Home Mchanganyiko MADAKTARIA WA MIFUGO WATAKIWA KUHUISHA TAARIFA ZAO KATIKA DAFTARI LA USAJILI

MADAKTARIA WA MIFUGO WATAKIWA KUHUISHA TAARIFA ZAO KATIKA DAFTARI LA USAJILI

0

Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania Dkt.Bedan Masuruli,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa juu ya Afya ya Mifugo nchini pamoja na kuwataka madaktari kuhuisha majina yao kwenye daftari la usajili wa madaktari.

………………………………………………………………….

Na Mwandishi wetu,

Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania, Dkt.Bedan Masuruli amewataka Madaktari wa Mifugo nchini kuhuisha majina yao kwenye daftari la usajili wa madaktari wa mifugo  kabla ya  Julai 1, 2020.

Akizungumza ofisini kwake wakati anatoa tamko hilo  jijini Dodoma Juni 26, 2020,  Dkt. Masuruli alisema ni muhimu wataalam kuhuisha majina yao ili Baraza liweze kufahamu wako wapi, wanafanya nini na wanatoa huduma gani.

“Nasisitiza madaktari wote wa mifugo ambao hawajahuisha taarifa zao kwenye daftari la usajili wa madaktari wafanye hivyo kuanzia leo hadi kufikia Julai 1, 2020 baada ya hapo tunaanza kusimamia Sheria inayowataka kuhuisha majina yao kwenye daftari la usajili” alisema Dkt. Masuruli.

 Dkt. Masuruli aliongeza kuwa baada ya zoezi hilo la kuhuisha majina ya madaktari wa mifugo kukamilika watatoa vitambulisho kwa madaktari hao  ili kuwatambulisha kwa jamii  kwa sababu taaluma hiyo imeingiliwa na vishoka wanaoharibu sifa za taaluma hiyo. 

Alisisitiza kuwa wanafanya hayo yote ili kuboresha huduma kwa wafugaji  huku akisema  wamejipanga kusambaza wataalamu wa mifugo kwenye ngazi za msingi ili kuwa karibu na wananchi na kuwashauri namna ya kuipatia kinga mifugo yao na kuleta tija katika ufugaji wao.

Aliongeza  kuwa ili kufikia adhma hiyo ni  lazima wataalamu wote wa ngazi ya msingi kusajiliwa, kujiandikisha na kujiorodhesha katika daftari ili kusaidia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujua ubora wa wataalamu walionao katika maeneo yote na  kusaidia wananchi  kuongeza tija katika  sekta ya ufugaji.

“Tumeongeza muda ili wataalum waweze kuhuisha majina yao kwenye daftari la usajili wa madaktari kabla ya Julai 1 wawe tayari wamejisajili, na kwa ambaye hata fanya hivyo sheria za usajili zitachukua mkondo wake,”alisisitiza

“Baada ya kuhuisha taarifa zao,  wataalamu watapatiwa vitambulisho maalum ili kusaidia wafugaji na wananchi kutambua kuwa ni mtaalamu aliyekidhi viwango na hivyo, mwananchi anaweza kupatiwa huduma kwa kupata ushauri, kinga na namna ya kuboresha ufugaji ili kufikia mafaniko makubwa,” aliongeza

Dkt.Masuruli amesema kuwa Wataalamu hao  watatakiwa kuwasilisha Wizarani taarifa za magonjwa ya mifugo inayosumbua katika maeneo yao ili kusaidia serikali kuandaa mpango kazi wa kutatua changamoto zilizoshindikana kutatuliwa na wataalaum hao.

Aidha, alisisitiza kuwa lengo kuu la kusogeza huduma hizo kwa wananchi ni kutaka kuhakikisha wanapatiwa huduma bora zinazokidhi viwango na itasaidia kubaini magonjwa yanayojitokeza katika mifungo ya wanachi wanao wahudumia na kuwasaidia kwa ukaribu.

“Natoa wito kwa vituo vyote vya afya ya wanyama kuanzia Julai Mosi, 2020 kuweka mpango wa muda wa miezi mitatu kupata vitendanishi na hadubini katika vituo hivyo ili kusaidia kujua magonjwa katika mifugo ya wanachi  wanao wahudumia,” alifafanua 

Dkt.Masuruli aliongeza kuwa   ili wananchi waweze kunufaika na ufugaji ni muhimu wataalamu hao kuwa karibu na wafugaji ili kuwasaidia kuwapatia huduma bora itakayokidhi viwango na kuleta tija kwa asilimia kubwa na kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.