Home Mchanganyiko MAWAZIRI NA WADAU WA UTATU WA SADC SEKTA YA KAZI NA AJIRA...

MAWAZIRI NA WADAU WA UTATU WA SADC SEKTA YA KAZI NA AJIRA WAPONGEZA SERIKALI YA TANZANIA KWA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA TAIFA YA UKUZAJI UJUZI KWA VIJANA

0

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (wa pili kulia) akizungumza na Mawaziri na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira walipotembelea eneo la Kaole, Wilaya ya Bagamoyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (wa pili kulia) akiteta jambo na Waziri wa Kazi, Usalama wa Zambia Mhe. Joyce Simukoko walipokuwa wakiangalia eneo la Makaburi ya Wapendanao yaliyopo eneo la Kaole Wilaya ya Bagamoyo Machi 6, 2020.

Sehemu ya Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira wakiangalia eneo la kaburi la Imamu aliyekuwa na uwezo wa kutabiri mambo mbalimbali lililopo katika eneo la Kaole wilaya ya Bagamoyo.

Baadhi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira (waliokaa) wakiangalia kikundi cha Ngoma Asilia cha Kaole walipotembela Magofu ya Kaole yaliyopo eneo la Kaole wilaya ya Bagamoyo.

Waziri wa Kazi, Uzalishaji na Ukuzaji Ujuzi wa Botswana Mhe. Mpho Balopi (wa tatu kutoka kushoto) akipiga ngoma pamoja na wanakikundi cha ngoma asilia cha Kaole. Wa pili kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainab Kawawa.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde akieleza jambo kuhusu Programu ya Ukuzaji Ujuzi kwa Vijana kwa Mawaziri na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akikata keki pamoja na Mawaziri wa SADC sekta ya Kazi na Ajira walipotembelea Chuo cha Don Bosco kujionea utekelezaji wa Programu ya Ukuzaji Ujuzi. Kulia ni Waziri wa Kazi, Usalama wa Zambia Mhe. Joyce Simukoko na Waziri wa Kazi na Ajira Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Mhe. Ilunga Nkulu Nene (wenye miwani).

Baadhi ya Vijana wa fani ya umakenika waliopo katika chuo cha Don Bosco wakitengeneza vipuri vya magari wakati walipotembelewa na Mawaziri na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira.

PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU

(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)

*********************************

Na: Mwandishi Wetu

Mawaziri na Wadau wa Utatu wa Nchi Wananchama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) sekta ya kazi na ajira waipongeza Serikali ya Tanzania kwa mikakati iliyojiwekea katika kuwajengea uwezo vijana kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi.

Pongezi hizo zimetolewa na Mawaziri na Wadau wa utatu wa Jumuiya hiyo ikiwemo Jukwaa la Vyama vya Waajiri Kusini mwa Afrika (SPSF), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Kusini mwa Afrika (SATUCC), Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Shirika la Kimataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji kanda ya Kusini mwa Afrika (IOM).

Akizungumza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) na waandishi wa habari wakati wa ziara yake aliyoambatana na Mawaziri na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira walipotembelea Chuo cha Don Bosco Network kilichopo Oysterbay Jijini Dar es Salaam na Maeneo ya Vivutio vya Utalii Bagamoyo alieleza kuwa Serikali iliamua kuanzisha programu hiyo lengo ikiwa ni kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kuwajengea mazingira wezeshi na yanayowahamasisha kuajiriwa au kujiajiri.

“Mawaziri na Wadu wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira wamefurahia kuona namna Serikali inavyotekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuza kwa Vijana ambayo kwa kiasi kikubwa itawawezesha vijana kupata uwezo na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira kwa nchi hizo wanachama,” alisema Waziri Mhagama.

“Zipo nchi wananachama wameomba kukutana na Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inatekeleza programu hiyo kwa lengo la kuweza kupata uelewa wa taratibu na namna ya kutekeleza programu hiyo, nchi ya Eswatini tayari imeonyesha nia ya kukutana na ofisi yangu ili nao waweze kuanzisha programu hiyo nchini kwao,” alieleza Mhagama

Alieleza kuwa wakati wa uzinduzi rasmi wa Mkutano huo wa Mawaziri na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira uliozinduliwa Machi 5, 2020 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Serikali iliona umuhimu wa kuzindua Programu mmoja wapo ambayo ni Programu ya Mafunzo ya Vitendo Mahala pa Kazi (Internship) ili kuelezea nchi wanachama mikakati ambayo Serikali imejiwekea katika kutatua changamoto ya ajira inayowakabili vijana kwa kuwawezesha vijana kuwa na uzoefu katika utendaji kazi.  

Aidha aliongeza kuwa katika mkutano huo uliowakutanisha waliweza kujadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya Kazi na Ajira ambazo ni masuala ya Hifadhi ya Jamii, Uhamishaji wa nguvu kazi, mapitio ya sera na miongozo iliyotungwa na nchi wanachama kuhusu masuala ya kazi na ajira, haki na wajibu wa wafanyakazi, mapitio ya mikataba ya kimataifa na mikataba ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) inayoongoza masuala ya ajira pamoja na kuwajengea uwezo vijana.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Anthony Mavunde wakati akielezea kuhusu programu ya ukuzaji ujuzi kwa Mawaziri na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira alieleza kuwa Programu hiyo ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inafadhiliwa na Serikali kwa lengo la kuwawezesha vijana ambao kwa asilimia kubwa ndio nguvukazi ya taifa wanapata ujuzi na uzoefu ambao utawafanya waweze kujitegemea.  

“Hii ni habari njema kwa sisi Watanzania kutembelewa na Mawaziri na Wadau wa Utatu ambao wamekuja kujionea namna serikali yetu inavyowajali vijana na jinsi inavyowatumikia katika kuwawezesha kupata ujuzi ambao utawasaidia pindi vijana hao wanapomaliza mafunzo waweze kujiajiri ama kuajiriwa,” alisema Mavunde

Alifafanua kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu Programu ya Ukuzaji Ujuzi ikiwemo Mafunzo kwa Njia ya Uanagenzi, Mafunzo ya Urasimishaji Ujuzi uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi, Mafunzo ya Vitendo Mahala pa Kazi kwa Wahitimu na Mafunzo ya Ukuzaji Ujuzi kwa walio Makazini na Mpango huo wa Urasimishaji Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi (Recognition of Prior Learning). 

Katika ziara hiyo Mawaziri na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira walipata fursa ya kutembelea maeneo ya kihistoria yaliyopo Bagamoyo ikwemo Ngome Kongwe, Soko la zamani la Watumwa, Bandari iliyokuwa inatumika kuwasafirisha watumwa, eneo la Msalabani ambapo Ukristo ulianzia kuenezwa hapo na wakoloni, Magofu ya Kaole lengo la ziara hiyo ilikuwa kutangaza maeneo ya vivutio vya kihistoria vilivyopo hapa nchini.

Waziri wa Kazi na Ajira Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Mhe. Ilunga Nkulu Nene alieleza kuwa wamevutiwa sana na maeneo ya kihistoria yaliyopo Tanzania na ni nchi ya kuigwa.

“Nchi ya Kongo ina maeneo mengi ya kitalii lakini hatuyatangazi kama Tanzania inavyofanya, kama kiongozi nimejifunza jambo katika ziara ya leo na hivyo nitakaporudi Kongo nitahamasisha utangazaji wa maeneo ya kihistoria yaliyopo kwa lengo la kuvutia watalii,” alisema Nene