Home Mchanganyiko TMA YATOA TAHADHARI NA USHAURI KWA WADAU KUHUSU MSIMU WA MVUA ZA...

TMA YATOA TAHADHARI NA USHAURI KWA WADAU KUHUSU MSIMU WA MVUA ZA MASIKA MACHI HADI MEI 2020

0

Rose Senyagwa Mtaalam wa hali ya hewa kutoka TMA wakati akitoa taarifa ya utabiri  wa hali ya hewa msimu uliopita kabla ya kumkaribisha Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk. Agnes Kijazi jana katikati ni Dk. Hamza Kabelwa Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA.

…………………………………………………

Taarifa ya Utabiri wa Mwelekeo wa mvua za masika katika msimu wa Machi hadi Mei 2020 iliyotolewa jana na Malmaka ya Hali ya Hewa Nchini TMA imetoa ushauri kwa wadau na kusema kunaweza kutokea  athari kutokana na mvua hizo.

Mamaka hiyo imetoa ushauri  katika taarifa iliyoandaliwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa kushirikiana na wataalam wa sekta husika katika mkutano wa wadau wa hali ya hewa uliofanyika tarehe 11 Februari, 2020.

Katika ushauri huo wa TMA taarifa hiyo ikielezea Kilimo, Usalama wa Chakula, Samaki na Mifugo imesema Maeneo yanayotarajiwa mvua za wastani hadi juu ya wastani mvua zinaweza kufaa kwa uzalishaji wa mazao ikiwa ni pamoja na yale yanayoweza kustawi kwenye unyevunyevu wa udongo uliopitiliza kama vile mpunga.  Wadudu waharibibu na magonjwa vinaweza kujitokeza kutokana na hali ya umajimaji na maji yaliyotuama. 

“Uzalishaji wa mifugo pamoja na mazao ya mifugo kama vile maziwa vinatarajiwa kuimarika kutokana na kuwepo kwa malisho na maji ya kutosha katika maeneo mengi. Hata hivyo, magonjwa ya mifugo kama vile homa ya bonde la ufa, ugonjwa wa kwato na midomo yanaweza kujitokeza. Wakulima wanashauriwa kuchukua hatua stahiki za kudhibiti mmomonyoko wa udongo na kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza” Imeeleza taarifa hiyo ya hali ya hewa. 

Imesema Sekta ya uvuvi inaweza pia kuathirika kutokana na uwezekano wa ongezeko kubwa la maji katika mabwawa ya kufugia samaki, hivyo wafugaji wa samaki wanashauriwa kuimarisha miundombinu ya mabwawa yao. 

Aidha, katika maeneo ambayo mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa, wakulima wanashauriwa kupanda mazao yanayokomaa mapema na yasiyohitaji maji mengi katika ukuaji wake. Jamii inashauriwa kuhifadhi malisho na kuvuna maji ya mvua kwa matumizi ya baadaye.

Kwa upande wa sekta ya Nishati, Madini na Maji taarifa hiyo imesema Upatikanaji wa maji ya kutosha unatarajiwa hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Vina vya maji katika mabwawa na mtiririko wa mito vinatarajiwa kuimarika. Hata hivyo, athari hasi zinaweza kujitokeza kwenye miundombinu ya rasilimali maji. Kwa upande wa shughuli za wachimbaji wa madini wadogo wadogo, tahadhari za kiusalama zinashauriwa kuchukuliwa kutokana na hali ya maji mengi kwenye udongo inayoweza kusababisha maporomoko ya udongo na machimbo ambavyo vinaweza kusababisha kupoteza maisha na mali. 

Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA katika taarifa yake hiyo imeongeza kuwa Mamlaka za Miji zinatahadharishwa kuwa  Miundombinu na huduma za maji safi na maji taka zinaweza kuathirika, hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani. Aidha, ubora wa maji yanayotumika kwa matumizi mbalimbali unaweza kupungua kutokana na mvua zinazotarajiwa.

Mamlaka za Miji pamoja na wananchi wanashauriwa kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa miundombinu pamoja na njia za kupitisha maji zinakuwa wazi na safi ili kuepusha mafuriko na athari nyingine zinazoweza kutokea kutokana na maji kutuama.

Katika ya Sekta ya Afya taarifa hiyo imesema Mvua za wastani hadi juu ya wastani zinazotarajiwa, zinaweza kusababisha kutuama kwa maji na kuweka mazingira mazuri kwa mazalia ya mbu na hivyo kupelekea matukio ya kuwepo na kuongezeka kwa ugonjwa wa malaria. Aidha, kwa maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, kuna uwezekano wa jamii kutumia maji ambayo sio salama na hivyo kupelekea kuwepo kwa magonjwa ya milipuko mfano ugonjwa wa kuhara na homa ya matumbo.

Hivyo, jamii na mamlaka husika wanashauriwa kuchukua hatua stahiki ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa mamlaka za maafa na wadau kwa ujumla wanashauriwa kuchukua hatua stahiki za kujiandaa na kukabiliana kikamilifu na athari zinazoweza kujitokeza  kwakuwa Mvua kubwa inaweza kupelekea mafuriko na hivyo kusababisha upotevu wa maisha, uharibifu wa muindombinu na mali nyingine. Hivyo.

Katika taarifa hiyo Ushauri unatolewa kwa vyombo vya habari kufuatilia mara kwa mara na kusambaza taarifa sahihi za mienendo ya hali ya hewa na mirejeo pamoja na tahadhari na ushauri zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Wanahabari wanahimizwa kutafuta na kutumia maelezo ya wataalam wa sekta husika katika kuandaa na kufikisha taarifa za masuala mtambuka ya hali ya hewa kabla ya kuzifikisha kwa jamii.

Pia waandishi wanashauriwa kubadilishana taarifa za hali ya hewa miongoni mwao. Ushauri unatolewa kwa Mamlaka za Udhibiti wa Mawasiliano kudhibiti kusambaza kwa taarifa zinazopotosha na kusababisha taharuki kwa jamii.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Wasafirishaji, Mamlaka za Maji na Afya kuendelea kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika.