Home Mchanganyiko NHIF YAELIMISHA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA UMUHIMU WA BIMA YA AFYA

NHIF YAELIMISHA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA UMUHIMU WA BIMA YA AFYA

0

………………………………………………………………………………….

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) leo umetoa elimu juu ya umuhimu wa bima ya afya kwa viongozi wa vyama vya siasa katika kikao kazi kilichoandaliwa kwa ajili yao na Msajili wa Vyama vya Siasa.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) aliwaambia viongozi hao kuwa suala la afya ni jambo la msingi hivyo kwa taasisi za siasa ni vema kuwa na elimu kuhusu bima ya afya ili waweze kunufaika nayo.
“Sisi wote ni wanasiasa hapa na tunajua ni jinsi gani katika utekelezaji wa majukumu yetu tunavyokutana na mahitaji ya matibabu kwa ajili ya afya zetu. Suala la bima ya afya kwetu ni la muhimu na niwapongeze NHIF kwa kuipa kipaumbele sana nafasi hii na kuja kutuelimisha” amesema Mhe. Jenista.

Akitoa mada kuhusu umuhimu wa bima ya afya, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw. Bernard Konga amesema NHIF sasa imefanikiwa kuweka taratibu zinazowezesha kila mtanzania kuwa na bima ya afya. Yale makundi ambayo hapo awali ilikuwa changamoto kujiunga sasa wanaweza kujiunga.
“Tumefungua milango kwa kila mtu kujiunga kulingana na mahitaji yake, tunajua wote kuwa ugonjwa unakuja bila hodi hivyo kwetu ni mafanikio kuwezesha kila mtu kujiunga” alisema Bw. Konga

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa bima ya afya Bwana Konga alisema kuwa kwanza ni kumpa uhakika wa matibabu mwananchi wakati wowote na mahali popote. Gharama za matibabu ni kubwa na sio rahisi mtu kumudu na mara nyingi watu wamekuwa wakipata changamoto na hata kutumia mtaji kwa matibabu na hivyo kusababisha umaskini usiotarajiwa.
“Bima inamwezesha mtu kutumia rasilimali fedha zake kwa ajili ya shughuli za kiuchumi wakati bima ya afya inampa uhakika wa kutibiwa atakapougua” alisema Bw. Konga

Mfuko huo umetoa pia fursa kwa viongozi wa vyama vya siasa, watumishi wa vyama vyao na wanachama wao kujiunga na bima ya afya na kunufaika.

Akizungumzia mojawapo ya changamoto za NHIF, Bw. Konga alisema ni wananchi kusubiri mpaka waugue ndipo wajiunge na bima ya afya kitu ambacho ni kinyume na dhana nzima ya bima ya afya. Alisema NHIF inaendelea kutoa elimu ili watu wajue bima ni suluhisho lakini kujiunga ni kabla ya kuugua.

Mfuko huo unaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na bima ya afya.

Akihitimisha mafunzo hayo Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Mhe. Jaji Francis Mutungi aliwakumbusha viongozi hao wa vyama vya siasa kwamba jamii inawaangalia na kuwasikiliza viongozi hivyo ni muhimu kwao kama viongozi wa wananchi kupata elimu hii ya bima ya afya na kuitumia.