Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy
Mwalimu akiwasili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kuangalia
changamoto mbalimbali wagonjwa wanazokutana nazo wakati wa kupatiwa
huduma, kushoto ni Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-
Mloganzila Dkt. Julieth Magandi na katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za
Uuguzi MNH-Mloganzila, Sr. Redemptha Matindi.
Mh. Ummy Mwalimu akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili
hospitalini hapa, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH), Prof Lawrence Museru.
Mh. Ummy Mwalimu na Prof. Lawrence Museru wakimsikiliza Bi. Anna
Msaki akielezea namna anavyopatiwa matibabu hospitalini hapa.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba katika Hospitali ya MNH-Mloganzila,
Dkt. Mohamed Mohamed akifafanua namna wataalam wa afya wanashirikiana
katika kutoa huduma hospitalini hapa.
Mh. Ummy Mwalimu akitoa mapendekezo ya namna eneo maalum la kupumzikia ndugu wanaosubiria miili ya wapendwa wao (Mochwari) linavyoweza kuboreshwa zaidi.
****************************
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu amewataka watanzania kuwa na imani na huduma za afya zinazotolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila.
Waziri Ummy ameyasema hayo leo mara baada ya kufanya ziara hospitalini hapa kwa lengo la kufahamu changamoto mbalimbali ambazo wagonjwa wanakutana nazo wakati wa kupatiwa huduma.
Hatua ya Waziri Ummy Mwalimu kutembelea Hospitali ya Mloganzila imekuja kutokana na malalamiko yanayotolewa na baadhi ya wananchi kupitia mitandao ya kijamii kuhusu huduma zinazotolewa hospitalini hapa kuwa ni za chini ya
kiwango.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Waziri huyo amesema amejionea huduma zikiendelea kutolewa na timu ya wataalam wa afya ngazi zote na kusisitiza kuwa Mloganzila sio ‘chinja chinja’ ni hospitali inayotoa huduma nzuri kama ilivyo Hospitali ya Muhimbili-Upanga.
“Nimekuja kupata ukweli juu ya malalamiko yanayotolewa na nimeshuhudia utaratibu uliopo hapa daktari mwanafunzi anafanya kazi chini ya usimamizi wa
daktari bingwa tofauti na inavyodaiwa na watu kuwa wanaotibu wagonjwa katika hospitali hii ni madaktari wanafunzi pekee kitu ambacho si kweli” amefafanua Mh.
Ummy Mwalimu.
“Pia imepata fursa ya kuongea na wagonjwa wa ndani na wa nje kwa nyakati tofauti ambao wameelezea kuridhishwa na huduma wanazopata katika hospitali
hii” Akielezea kuhusu gharama za matibabu amesema matibabu yanagharama na ndio maana serikali inaona umuhimu wa kila mtanzania kuwa na bima ya afya na
kuongeza kuwa ni marufuku kwa hospitali za Umma nchini kutompatia huduma mgonjwa kwa sababu ya kukosa pesa za matibabu.
“Kwa hili niwapongeze Muhimbili kwani mnatekeleza kwa asilimia 100 mnaanza kutoa huduma kwanza kisha malipo mnadai baada ya mgonjwa kupata huduma” amesema Mh. Ummy Mwalimu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof Lawrence Museru ameeleza kuwa kimsingi mafunzo ya wataalam wa afya yanafanyika hospitalini kwani bila mtaalam kufika hospitalini hawezi kupata ujuzi unaotakiwa.
“Mafunzo ya wataalam wa afya ni muhimu kwani wasipopata mafunzo hospitalini hawatapata ujuzi hivyo lazima tukubali suala la kutoa mafunzo kwa wanafunzi
kwani ndivyo wataalam wote wa afya wanavyofundishwa huku wakiwa chini ya usimamizi” amesema Prof. Museru.
Katika ziara hiyo Waziri wa Afya amepata fursa ya kutembelea baadhi ya maeneo ya hospitali ikiwemo wodini, kliniki ya wagonjwa wa nje pamoja na mochwari.