Home Mchanganyiko KUKAMATA SILAHA MOJA – PISTO NA KUPATIKANA NA MADINI BANDIA.

KUKAMATA SILAHA MOJA – PISTO NA KUPATIKANA NA MADINI BANDIA.

0

*****************************

Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya limekamata silaha moja Pistol aina Beretta Nambari H44675Y na CAR – 00098503 ikiwa na risasi 07 ndani ya Magazini.

 

Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 13.02.2020 majira ya saa 17:00 jioni huko Mtaa wa Sae uliopo Kata ya Ilomba, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya ambapo Kijana VICTOR
MWASOPO [17] mkazi wa Sae alikamatwa na silaha hiyo baada ya kutaka kuvamia kibanda cha M- PESA cha SAUDA DANDA [23] mfanyabiashara na mkazi wa Sae.

 

Ambapo alishambuliwa na kundi la wananchi na wakati anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya alifariki dunia.

Awali VICTOR MWASOPO alichukua silaha hiyo Pisto na kwenda kwenye kibanda cha M-PESA cha SAUDA DANDA na alipofika alikuwa amebeba silaha hiyo kwenye mifuko ya vifungashio akawa ameiweka mezani na kumuuliza huyo dada “wewe ni wakala wa NMB” akawa ametoa Pisto na kumtaka huyo dada ampe laki tano [500,000/=] huku akiwa amemnyooshea silaha.

 

Katika harakati hizo alitokea mtu mmoja akaja akiongea huduma kwenye kibando hicho, ghafla VICTOR MWASOPO alirudisha silaha hiyo katika mfuko na kutoka nje na
kumwambia dada SAUDA DANDA amwandalie hela anakuja kuchukua akawa ametoka na kuzunguka kwa nyuma akikimbia na ndipo dada SAUDA DANDA alitoka na kuanza kupiga kelele za mwizi, marehemu alikimbia na kwenda kujificha kwenye pipa la taka na kujifunika na taka.

 

Alipokamatwa alikutwa na silaha Pisto na risasi saba [07].
Uchunguzi wa awali unaonyesha silaha hiyo ni mali ya WAJINA ALICK MWASOPO ambaye ni baba yake mzazi na marehemu.

Aidha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH MATEI anatoa wito kwa wamiliki wa silaha kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili silaha zisiingie mikononi mwa wahalifu.

 

Pia anatoa onyo kwa wezi wa kutumia silaha kuacha mara moja, vinginevyo kwa Mkoa wa Mbeya hawatatoka salama. Aidha Kamanda MATEI anatoa wito kwa jamii kuacha
kujichukulia sheria mkononi, watuhumiwa wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili 1. JOSEPH SINGOGO [32] Mkazi wa Nkangamo na 2. JACOB MWANGOSI [42] Mwalimu wa Shule ya Msingi
Nkangamo wote wa Wilaya ya Momba Mkoani Songwe wakiwa na madini bandia.

 

Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 11.02.2020 majira ya saa 16:30 jioni huko katika Soko Kuu la Dhahabu lililopo Wilayani Chunya ambapo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na maafisa madini wa Wilaya hiyo waliwakamata watuhumiwa wakiwa katika harakati za kuuza madini hayo bandia waliyodai kuwa ni dhahabu yenye uzito wa gram 675.20 kwa mteja aliyefahamika kwa jina la PAUL HENRY GAGALA Mkazi wa Chunya Mjini ambaye ni mfanyabiashara ya madini.

 

Kama dhahabi hiyo ingekuwa halali, kwa siku hiyo ingekuwa na thamani ya Tshs.Milioni sabini [Milioni 70,000,000/=].

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH MATEI anatoa wito kwa Watanzania wote ili kutotapeliwa wasinunue/kuuza dhahabu nje ya masoko yaliyoidhinishwa na Serikali ambapo kuna wataalamu waliobobea katika fani hiyo
ambao wanatumia vifaa vya kisasa.

 

Aidha Kamanda MATEI anatoa wito kwa Watanzania
wote wanaopenda kufanya biashara hii wapate elimu yakutosha kuhusiana na madini.