Home Mchanganyiko ASHAURI ELIMU YA ZIMAMOTO IZINGATIWE

ASHAURI ELIMU YA ZIMAMOTO IZINGATIWE

0

Na, Francisca Swai-Musoma

……………………….

Viongozi wa ofisi za Serikali  wameshauriwa  kuwa na tabia kuzingatia kuwapatia watumishi wao elimu ya zima moto na uokozi , ikiwemo vifaa vya uzimaji ili  kuepusha madhara ya kuungua kwa nyaraka muhimu za taifa.

Kauli hiyo ilitolewa jana Desemba 19, mwaka huu na Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Bw. Peter Kisaka wakati alipokuwa akitoa mafunzo elekezi ya zimamoto na uokoaji kwa Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma. 

Akitoa  mafunzo hayo, Kisaka, aliyataja  aina, makundi na namna ya uzimaji moto, ambapo  pia aliupongeza  uongozi wa mahakama hiyo kwa kuwa umefanya jambo la msingi  kuyaandaa.

‘Maofisi mengi hasa ya Serikali yanatunza nyaraka muhimu kwa taifa letu lakini hawazingatii elimu ya zima moto na uokozi, na wengine hata vifaa vya zimamoto hawana kabisa. Mfano huu walionyesha viongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya  Musoma uwe wa kuigwa na viongozi wengine,’ alisema Masaka

Aliongeza kwamba suala la moto halina taarifa ni kitu cha ghafla na kisipodhibitiwa mapema mapema kinaweza kuleta madhara makubwa kwa taasisi na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake mtumishi wa mahakama hiyo, Bw. Juma Maiga alisema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambapo watumishi wameelimishwa juu ya tahadhari ya moto na uokozi kulingana na mifumo iliyopo katika jengo hilo.

 ‘Na hata tunapoendelea kufanya kazi mahali hapa tunakuwa na amani maana angalau tunajua pa kuanzia iwapo janga la moto likijitokeza wakati wowote,” alisema  Maiga.

Mafunzo hayo  yametolewa kwa watumishi  hao, baada ya  kuhamia katika jengo jipya la mahakama hiyo lililoko Bweri, Musoma mjini kutoka katika majengo ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ambako shughuli za Mahakama Kuu zilikuwa zikiendeshwa huko.