Home Mchanganyiko Shule 20 za Msingi Zenye Changamoto Kubwa ya Maji Zajengewa Miundombinu ya...

Shule 20 za Msingi Zenye Changamoto Kubwa ya Maji Zajengewa Miundombinu ya Maji Kukabiliana na Corona-Njombe

0

**********************************

NJOMBE

Takribani shule 20 za msingi zinazokabiliwa na changamoto kubwa ya maji kutoka kata nne za wilaya Ludewa mkoani Njombe zimejengewa miundombinu ya maji ya bomba na kisha kufungiwa pampu za umeme ili kusogeza na kurahisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu mashuleni katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona.

Miundombinu hiyo ambayo imejengwa usiku na mchana ndani ya siku 14 na shirika la SHIPO kupitia mradi wa MAMMIE kwa ufadhili wa WE WORLD ulianza kutekelezwa punde tu katika kata ya Mawengi,Milo,Mlangali na Lubonde wilayani humo baada ya rais Magufuli kuweka bayana tarehe ya kufunguliwa shule zote kutokana kupungua kwa maambukizi ya virus vya corona.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya miradi na vifaa vya kujikinga na corona zikiwemo mashine za kunawia mikono,sabuni na ndoo mratibu wa mradi wa kuboresha elimu wa MAMMIE unaotekelezwa na SHIPO Nemes Temba anasema wamelazimika kusaidia shule hizo zenye changamoto kubwa ya maji hivyo kusogezwa kwa huduma hiyo kutasaidia mapambano dhidi ya ugonjwa huo ambao umetikisa dunia.

Temba amesema shule nyingi za wilaya ya Ludewa zimekuwa na changamoto kubwa ya maji hali ambayo imekuwa ngumu kwa wanafunzi kutekeleza maagizo ya wizara katika kukabiliana na  COVID 19 na kudai kwamba msaada wa vifaa vya kujikinga na corona wa matenki ya lita elfu 2000,sabuni na ndoo ulioambatana na ujenzi wa miundombinu ya maji utawasaidia wanafunzi na walimu kukabiliana na ugonjwa huo.

Mbali na kutoa vifaa hivyo shirika la shipo pia limekagua miradi ya parachichi ambayo lilitoa msaada kwa shule za msingi katika wilaya ya Ludewa ili kuzisadia shule kutengeneza kipato pamoja na chakula.

Awali katika makabidhiano ya mradi wa maji na vifaa kinga Fundi Sanifu Mwandamizi RUWASA wilaya ya Ludewa Said Rubanga anasema zaidi ya vijiji 46 vya wilaya hiyo yenye vijiji zaidi ya 70 havina huduma ya maji ya uhakika hivyo kitendo cha shirika la SHIPO kupitia mradi wake wa MAMMIE unaofadhiliwa na WE WORLD kujenga miundombinu ya maji katika shule ya msingi 20 umeipunguzia mzigo serikali na kutoa rai kwa wananchi ,walimu na wanafunzi kutunza miundombinu hiyo

Wakati jitihada zikiendelea kuchukuliwa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu mashuleni,walimu wilayani humo  akiwemo Agnes Mwinuka na Andrew Haule wanasema ili kujikinga na ugonjwa huo mashuleni wamelazimika kutoa miongozo ya wizara kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na ukaaji .

Kuhusu athari za corona kitaaluma walimu hao wamesema ratiba ya masomo imevurugika kwa kiasi kikubwa hivyo ili kukimbizana na muda mchache uliosalia wamelazimika kuongeza muda wa masomo kutoka ma-saa 10 hadi 12

Kwa upande wao  wanafunzi akiwemo Elina Mwinuka Mwanafunzi shule ya msingi Mdete na Elemence Muhagama wa shule ya msingi Mavala wanasema wamerejea shuleni wakiwa na hofu kubwa lakini wanachukua jitihada za kukabiliana na ugonjwa huo kwa kufuata maagizo na miongozo inayotolewa na walimu na watumishi wengine wa serikali.