Home Mchanganyiko ZUNGU AIAGIZA BAGAMOYO KUFANYA UHAKIKI WA VIWANDA VYOTE VILIVYOPO WILAYANI HUMO

ZUNGU AIAGIZA BAGAMOYO KUFANYA UHAKIKI WA VIWANDA VYOTE VILIVYOPO WILAYANI HUMO

0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu (mwenye kofia mbele) akiingia ndani ya kiwanda cha Exel Chemical Ltd. kilichopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani kwa ajili ya kufanya ukaguzi kufuatia malalamiko ya wadau mbalimbali kuhusu uchafuzi wa mazingira. Hata hivyo uchunguzi unaendelea kuhusu tuhuma za kufanya kazi bila leseni na kukwepa kodi. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akikagua nyaraka mbalimbali za kiwanda cha Exel Chemical Ltd. cha wilayani Bagamoyo kinachodaiwa kukiuka taratibu mbalimbali zikiwemo jina la bidhaa kutofautiana na jina la kiwanda pamoja na uchafuzi wa mazingira ikiwemo kelele na vumbi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akingalia shehena ya mifuko ya unga wa kutengenezea rangi kutokana na mawe yaliyosagwa ambapo bidhaa hiyo imeandikwa Watercraft tofauti na jina la kiwanda la Exel Chemical Ltd. jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akitoa maelekezo kwa viongozi mbalimbali alipofanya ziara katika kiwanda cha kusaga mawe cha Exel Chemical cha wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ambapo ilibainika kiwanda hicho kinatumia jina tofauti na la bidhaa inayozalisha huku Serikali ikiendelea na uchunguzi na tuhuma za kufanya kazi bila leseni wala kulipa kodi.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)

………………………………………………………………………….

Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu ameiagiza Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kufanya uhakiki wa viwanda vyote vilivyopo wilayani hapa kubaini endapo vinaendeshwa kihalali au la.

Zungu ametoa agizo hilo leo wilayani hapa alipofanya ziara ya kukagua kiwanda cha Exel Chemical Ltd. kinachojishughulisha na kusaga mawe kwa ajili ya kutengenezea rangi kufuatia malalamiko kutoka kwa wadau wa mazingira pamoja kufanya zake shughuli kinyume cha taratibu.

Alisema kuwa Serikali inachunguza kubaini kiwanda hicho kinavyofanya shughuli zake kama inalipa kulipa kodi au leseni na kama wakibaini hailipi kodi hatua stahiki zitachukuliwa.

Katika ziara hiyo akiwa ameambatana na viongozi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) uongozi wa Wilaya hiyo Zungu alibaini jina la kiwanda ni Exel Chemical wakati bidhaa inayozalishwa ni Watercraft jambo ambalo linakwenda kinyume cha sheria.

Aidha, waziri huyo alisisitiza kuwa nchi inataka wawekezaji katika sekta ya viwanda wafanye kazi bila kubughudhiwa wala kuonewa na wala Serikali haitafunga kiwanda lakini sharti lazima wafuate sheria za nchi zikiwemo za mazingira.

“Viwanda hivi vinafanya kazi bila leseni na wakifanya hivi Serikali inakosa mapato, na Serikali ikikosa mapato halmashauri mtakosa ‘on source’ za kuendesha shughuli zenu sasa fanyeni auditing kubaini viwanda gani viko kihalali na vipi vipo kiharamu ili sasa tuanze kuchukua hatua ili walipe leseni kwa mafunfaa ya Taifa,” alisema Zungu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka alisema kuwa imebaini kiwanda hicho ambacho kipo karibu na makazi ya watu kinafanya shughuli zake kinyume cha taratibu za mazingira.

Dkt. Gwamaka alibainisha kuwa kutokana na ukaguzi uliofanyika imebainika kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikichafua hewa kwa kutoa vumbi na kuwa ni chanzo cha kelele jambo ambalo linatishia afya za wakazi wa eneo hilo.  

Hata hivyo bado uchunguzi kuhusu tuhuma mbalimbali zilizotolewa dhidi ya kiwanda hicho unaendelea ili kubaini ukweli na kuchukua hatua stahiki kwa mmiliki huyo.

Aidha Serikali kufuatia tuhuma hizo inaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini ni jina gani halisi la usajili wa kiwanda hicho pamoja na mwenendo mzima wa ulipaji kodi,