Home Mchanganyiko Ep4r kukarabati Shule ya Ufundi ya Mwadui

Ep4r kukarabati Shule ya Ufundi ya Mwadui

0

*************************

Nteghenjwa Hosseah, Kishapu

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu OR-TAMISEMI Gerald Mweli amesema kupitia mradi wa lipa kulingana na matokeo Serikali itakarabato shule ya Sekondari ya Ufundi ya Mwadui.

Mweli ameyasema hayo wakati alipotembelea Shule hiyo na kubaini uchakavu mkubwa wa miundombinu ambapo mpaka sasa shule hiyo imeshindwa kutoa Elimu bora ya Ufundi kutokana na uchakavu huo katika madarasa pamoja na karakana.

Akizungumza katika ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu Mweli amesema amejionea uchakavu uliokithiri wa miundombinu ya Shule hiyo kitu ambacho kinaweza kupelekea hata wanafunzi kutofanga vizuri katika masomo kutokana na hali hiyo.

“Nimekuja hapa leo kujionea dhahiri ni kwa kiwango gani shule hii ni chakavu na jinsia ambavyo Serikali inaweza kuinusuru kwa kufanya ukarabati mkubwa utakaorudisha shule hii kwenye hadhi yake.

Elimu ya ufundi ni muhimu sana kwa watoto wetu haswa katika kipindi hiki ambacho Nchi inaelekea katika Uchumi wa Kati wa Viwanda ni lazima tuzalishe nguvu kazi yenye taaluma ya ufundi itakayosaidia katika viwanda vyetu” Alisema Mweli.

Aliongeza kuwa ufundi unasaidia kumjenga mtoto kuwa na Elimu ya kujitegemea sio lazima awe ameajiriwa hivyo shule hii ikifanyiwa maboresho na kutoa Elimu ya ufundi kwa wanafunzi wengi tutakua tumesaidia katika suala la ajira kwa vijana hao.

“Sasa kwa hali hii kupitia mradi wa lipa kutokana na matokeo “Ep4r” tutakarabati shule hii na kuirudisha kwenye hadhi yake na iendelee kutoa elimu ya ufundi wa watoto wanaochaguliwa katika shule hii na kazi hiyo itaanza hivi karibu”

Akizungumza katika Shule hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe· Nyabaganga Taraba amesema Majengo mengi ya shule ya Ufundi Mwadui yamechakaa na
mashine nyingi kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo zimekufa hivyo shule haitoe elimu ile iliyokusudiwa hapo awali.

“Shule hii ikikarabatiwa ni Mkombozi wa watoto wa Kishapu maana watapata ujuzi wa kutosha wa kuweza kuwasaidia katika maisha yao hapo baadae na ninaishukuru Serikali kwa kuona uchakavu uliopo na kuahidi kuikarabati nina uhakika kiwango chetu cha Elimu kitaongezeka baada ya ukarabati huo” alisema Taraba.

Naye Mkuu wa Shule ya Ufundi Mwadui amesema shule hiyo ilijengwa mwaka 1961 kwa ufadhili wa Mgodi wa Almasi wa Williamson na kwa sasa ina wanafunzi 800; Elimu ya ufundi inayotolewa kwa sasa ni ujenzi, uselemala, umeme na kuchonga vyuma.

Katika ziara hiyo pia Mweli alitembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mwadui ambayo pia iko kwenye hatua za ukamilishaji na itaanza kupokea wanafunzi hivi karibuni aliridhishwa na ukarabati unaoendelea na kumuagiza Mkuu wa Wilaya kuendelea na hatua za kuanza kutoa Elimu kwa watoto wa kike.