Home Mchanganyiko SHULE YA SEKONDARI MAPINGA YAONDOKANA NA UKOSEFU WA MAJI

SHULE YA SEKONDARI MAPINGA YAONDOKANA NA UKOSEFU WA MAJI

0
………………………………………………………………………………………………..
NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
WANAFUNZI 320 wa shule ya sekondari ya Kata ya Mapinga wameondokana na kero ya ukosefu wa maji uliokuwa ukiwakabili,baada ya taasisi ya It’s Time To Help Foundation Tanzania ikishirikiana na Feza Schools Tanzania kutekeleza mradi wa uchimbaji kisima kilichogharimu mil.12.
Ofisa Uhusiano wa Taasisi hiyo, Mbwana Kitendo akizungumza kwenye makabidhiano ya mradi huo alisema, taasisi hiyo ina utaratibu wa kutoa misaada kwa jamii katika sekta za afya, elimu na ustawi wa jamii,pia hutoa misaada kwa vituo vinavyohudumia watoto wanaotoka katika mazingira magumu.
“Ni kiu yetu kuona tunaipunguzia jamii baadhi ya changamoto hasa zinazowakabili watoto katika kujenga Taifa la kesho imara, baada ya kupata taarifa kuwa wanafunzi takribani 320 wa Shule hii mpya ya Sekondari wana changamoto kubwa ya ukosefu wa maji, tuliona umuhimu wa kuja kuwasaidia kupata huduma ya maji hasa ikizingatiwa kuwa maji ni uhai na ni uhitaji muhimu kwa mwanadamu yeyote”alisema. 
Kutatua changamoto hii kwetu ni mafanikio makubwa kwani tunaamini sasa wanafunzi watasoma kwa amani bila kufikiri tena changamoto ya kukosa maji na hii itawaongezea utulivu na ubunifu katika masomo yao” alieleza. Mbwana.
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ,Julius Mwanganda aliishukuru taasisi ya hiyo  na kuwa tayari kutoa msaada huo  kwani ni ukweli usiopingika kuwa Shule hiyo ilikuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji.
Alifafanua, hali hiyo iliyowaletea usumbufu mkubwa na kuwaondolea utulivu wanafunzi hasa wa kike na si wanafunzi tu hata walimu kwani maji ni huduma muhimu na ya msingi kwa mwanadamu yeyote mahali popote, hivyo utatuzi wa changamoto hii utaleta ufanisi mkubwa kielimu na utendaji kazi kwa ujumla shuleni hapo.
Kwa upande wake Mkuu wa shule ya sekondari Mapinga, Agnes Mmbaga alisema awali walikuwa wakitumia maji toka katika kisima cha kuchimba kwa mkono kilichochimbwa na walimu pembezoni mwa Shule hiyo, ambacho hakikuwa na maji ya uhakika wala salama kiafya, hali hii ilipelekea kupoteza muda mwingi kutafuta maji badala ya kutumia muda huo kwenye masomo.
Alibainisha, mradi huo wa maji ni ukombozi kwa wanafunzi na walimu wa Shule hiyo huku akiahidi kuutunza mradi huo ili uendelee kutoa huduma hiyo muhimu kwa muda mrefu.
Mmbaga anaongeza, “Shule yetu hii ina changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa, uzio, umeme, maabara, maktaba, matundu ya vyoo na Ofisi ya Walimu, hivyo nawaomba wadau wa elimu kufika katika Shule yetu na kutusaidia kutatua changamoto hizi.
Shule mpya ya Sekondari Mapinga,ilianza kujengwa mapema mwaka 2019 kwa nguvu za wananchi, Halmashauri na wadau wa maendeleo katika Kata hiyo na ilipata usajili Mwezi Januari mwaka huu.