njia ya kibenki jambo hili siwezi kukubaliana nalo.

“Nilitoa siku 14 kuhakikisha kuwa wakulima wa
Korosho Wilaya ya Mkuranga wawe wamemaliza kulipwa fedha zao lakini mpaka sasa
bado natoa siku tano Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko
Tanzania(CPB), viongozi wa Vyama vya Ushirika pamoja na Benki ya Kilimo
kuhakikisha hili suala linamalizika” Alisema Hasunga

Aidha, Hasunga ametoa siku mbili
kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania CPB kuhakikisha
wanabandika majina ya Wakulima waliolipwa fedha zao za Korosho kuanzia Mwezi
Januari 2020 kwenye mbao za matangazo ili kuwasaidia wakulima kutambua
walikwisha kulipwa fedha zao na ambao bado ili pia serikali kuweza kubaini
udanganyifu unaofanywa katika malipo.

Pia amesema serikali kupitia Wizara ya Kilimo
na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga imewakamata na itaendelea kuwakamata
viongozi wa vyama vya ushirika wanaofanya ubadhilifu wa mali za wanaushirika,
pia na waliofanya ubadhilifu na wizi kwenye uuzaji wa Korosho msimu uliopita

Hivyo, Hasunga amewataka wakulima kuendelea
kuvumilia wakati  serikali ikiendelea kuwafuatilia na kuwakamata
waliofanya wizi wa kuuza korosho za wakulima bila kufuata utaratibi na kuwalipa
Wakulima hao.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga mbali na
kutembelea, kusikiliza na kutatua kero za Wakulima wa Korosho Wilayani Mkuranga
Mkoani Pwani alifika pia kuzungumza na wakulima Wilayani Kibiti Mkoani hapo
huku akiendelea kutoa maagizo ya kuhakikisha wakulima wa Korosho wanalipwa
stahiki zao kwa wakati na waliofanya udanganyifu na kuuza korosho za wakulima
kuchukuliwa hatua za Kisheria.