Home Mchanganyiko DC MLELE ATANGAZA UTARATIBU WA UNUNUZI WA MAZAO

DC MLELE ATANGAZA UTARATIBU WA UNUNUZI WA MAZAO

0

Mkuu wa wilaya ya Mlele mkoani Katavi Rechal Kassanda akitoa taarifa kuhusu kuanza kwa kazi ya ununuzi wa mazao ya wakulima katika msimu wa mwaka 2020 ambapo  wilaya hiyo yenye Halmashauri mbili ya Mlele na Mpimbwe imetenga jumla ya vituo 80 kwa ajili ya kununulia mazao.

***************************************

Na Mwandishi wetu
Katavi

WILAYA ya Mlele mkoani Katavi  yenye Halmashauri mbili za wilaya, imetenga  vituo 80 vya kununulia mazao mbalimbali katika msimu wa 2020  huku wilaya hiyo ikiwa ni mara ya kwanza  kuingia katika mfumo  rasmi wa stakabadhi gharani.

Kati  ya hivyo,Halmashauri ya Mpimbwe imetenga vituo 49 na Halmashauri ya wilaya Mlele imetenga vituo 31 huku wafanya biashara wakionywa kujiepusha kununua mazao  kwa  kutumia vipimo haramu.

Mkuu wa wilaya hiyo Rachel  Kassanda amesema hayo jana,wakati akiongea na wanunuzi wa mazao katika kikao kazi  kilichohudhuriwa na wafanyabiashara wa mazao na wataalam kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Mlele.

Kassanda aliyataja, mazao yatakayouzwa kupitia mfumo wa stakabadhi gharani ni ufuta na Alizeti ambapo mazao mengine kama mahindi,mpunga na karanga yatapelekwa katika vituo maalum vilivyotengwa.

Alisema,lengo la kuweka utaratibu huo ni kuongeza pato la wananchi wa wilaya hiyo  baada ya siku nyuma kuwepo kwa wimbi kubwa la wafanya biashara ambao walikwenda moja kwa moja kwa wakulima  shambani na kununua mazao, hivyo kuwaacha wakulima maskini licha ya juhudi kubwa wanazofanya.

Sambamba na hilo, amewataka wafanya biashara wote kuwa na leseni ya Halmashauri na kutumia mizani wakati wa ununuzi wa mazao na kujiepusha  kabisa  kutumia vipimo visivyo halali  kama madebu maarufu kama Mozambiki ambayo vinachangia sana kuwaibia  wakulima.

Kassanda ametahadharisha,mfanyabiashara atakayekamatwa ananunua mazao kwa kutumia vipimo visivyo rasmi na kutorosha mazao atalazimika kulipia ushuru wa mzigo aliokutwa nao, kupigwa faini ya shilingi laki tatu na kama hana leseni atalazimika kulipia leseni na kuwataka wafanya biashara kufuata  utaratibu uliowekwa na Halmashauri za wilaya.

Alisema, vyombo vyote vya ulinzi na usalama vitahusika katika kusimamia suala zima la ununuzi wa mazao  kwa msimu wa 2020 na hakutakuwa na huruma kwa mtu yeyote atakayekamatwa akitorosha mazao.

Alisema, wilaya imejipanga vema katika kukabiliana na wafanya biashara wajanja ambapo vimeundwa vikosi kazi ambavyo wakati wote vitakuwa makini katika kusimamia ununuzi wa mazao na katika vizuizi vyote ili kuepuka utoroshaji wa mazao na ulaghai unaofanywa na wafanya biashara kwa wasimamizi waliopo kwenye vizuizi.

Alisema, Alizeti na Ufuta yatauzwa kwa njia  ya mnada  kwenye vyama vya msingi vya ushirika na Amcos ambapo katika  Halmashauri ya wilaya Mlele kuna vyama vya msingi vya ushirika  vinne na Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe  vyama 7 ambavyo vitatumika kwa ajili ya kuuza na kununua mazao hayo.

Alisema, ili kukabiliana na udanganyifu unaofanywa na wanunuzi  kwa wakulima,Serikali kupitia Maafisa ushirika wamepewa elimu kuhusiana na faida  ya mfumo wa uuzaji mazao kwa njia ya stakabadhi gharani na umuhimu wa kutumia vipimo halali vilivyothibitishwa na Serikali.

Alieleza kuwa, serikali imeweka  kituo cha kununulia mazao kwa kila kitongoji kuweka mizani  ili kurahisisha uuzaji na ununuzi mazao na kila kituo kutakuwa na msimamizi hivyo hakuna udanganyifu unaoweza kutokea.

Kwa upande wake katibu tawala wa mkoa wa Katavi Abdala Malela alisema,  katika msimu wa mwaka huu wameanza kampeni ya  mkulima kuuza mazao yake kwa utaratibu wa stakabadhi gharani ambao utawasaidia sana wakulima  na Halmashauri kuongeza mapato yake.

Alisema, mwaka huu hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kununua mazao moja kwa moja kwa mkulima badala yake atakwenda katika vituo maalum vilivyoweka na kwenye vyama vya msingi vya ushirika na Amcos.

Kwa mujibu wa katibu Tawala,  utaratibu utakaotumika ni mkulima kupeleka mazao yake kwenye Amcos  na wafanyabiashara watashindanishwa  na wale  watakaoshinda ndiyo watapata nafasi  ya kununua mazao  katika mkoa huo.

Ameyataja mazao yatakaingizwa katika utaratibu wa stakabadhi gharani ni ufuta na Alizeti na mazao  ya chakula yatauzwa  katika vituo maalum vilivyowekwa na halmashauri husika.

Baadhi ya wakulima, wamepongeza utaratibu huo  kwa madai kwamba utathibiti vitendo vya wizi na udanganyifu unaofanywa na wanunuzi wa mazao ambao wanatumia vipimo visivyo rasmi jambo linalo changia wizi na dhuruma.

Debora Mwamba(50) ameiomba Serikali  kuimarisha mfumo huo kwa kuwa utaleta manufaa makubwa kwa mkulima sambamba na kuziwezesha Halmashauri kuongeza mapato yake ya ndani.

Alisema,utaratibu wa soko huria umechangia sana wakulima kuwa maskini  licha ya kazi kubwa wanayoifanya mashambani mwaka hadi mwaka  na kuchangia  hali zao za maisha kuwa duni na  kuwanufaisha wafanya biashara ambao hawana hata huruma na wakulima.