Home Mchanganyiko MAPATO YAWAWEKA ‘KIKAANGONI’ WAKURUGENZI NA WEKAHAZINA

MAPATO YAWAWEKA ‘KIKAANGONI’ WAKURUGENZI NA WEKAHAZINA

0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa  taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha nusu mwaka (Julai – Disemba, 2019) kwa mwaka wa fedha 2019/2020 jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo,akifafanua jambo kwa  waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa  taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha nusu mwaka (Julai – Disemba, 2019) kwa mwaka wa fedha 2019/2020 jijini Dodoma.

PICHA NA ALEX SONNA-FULLSHANGWEBLOG

………………………………………………………………………………….

Na.Alex Sonna,Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo,amewataka wakurugenzi na wekahazina wa mamlaka ya serikali za mitaa ambao halmshauri zao hazijafikia  malengo waliojiwekea kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani mpaka kufikia mwisho mwa mwaka huu wa fedha wajitathimini katika utendaji kazi wao kabla ya 18 Juni,2020.

Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dodoma alipokuwa akitoa  taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha nusu mwaka (Julai – Disemba, 2019) kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

 Mhe. Jafo amesema kuwa wakurugenzi wa halmashauri ambazo hazitafikia malengo 18 Juni,2020 atapeleka mapendekezo kwa Mamlaka husika ili waweze kuchukuliwa hatua stahiki kwa kushindwa kukusanya mapato ikiwa sehemu ya jukumu lao na kurudisha nyuma jitihada za Serikali katika kuinua uchumi wa taifa.

“Hivyo  napenda kuweka wazi kuwa Mamlaka ya Wekahazina yako chini ya Ofisi yangu yeyote atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake kwa ufasaha atapisha nafasi hiyo ili wapatiwe watu wenye uwezo wakutekeleza majukumu hayo kwa ubora na kiwango kinacho hitajika”, aamesisitiza Jafo

Aidha Mhe. Jafo amesema ukusanyaji wa Mapato zilipanga kukusanya Shilingi Bilioni 765.48 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani na kipindi cha nusu mwaka (Julai hadi Desemba, 2019) Halmashauri zimekusanya Jumla ya Shilingi bilioni 356.81 ambayo ni asilimia 47 ya makisio ya mwaka.

Jafo amesema kuwa taarifa za mapato ya vyanzo vya ndani katika kipindi cha Julai – Desemba, 2019 umeonesha kuwepo kwa ongezeko la mapato yaliyokusanywa kwa kiasi cha  Shilingi bilioni 56.7 ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa katika kipindi kama hicho cha Julai – Desemba, 2018 sawa na ongezeko la asilimia 19.

“Uchambuzi unaonesha kuwa Halmashauri 63 kati ya Halmashauri 185 zimekusanya mapato ya ndani kwa asilimia 50 na zaidi ya makisio kwa Mwaka wa Fedha 2019/20 na halmashauri mia ishirini na mbili (122) zimekusanya mapato ya ndani chini ya asilimia 50 ya makisio ya mwaka” amebainisha Mhe.Jafo.

Pia Mhe. Jafo ameweka wazi kuwa Halmashauri hukusanya mapato mengi au kidogo kwenye vyanzo tofauti kulingana na hali halisi ya shughuli za kiuchumi za kila Halmashauri hivyo, ongezeko hilo limetokana na sababu mbalimbali ikiwemo ushuru wa zao la Korosho katika Halmashauri za Mikoa ya Mtwara na Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma.

Kwa kuongezea  Mhe. Jafo amesema kuwa katika kipindi cha miezi sita (Julai – Desemba, 2019), Halmashauri za Wilaya za Tunduru na Kibondo zimekusanya mapato kwa asilimia 104 ya makisio ya mwaka 2019/2020.

Hata hivyo Mhe.Jafo amezitaka Halmashauri zote zilizokusanya zaidi ya asilimia 100 hadi Desemba, 2019 na zile ambazo zimejitathmini na kuona upo uwezekano wa kuzidi asilimia 100 ya bajeti za mapato ya ndani ifikapo Juni, 2020 zinaelekezwa kufanya mapitio ya Bajeti kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 ili ziweze kuongeza Bajeti za mapato na matumizi ya fedha hizo.

“Katika kuzipima Halmashauri zote kwa kigezo cha wingi wa mapato (pato ghafi), Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekusanya mapato mengi zaidi kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya Shilingi Bilioni 29.75 na Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli imekusanya mapato kidogo kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya Shilingi Milioni 186.10” ,ameeleza Mhe. Jafo.

Hata hivyo Jafo amesema kuwa ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri Kimkoa kwa Kuzingatia Asilimia ya Makusanyo amesema Mkoa wa Geita umefanya vizuri ambapo umekusanya wastani wa asilimia 63 ya makisio ya Halmashauri za Mkoa huo.

Huku Mkoa wa mwisho kwa kigezo hicho ni Mkoa wa Tanga ambao umekusanya wastani wa asilimia 36 ya makisio ya mwaka ya Halmashauri za Mkoa huo.

Mhe. Jafo amesema kuwa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri Kimkoa kwa Kuzingatia wingi wa Mapato kuwa Mkoa wa Dar es Salaam umefanya vizuri kwa kukusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 83.86 na  Mkoa wa mwisho katika wingi wa ukusanyaji wa mapato ni Mkoa wa Katavi ambao umekusanya Shilingi bilioni 4.68.

“Ukusanyaji wa mapato kwa Halmashauri kwa Kuzingatia aina ya Halmashauri kwa Kigezo cha asilimia ya makusanyo ukilinganisha na makisio Waziri Jafo amesema kwa upande wa Majiji Jiji la Dar es Salaam limeongoza kundi la Halmashauri za Majiji kwa kukusanya mapato kwa asilimia 71 ya makisio yake na halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya kwa asilimia 41 ya makisio yake ya mwaka”,amefafanua Mhe.Jafo.

Kwa Upande wa Manispaa, Ilemela imeongoza kundi hilo kwa kukusanya  asilimia 75 ya makisio yake na Manispaa ya Kigoma imekuwa ya mwisho ambapo imekusanya kwa asilimia 26 ya makisio yake.

“ Katika Halmashauri za Miji, Mji wa Njombe umeongoza kwa kukusanya kwa asilimia  88 ya makisio yake ambapo Halmashauri ya Mji wa Babati imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 30 tu” alisema Jafo.

Aidha, kwa kundi la Halmashauri za Wilaya amesema  Wilaya za Tunduru na Kibondo zimeongoza kwa kukusanya asilimia 104 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka wa Fedha 2019/20 wakati Halmashauri za Mafia, Ukerewe na Gairo zimekuwa za mwisho katika kundi hilo kwa kukusanya asilimia 18 ya makisio.

Waziri Jafo aliongeza kuwa kwa upande wa mapato ya ndani ya Halmashauri kwa Kuzingatia Aina za Halmashauri kwa Kigezo cha Wingi wa Makusanyo Jiji la Dodoma limeongoza kwa kukusanya Shilingi bilioni 29.75 na Jiji la Dar es Salaam limekuwa la mwisho kwa kukusanya Shilingi bilioni 6.03.

“Halmashauri za Manispaa, Ilala imeongoza kwa kukusanya Shilingi bilioni 29.13 na  Manispaa ya Kigoma imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi Milioni 694.93.

Halmashauri ya Mji wa Geita imeongoza kwa wingi wa mapato katika Halmashauri za Miji ambapo imekusanya Shilingi Bilioni 4.64. Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi Milioni 459.44” alisema Jafo.

Kwa upande wa Halmashauri za Wilaya, Chalinze imeongoza kwa kukusanya mapato mengi kwa Halmashauri za Wilaya ambapo imekusanya Shilingi Bilioni 3.89 na Wilaya ya Bumbuli imekuwa ya mwisho kwa kukusanya Shilingi Milioni 186.08.

Hivyo Mhe. Jafo amezitaka halmshauri  zote kuendelea kukusanya mapato kwa njia ya kielektroniki na kudhibiti ukusanyaji wa fedha na mbichi na ameweka wazi kuwa     Taarifa ya mwisho ya kota ya nne ya ukusanyaji wa mapato ya ndani sambamba na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ataitoa tarehe 18.06.2020 kabla ya Bunge kuvunjwa hivyo kila mtu ahakikishe anatekeleza jukumu hili kwa ufanisi ili kufikia malengo