Home Mchanganyiko MWILI WA MZEE MKAPA WA PUMZISHWA KIJIJINI KWAO LUPASO WILAYANI MASASI –...

MWILI WA MZEE MKAPA WA PUMZISHWA KIJIJINI KWAO LUPASO WILAYANI MASASI – MTWARA

0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiweka udongo kwenye kaburi la Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa katika Mazishi yaliyofanyika katika Kijiji cha Lupaso Masasi Mkoani Mtwara

……………………………………………………….

Na.Majid Abdulkarim, Lupaso – Masasi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa eneo lililotengwa kwa ajili ya  mazishi ya Viongozi Dodoma litumike kwa mambo mengine kwa ajili ya wananchi na viongozi hao watazikwa katika maeneo yao walipozaliwa.

Kauli hiyo ameitoa leo katika mazishi ya Hayati Benjamini Mkapa aliyekuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika  Kijijini cha Lupaso wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara .

“Kuna wakati tulipanga sehemu ya kuzika Viongozi Dodoma, Mzee Mkapa akasema nizikeni Lupaso, nilipomuuliza Mzee Kikwete akasema Msoga, nikaogopa kumuuliza Mzee Mwinyi maana ana miaka mingi isije kutokea kitu nikaonekana nimemletea uchuro, mimi pia nikawaza nikifariki nizikwe Chato”ameeleza Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amesema kuwa  Watu wa Lupaso wana bahati sana kumpa Mzee Mkapa ambaye ni Mzalendo aliyependa nyumbani kwao ndio maana hata akachagua akifariki azikwe Lupaso.

Hivyo Rais Magufuli ametoa wito kwa Jamii ya Watanzania kuwa inapaswa kujifunza kwa Mzee Mkapa kwa upendo aliouonyesha kwa Wananchi wote,  Kijiji cha Lupaso kimeacha alama kubwa kwa Taifa la Tanzania kutokana na kutoa Kiongozi Mzalendo na aliyependa Wananchi wake

Rais Magufuli amehitimisha kwa kuishukuru Kamati ya Maandalizi ya Mazishi iliyoongozwa na Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Viongozi wote, Wananchi, Viongozi wa Dini zote sambamba na Waombolezaji walioshiriki bega kwa bega kuhakikisha safari ya mwisho ya Hayati Mzee Benjamin Mkapa katika makazi yake ya milele.

Naye Rais wa Zanzibar, Dkt.  Ali Mohammed Shein akitoa salam za mwisho katika mazishi hayo amesema kuwa leo tunamuaga mkapa kwa majonzi makubwa wananchi wa zanzibari wanaungana na watanzania  kumuombea mzee mkapa Mwenyezi mungu amsamehe huko mbinguni.

Naye Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameeleza kuwa kuna kipindi alipita  nyakati ngumu, nzito na katika nyakati zile mzee Mkapa alikuwa ni mmoja wa nguzo zake za kuegemea katika kipindi kile kigumu, kwa hiyo ni mtu aliyekuwa na msaada mkubwa kwake na kwa taifa .

“Wilaya hii ya Masasi ilikuwa na tatizo la njaa wakati ule, nikiwa Katibu CCM Masasi na DC tukabuni mradi wa kilimo cha muhogo hakikupendeza sana kwasababu Wamakuwa hawapendi sana kula ugali wa mihogo kama Mashemeji zangu Wamakonde, ila Mzee Mkapa alisimama nasi” ameweka wazi Dkt. Kikwete

“Ni ngumu kupata maneno ya kumuelezea Mzee Mkapa, nimemfahamu miaka mingi lakini nimemfahamu zaidi nilipokuwa Katibu CCM Wilaya ya Masasi na yeye alikuwa Mbunge Nanyumbu, alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje ila pamoja na ubize aliwatumikia Wananchi wake”, ameeleza Dkt. Kikwete.

Katika mazishi hayo  baada ya mwili wa hayati Mkapa kushushwa kaburini na taratibu za kidini kukamilika, imepigwa  mizinga 21 ikiwa ni ishara ya heshima kwa marehemu Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu Benjamin William Mkapa.