Home Mchanganyiko UMEME NI USALAMA WEKENI KWENYE NYUMBA ZENU-WAZIRI KALEMANI

UMEME NI USALAMA WEKENI KWENYE NYUMBA ZENU-WAZIRI KALEMANI

0

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, akitunza moja ya kikundi cha waimbaji cha kijiji cha Kakeneno kabla ya kuwasha umeme katika kijiji hicho.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akikata utepe kuashiria kuwashwa kwa umeme katika kijiji cha Kakeneno kata ya Nyarutembo wilayani Chato  Mkoa wa Geita.

Katibu kata wa kijiji cha Kakeneno Emmanuel Ruzigamazi akizungumza kwenye mkutano wa hadhara kabla ya Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani hajawasha umeme katika kijiji hicho.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani,( mwenye shati la bluu) akiagana na wananchi wa kijiji cha Kakeneno mara baada ya kuwasha umeme katika kijiji hicho.

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kakeneno ambao walijitokeza kwa wingi kumsikiliza kiongozi huyo.

****************************

Hafsa Omar- Geita

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amesema kuweka umeme kwenye nyumba ni kujihakikishia usalama ndani ya nyumba na inasaidia kuepuka madhara mbali mbali yatokanayo na binadamu, wadudu na wanyama wakali.

Ameyasema hayo, Desemba 17, mwaka huu katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kakeneno, kata ya Nyarutembo, Wilaya ya Chato, mkoani Geita kabla ya kukiwashia umeme kijiji hicho.

“Nyumba inapokuwa giza kuna hatari wa wanyama wakali  au wadudu wenye sumu kuingia bila ya wewe kuwaona, anaweza kuingia Nyoka, Nge na  kusababisha madhara makubwa, lakini nyumba ikiwa na umeme utawaona na utaweza kukabiliana nao.” Alisema

Vile vile, amewahimiza wananchi kujenga viwanda vidogo vidogo ambavyo vitawasaidia kujikwamua kiuchumi na kuviunganisha na umeme, kwasababu utumiaji wa umeme kwenye viwanda hivyo utawasaidia kupata kupata faidi nyingi kulinganisha na utumiaji wa mafuta. 

“ Nimefurahi kuona mashine ya kukoboa na kusaga mahindi hapa, unganisheni mashine hizo na umeme, ukiwa na umeme badala ya kupata mabede manne kwa siku utapata madebe kumi kwa siku.” Aliongeza

Naye, Katibu Kata, Emmanuel Ruzigamazi amesema ujio wa umeme katika kijiji hicho utaleta mabadiliko mengi ya kiuchumi kwani wananchi wa kijiji hicho walikuwa wanausubiri umeme kwa muda mrefu ili kuutumia kwa shughuli mbalimbali ikiwemo za kiuchumi.

Pia ameipongeza Serikali kwa kupeleka umeme katika kijiji hicho, ambacho kabla ya kuwepo kwa umeme kulikuwa na changamoto kubwa kwenye zahanati ambapo baadhi ya

wagonjwa walikosa huduma kwa sababu ya kukosekana kwa nishati hiyo, ila kwa sasa huduma zitazidi kuboreka.