Mdau wa maendeleo wa Kata ya Magara Wilayani Babati Mkoani Manyara Dkt Juma Muna (katikati aliyevaa suti) akifuatilia fainali ya michuano ya Magara Salama 2019/2020 AFYA CUP iliyoshirikisha timu nane.
Mgeni rasmi wa michuano hiyo Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wa CCM wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Wilbroad Bayo akikagua mabingwa wa soka wa michuano ya Magara Salama 2019/2020 AFYA CUP Majita FC.
*********************************
Timu ya soka ya Majita FC ya Magara Wilayani Babati Mkoani Manyara, imetwaa ubingwa wa AFYA CUP Magara Salama 2019/2020 kwa mwaka wa pili mfululizo kuifunga Mkombozi FC mabao 2-0.
Katika michuano hiyo iliyodhaminiwa na mdau wa maendeleo wa kata ya Magara Dk Juma Muna, timu ya Majita FC ilijipatia kombe na sh100,000.
Dk Muna alisema lengo la kuandaa michuano hiyo ni kukuza michezo kwenye kata ya Magara na Babati kwa ujumla na kupanua wigo wa ajira kwa vijana kupitia vipaji vya mpira.
Alisema pia kuwaleta vijana pamoja na kuwapa elimu juu ya vita dhidi ya dawa za kulevya na kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi ili kupambana na maradhi yasiyoambukizwa.
Mgeni rasmi wa michuano hiyo Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wa CCM wilaya ya Babati, Wilbroad Bayo ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa CCM wilayani Babati, Alhaji Sogora aliwataka vijana kutumia michuano hiyo kukuza vipaji vilivyopo na kuibua vipaji vipya.
Bayo alisema vijana kama Dk Muna wanapaswa kuungwa mkono kwenye maendeleo ya jamii kwani wametumia elimu yao kwa manufaa ya watu wanaowazunguka.
Wachezaji 240 wa timu zote nane, kila timu wachezaji 30 walipimwa magonjwa mbalimbali ikiwemo shinikizo la damu, kisukari, malaria, hali ya mlo na elimu ya maambukizi ya VVU.
Michuano hiyo ilishirikisha timu nane za Majita FC, Mkombozi FC, Tiger Stars, Manyara FC, Town Worious, Kisese SC, Scopion FC na Wayamkali.
Michuano hiyo iliwapa faida wachezaji sita wa timu tofauti waliopata fursa ya kuunganishwa na kituo cha michezo Arusha kwa lengo la kuendeleza vipaji vyao.