Home Mchanganyiko MASJID TAQWA YATAKA MAJUMBA YA STAREHE YANAYOHUSISHA MIKUSANYIKO YAFUNGWE

MASJID TAQWA YATAKA MAJUMBA YA STAREHE YANAYOHUSISHA MIKUSANYIKO YAFUNGWE

0
NA MWAMVUA MWINYI, BAGAMOYO
SERIKALI imeshauriwa kufunga majumba yote ya starehe,yanayohusisha mikusanyiko katika kipindi hiki cha toba kupitia ibada ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Hatua hiyo inatokana na umuhimu wa mwezi huu, unaoingia wakati huu ambao Tanzania na dunia nzima ipo katika maombi ya kunusurika kwa ugonjwa hatari wa Corona, ambao mpaka sasa wataalamu wanaangaika kuutafutia tiba.
Rai hiyo imetolewa na Sheikh wa Msikiti wa Masjid Taqwa uliopo Bagamoyo mjini Jambia Mwikali, ambapo alisema katika kupindi hiki cha maombi kwa Mwenyezimungu atuepushie janga lililopo, ni vema utulivu ukawepo.
“Niishauri Serikali katika kipindi hiki cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, majumba yote yanayojihusisha na mikusanyiko, unywaji wa pombe, bar zinazoweka maDJ wa muziki, kamali na kila matendo maovu ni vema yakadhibitiwa, ili kwa uwezo wake Mwenyeezimungu ugonjwa huu umalizike kabla ya kufika katikati ya mfungo,” alisema Sheikh Mwikali.
Kwa upande wake Imamu Msaidizi wa msikiti huo Nassoro Hamisi alisema kuwa ni vema kwa waumini wa dini ya Kiislamu wakashiriki katika mfungo wa mwezi wa Ramadhani, ili kupata nusura ya Mwenyeezimungu kupitia kipindi hiki cha siku 30.
“Nawaomba waumini wa dini ya Kiislamu popote walipo hapa nchini na duniani kwa ujumla, tutumie kipindi hiki cha ibada ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani tufunge kwa dhati, sanjali na kushiriki swala 5 sanjali na Tarawei,” alisema Imamu Hamisi.
Nae Imamu Msaidizi Kombo Makame amewashauri wa-Tanzania kujinyenyekeza kwa Mwenyeezimungu ili aweze kutuepushia janga hili kubwa la ugonjwa hatari wa Corona.