Na Mwandishi wetu-OSG
Mnamo tarehe 15 Juni, 2020 Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imetoa uamuzi wa kufuta shauri la Kikatiba Na. 12 la mwaka 2020 lililofunguliwa Mahakamani hapo na asasi ya kiraia ya Civic and Legal Aid Organization (CILAO) dhidi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mbunge wa jimbo la Ndanda, Mhe. Cecil Mwambe.
Asasi ya kiraia ya Civic and Legal Aid Organization iliomba Mahakama Kuu kutengua amri ya Spika ya kumtambua Mhe. Mwambe kama Mbunge halali wakati Mbunge huyo alikwisha tangaza kujindoa uanachama wa chama chake cha Demokrasi na Madendeleo (CHADEMA) na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Asasi ya Civic and Legal Aid Organization ilidai Mahakamani hapo kuwa, kitendo cha Spika kumtambua Bwana Mwambe kama mbunge halali wakati Bwana Mwambe ameshajivua uanachama wa chama kilichomdhamini kama mbunge wa jimbo la Ndanda (2015-2020), ni ukiukwaji wa ibara ya 71(1)(f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka1977.
Mwakili wanaoiwakilisha Asasi hiyo waliongeza kuwa Kifungu cha 6C (1) na (2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 kama ilivyorekebishwa. Ilielezwa kuwa, hakuna mamlaka yoyote nchini, achilia mbali Spika, yenye uwezo wa kumrudisha Bungeni mbunge ambaye kwa hiari yake mwenyewe ameamua kujivua uanachama wa chama cha siasa kilichomdhamini kupata ubunge.
Wakiwasilisha mapingamizi ya serikali mbele ya Jaji anayesikiliza shauri hilo Mhe. Jaji. Stephen Kirimi Magoiga, Mawakili wa Serikali kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali waliwasilisha majibu ya kupinga shauri hilo na kuweka mapingamizi ya awali ya kisheria yapatayo manne yaliyosikilizwa tarehe 11 Juni, 2020. Moja ya mapingamizi hayo ni kuwa, shauri husika halikuwa na msingi wowote kisheria na lililenga kusababisha usumbufu kwa Mahakama.
Mawakili wa Serikali Bw. George Mandepo na Erigh Rumisha Serikali waliiomba Mahakama hiyo kutupilia mbali shauri hilo kwa kuwa shauri hilo linafanana na shauri jingine la Kikatiba Na. 10 la mwaka 2020 lililofunguliwa na Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Bw. Paul Kaunda dhidi ya Spika, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mhe.Cecil Mwambe.
Aidha Mawakili hao waliieleza Mahakama kuwa shauri la Asasi ya Civic and Legal Aid Organization linafafana kabisa na la Bw. Paul Kaunda dhidi ya Spika, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mhe.Cecil Mwambe, hivyo wakaiomba Mahakama hiyo ilitupilie mbali kwa kuwa Halina msingi wa kisheria.
Wakiendelea na utetezi wao mawakili wa Serikali waliiomba Mhakama hiyo kulitupilia mbali shauri hilo kwa kuwa shauri hilo halikuwa na msingi zaidi lilikusudia kuitaka Mahakama kutoa uamzi usiofaa kwani shauri hilo lilipaswa kuletwa Mahakamani hapo kwa kuzingatia sheria ya Taifa ya Uchaguzi.
Baada ya kuchambua hoja za mapingamizi hayo, Mhe. Magoiga ilikubaliana na hoja ya Mawakili wa Serikali kuwa shauri hilo la Civic and Legal Aid Organization halina msingi wowote kisheria na halikupaswa kuletwa kama shauri la Kikatiba bali kama kesi ya kawaida ya kupinga ubunge.
“Mahakama imeona kuwa suala la uamuzi kama mtu ni mbunge au sio Mbunge na kiti chake katika Bunge kiwazi au hapana lina utaratibu wake chini ya Katiba”. Alisema Jaji Magoiga.
Jaji Magoiga aliongeza kuwa Mahakama imeamua kuwa suala la uhalali wa mbunge linasimamiwa na Ibara ya 83(1)(b) na ibara ndogo ya 83(3) ya Katiba ikisomwa sambamba na kifungu cha 37(3) na (4) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 Hivyo basi, Mahakama ilifikia uamuzi wa kulitupilia mbali shauri hilo la kupinga ubunge wa Mhe. Cecil Mwambe pasipo kutoa gharama kwa upande wa Serikali.
Katika shauri hilo upande wa mlalamikaji uliwakilishwa Mahakamana hapo na Wakili wa Kujitegemea Bw. John Seka na Mhe. Mwambe aliwakilishwa na Wakili Dismas Raphael.