Home Mchanganyiko Kondomu bado ni njia madhubuti ya kuzuia maambukizi ya magonjwa ya ngono...

Kondomu bado ni njia madhubuti ya kuzuia maambukizi ya magonjwa ya ngono na mimba zisizopangiliwa

0

Mkurugenzi wa Bidhaa na Huduma kwa Jamii T-Marc Tanzania Bw. Flavian Ngole Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya  shirika hilo kuhusu siku ya kimataifa ya kukuza uelewa juu ya matumizi ya Kondom  Kushoto ni Bi Geraldine Duwe Meneja Rasilimali watu na Ugavi.

Mkurugenzi wa Bidhaa na Huduma kwa Jamii T-Marc Tanzania Bw. Flavian Ngole Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya  shirika hilo kuhusu siku ya kimataifa ya kukuza uelewa juu ya matumizi ya Kondom  kulia ni Larson Chumi Meneja Mauzo na Kushoto ni Bi Geraldine Duwe Meneja Rasilimali watu na Ugavi.

Waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi wa Bidhaa na Huduma kwa Jamii T-Marc Tanzania Bw. Flavian Ngole Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya  shirika hilo kuhusu siku ya kimataifa ya kukuza uelewa juu ya matumizi ya Kondom.

……………………………………

Ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya Kukuza Uelewa Juu ya Kondomu. Ni muda wa kuhamasisha juu ya matumizi ya kondomu na kuwaelimisha watu juu ya umuhimu wa kufanya ngono salama muda wote. Lengo ni kuwafanya watu zaidi wawe huru katika kununua, kubeba, na kuzungumza juu ya kondomu na matumizi yake wakati wa kufanya mapenzi.

Ikiwa na kauli mbiu yenye kuangalia umuhimu wa ridhaa ya kutumia kondomu na pia upimaji wa magonjwa yanayoambukizwa kupitia ngono ikijumuisha virusi vya VVU na Ukimwi miongoni mwa wapenzi, maadhimisho haya hufanyika kila tarehe 13 mwezi wa pili siku moja kabla ya Siku ya Wapendanao Duniani (Valentine’s Day)

Wote tunajua furaha inayoambatana na siku hii duniani kote. Tunadhani ni muda mzuri wa kuhamasisha juu ya mahusiano mazuri na salama na kuwakumbusha watu juu ya hatari za magonjwa yanayoambukizwa kwa ngono na mimba zisizopangiliwa. Kwa kifupi, tunaitumia siku hii kama fursa ya kukumbusha kila mtu kuhakikisha kuwa anafanya mapenzi salama.

Mbali ya hilo, Siku ya Kimataifa ya Kukuza Uelewa Juu ya Kondomu ni ukumbusho wa umuhimu wa kutumia kondomu kwa usahihi ili kujilinda na maambukizo ya magonjwa yanayoambukizwa kwa ngono na mimba zisizopangiliwa.

Pia, bado kuna kundi kubwa la watu bado halijui kuwa unaweza kupata kondomu bure katika kliniki za maeneo yao, vituo vya afya na katika taasisi nyingine. Wengine wanasikia aibu kwenda kwenye maduka na kuulizia pamoja na kununua kondomu pale wanapozihitaji.

Kwa hiyo siku hii inatumika kwa ajili ya kupinga unyanyapaa huu ambao unahatarisha maisha ya watu wengi sana hususan vijana na wanawake ambao wapo kwenye hatari kubwa. Watu wanatakiwa wawe na uwezo wa kufanya maamuzi yao wenyewe na ridhaa zao na kujifunza namna ya kutumia kondomu kwa usahihi kutoka katika maeneo haya na wakati huo huo wapate majibu ya maswali yao mbali mbali yanayohusu afya ya uzazi na masuala ya ngono salama.

Kwa hapa T-MARC Tanzania tumekuwa tukifanya kazi kwa ukaribu na Serikali na wadau wengine katika kuboresha sekta ya afya ya umma na ustawi wa Watanzania kwa kujenga ubia imara na programu kuhakikishia uwezo wa kufikia huduma na bidhaa muhimu za afya zenye gharama nafuu na ubora.

Tunafanya kazi katika afua kadhaa za masuala ya afya ikijumuisha VVU/UKIMWI, afya ya uzazi/uzazi wa mpango, malaria, saratani ya mlango wa uzazi, lishe na usafi wa mazingira na usafi binafsi wa watu.

Programu zetu zinatumia njia za kibunifu kuwafikia Watanzania wote hususan wale ambao hawajafikiwa na huduma muhimu kupitia njia utolewaji wa huduma na bidhaa za kijamii na mawasiliano. Kupitia utoaji huduma na bidhaa za kijamii, tunatoa na kuhamasisha matumizi ya bidhaa na huduma mbali mbali zenye ubora kama vile kondomu huku walengwa wakuu wakiwa ni watu walio katika makundi yaliyopo kwenye hatari kubwa ya maambukizi.

Tunaposherehekea Siku ya Kimataifa ya Kukuza Uelewa Juu ya Kondomu kwa mwaka 2020, tungependa kuwashukuru wadau wetu wote kwa kuiwezesha T-MARC Tanzania kutoa huduma na bidhaa bora na kwa wakati kwa wale wenye uhitaji na hivyo kuchangia katika kuzuia maambukizi ya magonjwa ya ngono na mimba zisizopangiliwa nchi  nzima.

Katika kusaidia juhudi za Serikali kwenye kuzuia maambukizi ya VVU/UKIMWI, mimba zisizopangiliwa na magonjwa ya ngono, T-MARC Tanzania kupitia utoaji huduma na bidhaa kwa jamii inahamasisha ununuzi na matumizi juu ya aina mbali mbali ya kondomu na zenye sifa tofauti tofauti inazozitoa ili kuwapa watu fursa ya kuchagua. Miongoni mwa bidhaa hizo ni kondomu za kiume Dume Classic – ambayo haina manukato, Dume Desire ambayo ina manukato ya matunda ya aina ya strawberry, na Dume Extreme, ambayo ina vipele na harufu ya pipi kifua pamoja na Lady Pepeta ambayo ni kondomu maalum kwa ajili ya wanawake. 

Wote wanaume na wanawake wanatakiwa wawe huru katika kuridhia na kufanya maamuzi juu ya matumizi ya kondomu ili kujilinda. Pia wahamasishwe na kusaidiwa kwenda kufanya upimaji wa hiari wa magonjwa yanayoambukizwa kupitia ngono na kupewa msaada pale unapohitajika.

Tuaamini kwa pamoja tunaweza kufanikiwa kuisaidia Tanzania katika juhudi zake za kuboresha afya ya umma na ustawi wa Watanzania wote hususan wale walio kwenye hatari kubwa ya maambukizi hususan vijana na wanawake. Kila mmoja atekeleze wajibu wake!