Home Mchanganyiko Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Imeombwa Kuwafikia Wananchi Wanaoishi Maeneo ya...

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Imeombwa Kuwafikia Wananchi Wanaoishi Maeneo ya vijijini

0

Wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwapima wananchi waliotembelea banda la JKCI lililopo ukumbi wa Karume shinikizo la damu (BP) pamoja na kutoa ushauri wa magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mary Haule akimpima kiwango cha sukari mwilini  mwananchi aliyetembelea banda la JKCI JKCI lililopo ukumbi wa Karume wakati wa  maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Smitha Bhalia akimweleza kuhusu ugonjwa wa kutanuka kwa moyo mwananchi aliyetembelea banda la JKCI lililopo ukumbi wa Karume wakati wa  maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

Wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwahudumia  wananchi waliotembelea banda la JKCI wakati wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam. Katika maonesho hayo Taasisi hiyo inatoa huduma za upimaji na ushauri wa magonjwa ya moyo

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Winnie Masakuya akimuelezea mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo  namna ambavyo mishipa  inayopeleka damu kwenye moyo inavyoweza kuziba kutokana na kuganda kwa mafuta  katika mishipa hiyo wakati wa maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ipyana Mwailafu kiwango cha sukari mwilini  mwananchi aliyetembelea banda la JKCI lililopo ukumbi wa Karume wakati wa  maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

Picha na JKCI

……………………………………………………………………

Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam

 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeombwa kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa wanaoishi maeneo ya vijijini ili waweze kupata huduma za upimaji, ushauri  na matibabu ya moyo kama wanazozitoa kwa wananchi wanaoishi mjini.

Ombi hilo limetolewa na baadhi ya wananchi waliotembelea banda la Taasisi hiyo lililopo ukumbi wa Karume kwa ajili ya kufanya vipimo na kupata ushauri wa magojwa ya moyo wakati wa maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

Wananchi hao walisema watu wengi wanaoishi maeneo ya mjini wanapata nafasi ya kupima afya zao mara kwa mara hii ni kutokana na taasisi mbalimbali za afya kufanya upimaji wa bila malipo tofauti na ilivyo kwa wanachi wanaoishi vijijini.

“Leo hii nimetembelea katika maonesho haya nimepata bahati ya kupima afya na kupata ushauri wa mtaalamu wa lishe ambao utanisaidia kula chakula bora ambacho hakitaniletea madhara  katika mwili wangu”, alisema Patricia Chikojo ambaye ni mkazi wa Mkuranga mkoani Pwani.

Patricia aliwashauri wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam pamoja na mikoa ya jirani kutembelea banda la Taasisi hiyo lililoko katika ukumbi wa Karume ili waweze kupata huduma mbalimbali za upimaji wa magonjwa ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi hiyo.

“Wito wangu kwa wananchi watembelee maonesho hayo na kwenda kupima magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa moyo kwa kufanya hivyo watatambua hali zao kuliko kusubiri waumwe ambapo wanaweza kugundulika kuwa na magonjwa makubwa ambayo matibabu yake yakawa ya gharama au magonjwa hayo yakashindwa kutibika kutokana na kuchelewa kugundulika”, alisema Patricia.

Kwa upande wake Cyril Kessi ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam alifurahia huduma aliyoipata ya upimaji na ushauri wa magonjwa ya  moyo pia alipata muda wa kupima vipimo mbalimbali ikiwemo urefu, uzito, damu, kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO) na umeme wa moyo (ECG).

“Huduma niliyoipata ni nzuri, kuna vipimo nimepima bure na vingine nimelipia gharama kidogo  ukilinganisha na kama ningekwenda Hospitali kupima. Pia nimepata muda wa kutosha wa kuzungumza na daktari ambaye amenieleza kwa kina kuhusu magonjwa ya moyo”, alisema Kessi.

Akizugumzia  kuhusu maonesho hayo Mkuu wa kitengo cha Utafiti na Mafunzo wa Taasisi hiyo Dkt. Naiz Majani alisema katika maonesho hayo wanatoa huduma za uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo bila malipo yoyote, upimaji wa magonjwa ya Moyo vikiwepo vipimo vya damu, ECHO na ECG.

Ushauri wa kiafya kuhusiana na magonjwa ya moyo, elimu ya lishe bora, kuelezea kwa kina huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo na kutoa Rufaa ya moja kwa moja kwa wagonjwa watakaokutwa na matatizo ya Moyo yanayohitaji kupewa rufaa.

Dkt. Naiz ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto alisema  asilimia kubwa ya watu waliowapima walikuwa wanatumia dawa za shinikizo la damu (BP) lakini baada ya kuona hali zao ziko vizuri  wameacha kutumia dawa kitu ambacho siyo sawa kwani mgonjwa wa shinikizo la damu akianza kutumia dawa hatakiwi kuziacha katika maisha yake yote.

“Tumewaanzishia  dawa wagonjwa tuliowakuta wameacha kutumia dawa za shinikizo la damu pia tumewaeleza madhara ya kuacha kutumia dawa hizo hii ikiwa ni pamoja na moyo kutanuka na kushindwa kufanya kazi , kupofuka kwa macho, figo kuacha kufanya kazi, kiharusi  na vifo vya ghafla”, alisema Dkt. Naiz.

Aliwashauri wazazi wanaokwenda kupima afya zao katika banda hilo kwenda kupima na familia zao wakiwemo watoto kwani tafiti zinaonesha kuwa kati ya watoto 100 wanaozaliwa wakiwa hai mmoja anatatizo la moyo.