Home Mchanganyiko TAKUKURU MANYARA YAWASHIKILIA MAAFISA WATATU WA TRA KWA RUSHWA

TAKUKURU MANYARA YAWASHIKILIA MAAFISA WATATU WA TRA KWA RUSHWA

0

………………………………………………………………

Na mwandishi wetu, Babati

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, inawashikilia maafisa watatu wa Mamlaka ya mapato nchini (TRA) kwa kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni moja kwa mfanyabiashara wa eneo hilo ili wasimuongezee makadirio ya kodi katika biashara yake ya duka la rejareja.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu aliwataja maafisa hao wa TRA wanaowashikilia ni Eva Joseph Mtandao, Jackline Leonard Manjira na Ephrahim John Medard.

Makungu alisema uchunguzi wa TAKUKURU Mkoani Manyara, ulibaini kuwa mfanyabiashara huyo alikadiriwa kulipa kodi ya shilingi 250,000 kwa mwaka na mtumishi wa TRA ambaye hakumdai rushwa.

Alisema mfanyabiashara huyo akaomba kulipa kodi hiyo kwa awamu na akakubaliwa ambapo hadi Juni 20 alikuwa amelipa awamu ya kwanza ya kodi aliyokadiriwa.

“Wakati akiendelea na biashara yake huku akisubiri kulipa awamu ya pili alifuatwa tena na watuhumiwa hao watatu ambao walimwambia kuwa amekadiriwa chini ya kiwango kwani kwa biashara yake alitakiwa kuwa na mashine ya EFD hivyo ametenda makosa,” alisema Makungu.

Alisema baada ya maelezo hayo walimtaka aende ofisi za TRA zilizopo mjini Babati kwa hatua zaidi jambo ambalo mfanyabiashara huyo alilitimiza kwa kufika ofisini hapo.

Alisema alipofika mjini Babati mfanyabiashara huyo alielezwa kuwa alikadiriwa chini ya kiwango hivyo anatakiwa kulipa kodi ya shilingi 450,000 kwa mwaka na faini ya shilingi milioni 3 kwa kutotumika mashine ya EFD.

“Mfanyabiashara huyo aliwaeleza maafisa hao kuwa hawezi kulipa fedha hizo kutokana na biashara aliyonayo, vinginevyo ni bora afunge tu biashara hiyo, baada ya kutoa msimamo huo ndipo akafahamishwa na Afisa Jackline Manjira wa TRA Babati ili asipigwe faini awape shilingi milioni moja,” alisema Makungu.

Alisema hata hivyo, kutokana na mwamko walionao wananchi wa Manyara kwa sasa mfanyabiashara huyo aliamua kutoa taarifa TAKUKURU na mtego wa shilingi milioni moja uliandaliwa ambao uliwezesha kukamatwa kwa watumishi hao.

Alisema uchunguzi unaonyesha kuwa baada ya watumishi hao kukabidhiwa fedha za mtego wa hongo Jackline Manjira na Eva Mtandika waliandika kwenye faili la mfanyabiashara huyo kuonyesha kuwa amesamehewa ongezeko la kodi na ununuzi wa mashine ya EFD hadi mwaka 2021.

“Tunatarajia kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao wakati wowote mara uchunguzi utakapokamilika, tunawataka TRA Babati na watumishi wa umma kwa ujumla wafahamu kuwa uadilifu siyo karama au kipaji ni uamuzi tu wa mtumishi wa umma,” alisema Makungu.

Makungu alitoa wito kwa wana Manyara na watanzania kwa ujumla kuendelea kutoa taarifa za rushwa kwa ofisi ya wilaya iliyopo karibu ambapo TAKUKURU wamefungua ofisi za wilaya kote Tanzania bara au wawasiliane nao kwa namba ya dharura 113.