Home Mchanganyiko WAGANGA WAFAWIDHI WATAKIWA KUJENGA UWEZO WA KUJITEGEMEA

WAGANGA WAFAWIDHI WATAKIWA KUJENGA UWEZO WA KUJITEGEMEA

0

*************************************

Na.WAMJW-Dodoma

Waganga Wafawidhi wa hospitali wote nchini wametakiwa kujijengea uwezo wa kujitegemea katika kuboresha huduma za afya nchini kwa kuwa wabunifu katika huduma na vyanzo vya mapato ili kupunguza utegemezi wa kifedha toka Serikalini.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi mara baada ya kutembelea hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma katika ziara yake ya kujionea hali ya utoaji huduma za afya zinazofanywa na hospitali za rufaa za mikoa.

“Mjenge mfumo wa kujitegemea kwani mnapaswa mambo mengine kuyafanya wenyewe katika kuendesha hospitali zenu licha ya serikali kuwapatia fedha”.

Alisema licha ya serikali kuwapatia fedha ni wakati sasa kuondoa mtazamo huo kwani serikali itawasaidia masuala kadhaa hivyo mambo mengine lazima wajitegemee ili kuacha kulalamika na kutoa huduma mbovu kwenye hospitali hizo

Hatahivyo aliwataka waganga wafawidhi kukaa na watumishi wote kuweza kupata mawazo ambayo wanaweza kuboresha Hospitali zao na kuweza kuongeza vyanzo vya mapato na kutoa motisha kwa wafanyakazi wake.

Kwa upande kwa huduma za kibingwa Prof. Makubi alielekeza viongozi wa hospitali hizo zishirikishe watumishi na jamii katika kuboresha hali ya utoaji huduma katika maeneo yao.

Hata hivyo Prof. Makubi ametoa miezi mitatu kwa waganga wafawidhi wote wasiokua wabunifu waamke na kuahidi wizara yake itafanya tathmini na kuchuja Waganga wafawidhi wanaoendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale ambao wataonekana hawafai wataondolewa.