Home Mchanganyiko RC MNYETI AIFAGILIA SIMANJIRO KWA HATI SAFI

RC MNYETI AIFAGILIA SIMANJIRO KWA HATI SAFI

0

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza nao Mji mdogo wa Orkesumet, yalipo makao makuu ya Halmashauri hiyo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Jackson Leskary Sipitieck akifungua kikao cha Baraza la madiwani juu ya hoja ya CAG.

************************************

MKUU wa Mkoa wa Manyara Alexander Pastory Mnyeti ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kwa usimamizi mzuri wa matumizi ya fedha za Serikali na kufanikisha kupata hati safi kwa miaka minne mfululizo ya utawala wa Rais John Magufuli. 
Mnyeti aliyasema hayo kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro cha kupitia taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali CAG kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2019 ambapo walipata hati safi. 
Alisema halmashauri hiyo chini ya madiwani wanaoongozwa na Mwenyekiti wao Jackson Sipitieck, mkurugenzi mtendaji Yefred Myenzi na mkuu wa wilaya hiyo Zephania Chaula wamefanikisha usimamizi mzuri wa fedha za serikali. 
Alisema kulingana na mfumo uliopo hivi sasa serikalini ni vigumu kufuja fedha fedha hivyo anaipongeza halmashauri hiyo kwa kuhakikisha inatumia fedha za serikali kwa namna ilivyopangwa. 
“Mtumishi wa serikali unapopewa nafasi ya kufanya kazi mahali kuwa muadilifu epuka kulamba fedha nanyi Simanjiro hongereni kwa usimamizi na matumizi ya fedha na kupata hati safi,” alisema Mnyeti. 
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Jackson Sipitieck alimpongeza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Yefred Myenzi kwa ushirikiano alionao na madiwani na watumishi hadi kufanikisha upatikanaji wa hati safi. 
“Tuna imani kubwa na Myenzi na hata mara baada ya baraza la madiwani kuvunjwa atasimamia vizuri halmashauri yetu ili madiwani watakaorudi mwezi Oktoba wakute hali ni shwari,” alisema Sipitieck. 
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula alisema mshikamano ulioonyeshwa unapaswa kuendelea ili upatikanaji wa hati safi uzidi kuwepo kwa kusimamiwa kwa miradi na fedha kwa njia ya uadilifu. 
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Yefred Myenzi alisema ofisi ya CAG imetoa hati safi kwa mwaka 2018/2019 na miradi yote ya uendelezaji maji vijijini, mradi wa afya na maendeleo ya jamii. 
Mweka hazina wa halmashauri hiyo Mkama Musese alisema hoja 17 hazijafungwa, hoja tisa ni za kiutendaji, hoja nane ni za kimfumo na utekelezaji wake unaendelea. 
Mkaguzi mkazi wa mkoa wa Manyara, Paschal Mahwago alisema atashirikiana na halmashauri hiyo kuhakikisha hoja ambazo hazina mashiko zinaondolewa. 
Diwani wa kata ya Loiborsiret Ezekiel Lesenga (Mardad) alisema kwa kipindi ambapo Mnyeti amekuwa mkoani humo wilaya ya Simanjiro ilitulia na kumaliza migogoro isiyo na tija.