…………………………………………………..
Na Robert Hokororo, Singida
Wakati Serikali inaendelea kuweka utaratibu wa kupata mbadala wa matumizi ya
zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu imeshauri watumie vifaa
vinavyowakinga wakati wakifanya shughuli hizo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Mussa Sima wakati akizungumza na wachimbaji wadogo kwa
nyakati tofauti katika vijiji vya Sambaru wilayani Ikungi na Londoni wilayani
Manyoni mkoani Singida.
Sima alisema kuwa Serikali inaendelea na kuwapa elimu wachimbaji hao katika
maeneo mbalimbali nchini ili waweze kuepuka madhara ya kiafya yanayotokana
na kemikali hiyo.
“Tanzania tuliridhia Mkataba wa Minamata mwaka jana unaotaka kupunguza
ama kuondoa kabisa matumizi ya zebaki kwa ninyi wachimbaji ili kuwaepusha
madhara ya kiafya na kimazingira katika maeneo yenu,” alisema naibu waziri.
Akiwa katika ziara hiyo ambapo alitembela kuona shughuli za uchimbaji na
kukagua namna wanavyotunza mazingira, Sima alisema kuwa jukumu la Serikali
ni kutoa elimu juu ya madhara ya zebaki ili kulinda afya za wachimbaji wadogo.
“Niwaahidi tu tutashirikiana na Ofisi ya Madini ili muweze kupata vifaa maalumu
vya kujikinga wakati wa kuchenjua badala ya mikono, tutawaletea gloves mvae
mikononi na musk wakati tunachoma ili kufunika pua kwani kemikali hii ina
madhara kiafya,” alisema.
Aidha, Naibu waziri aliwataka wachimbaji hao kuacha kukata miti wakati wa
shughuli za uchimbaji wa dhahabu na badala yake wawe na utamaduni wa
kutumia njia mbadala kama ambavyo wanavyoelekezwa na mamlaka
zinazohusika.
Aliongeza kuwa jukumu la Ofisi ya Makamu wa Rais na Serikali kwa ujumla ni
kuhakikisha nchi inakabiliana na changamoto ya mabadilkko ya tabianchi na
hivyo kuleta athari.
Alisema tunapoendelea kuchoma na kukata miti ovyo, kulima kholela na
kuchimba mashimo ovyo kwa ajili ya madini ni mambo yanayosababisha mvua
isije kwa wakati pamoja na jua kuwa kali kuliko kawaida.