Home Mchanganyiko TAKUKURU YAKAMILISHA UCHUNGUZI WA MAKUBALIANO YA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI NA...

TAKUKURU YAKAMILISHA UCHUNGUZI WA MAKUBALIANO YA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI NA KAMPUNI YA ROM SOLUTIONS KWA ASILIMIA 99.9

0

*************************

NA EMMANUEL MBATILO

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU imekamilisha Uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola na aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ,Thobias Andengenye.

Uchunguzi huo kwa watuhumiwa hao ulihusu kusainiwa kwa mkataba wa ununuzi wa vifaa vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wenye thamani ya zaidi ya shilingi Trilioni moja kinyume cha sheria.

Akizungumza na Wanahabari Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo , Brig.Jen.John Mbungo amesema kuwa baada ya maelekezo ya Mhe.Rais, TAKUKURU ilianzisha uchunguzi kwa kukusanya vielelezo na kufanya mahojiano na watu mbalimbali kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jeshi la zimamoto na Uokoaji, Watumishi wa Serikali pamoja na makampuni husika katika MoU hiyo.

“Uchunguzi huu ulilenga kuthibitisha iwapo kuna uwezekano wa baadhi ya watumishi kufanya uzembe kwa kutotekeleza majukumu yao ipasavyo na kutozishauri Mamlaka zao kuhusu taratibu mbalimbali za usajili wa makampuni pamoja na uzingatiwaji wa sheria ya Ununuzi wa Umma?”. Amesema Brig.Jen.Mbungo.

Aidha Brig.Jen.Mbungo amesema kuwa katika makosa hayo yanaangukia katika makosa ya ujumu uchumi ambayo kisheria TAKUKURU haitakuwa na mamlaka ya kuyafikisha mahakamani .Kitakachofanyika ni kuwasilisha jalada la uchunguzi katika ofisi ya Taifa ya Mashitaka ili kwa kibali chake watuhumiwa waweze kufikishwa mahakamani.

Pamoja na hayo Brig.Jen.Mbungo amesema kuwa wapo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha uchunguzi huo ambapo baada ya wiki moja watakuwa tayari kwa kukabidhi jalada hilo katika ofisi ya Taifa ya Mashitaka.