Home Mchanganyiko KABATI AOMBA USHURU WA MAZIWA KUTOKA NJE UONGOZWE

KABATI AOMBA USHURU WA MAZIWA KUTOKA NJE UONGOZWE

0
……………………………………………………………..
NA SULEIMAN MSUYA
MBUNGE wa Viti Maalum mkoa wa Iringa, Rita Kabati ameiomba Serikali kuongeza kodi ya ushuru wa bidhaa ya maziwa kutoka nje ili kulinda viwanda vya ndani.
Aidha, Kabati ameipongeza Kampuni ya Kuzalisha Maziwa ya ASAS ya mjini Iringa kwa kutumia fursa ya kuongeza ushuru wa bidhaa kwa kuzalisha maziwa mengi.
Kabati ametoa ombi na pongezi hizo Bungeni jiini Dodoma wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyowasilishwa na Waziri wa Luhaga Mpina jana.
Mbunge huyo wa Viti Maalum alisema Waziri Mpina na wasaidizi wake wameweza kumpaisha Rais John Magufuli kupitia Wizara hiyo hivyo wanapaswa kuongeza nguvu.
“Tunaiomba Serikali iongeze ushuru wa bidhaa kwa maziwa yanayotoka nje ili kulinda viwanda vya ndani bei iwe chini viweze kujiendesha kwa faida,” alisema.
“Wananchi wengi wanaridhika na utendaji wa Wizara na Rais Magufuli hivyo nina imani watamchagua tena kwa kura nyingi,” aliongeza.
Mbunge huyo alisema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejitahidi kukuza sekta hiyo hivyo ombi lake ni ushuru wa bidhaa kuongezwa ili kukuza viwanda hasa vya maziwa.
Alisema sekta hiyo ni muhimu katika kukuza uchumi wa nchi na wananchi  kwa kuwa inashirikisha kundi kubwa la wavuvi na wafugaji.
Kabati alisema iwapo ushuru wa bidhaa utaongezwa wawekezaji wa nje ambao wamekuwa wakiingiza maziwa kutoka nje wataacha na kutumia yanazalishwa hapa nchini.
“Wawekezaji wanaingiza maziwa kutoka nje na kuuza bei mdogo na kuuwa viwanda vyetu vya ndani. Hili halikubaliki lazima tuongeze ushuru wa bidhaa,” alisema.
Mbunge huyo alitolea mfano Kampuni ya ASAS  ya mkoani Iringa ambayo imetumia fursa ya kuongeza ushuru wa bidhaa na kuzalisha maziwa mengi yanayotumika nchini.
 “ASAS imeweza kuinua kipato cha wafugaji wadogo wadogo wa Iringa, Njombe na Mbeya. Lakini ameenda mbali kwa kuwakopesha  ng’omba wa maziwa na ukiangalia yote haya ni uamuzi wa Serikali kuongeza ushuru wa bidhaa,” alisema.
Aidha, Kabati alisema Kampuni ya ASAS, imekuwa akitoa mchango mkubwa kwa kijamii ya mkoa huo.
“Mfano amejenga jengo la damu salama, jengo la ustawi wa jamii ,amekuwa akitoa maziwa kwa shule zote za Iringa sasa hivi ametoa vifaa na mashine na vifaa ya kusaidia madktari na wauguzi, barakoa, ndoo na sanizer maeneo ya masoko,” alisema.
Kabati alisema Serikali inapaswa kuunga mkono jitihada za wawekezaji wazawa kama ASAS ili kuvutia wengine kuwekeza katika sekta ya viwanda vya maziwa.