Home Mchanganyiko NAIBU MKURUGENZI WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI NCHINI KOREA AMETEMBELEA MLOGANZILA

NAIBU MKURUGENZI WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI NCHINI KOREA AMETEMBELEA MLOGANZILA

0

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru (kushoto), akizungumza na Naibu Mkurugenzi wa Wizara ya Fedha na Uchumi nchini Korea, Bw. Hwang Seokchae alipotembelea hospitalini hapa.

Baadhi ya viongozi wa Hospitali ya Mloganzila waliompokea Bw. Hwang Seokchae, kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala Bi. Njoikiki Mapunda, kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Dkt. Mohamed Mohamed.

Baadhi ya Viongozi wa MNH-Mloganzila wakisikiliza mambo mbalimbali yaliyokuwa yakizungumzwa wakati wa mkutano mara baada ya mapokezi ya wageni waliotembelea hospitalini hapa leo.

Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Tehama, Bw. Pius Maswaga akiwaelezea wageni waliotembelea kitengo hicho namna chumba cha kuhifadhi data (Server room) kinavyofanya kazi.

 Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi MNH-Mloganzila Sr. Redemptha Matindi akiwaonyesha wageni baadhi ya wodi za wagonjwa binafsi (Private ward) zilizoko hospitalini hapa.

Wageni wakiangalia namna mashine ya CT-Scan inavyofanya kazi mara baada ya kutembelea Kitengo cha Radiolojia.

Prof. Museru na Bw. Seokchae katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Hospitali ya Mloganzila mara baada ya kutembelea hospitalini hapa.

……………….

Naibu Mkurugenzi wa Wizara ya Fedha na Uchumi nchini Korea leo ametembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila ili kufahamu huduma zinazotolewa hospitalini hapa.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni huyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru amemueleza kuwa hospitali ya Mloganzila inatoa huduma za kibingwa na kibobezi na ina jumla ya vitanda 608 pamoja na wafanyakazi takribani 700.

“Hospitali yetu inatoa huduma za kibingwa na kibobezi na ina jumla ya vitanda 608 ikiwa ni hospitali ya tatu kwa ukubwa nchini na yenye wafanyakazi takribani 700 wanaofanya kazi ya kutoa huduma za afya kwa umma,” amesema Prof. Museru.

Aidha Prof. Museru amefafanua kuwa lengo la hospitali ya Mloganzila ni kufikia uwezo wa kutoa matibabu ya ubingwa wa juu ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano ya kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi na badala yake matibabu hayo kutolewa hapa nchini.

Prof. Museru ametaja kuwa hospitali inatarajia kuanza kutoa huduma mbalimbali za kibingwa kama vile upandikizaji uloto (Bone marrow transplant) na hivyo kwa kushirikiana na wataalam kutoka Korea itaisaidia hospitali kuweza kuendelea kutoa huduma bora za afya kwa watanzania.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Wizara ya Fedha na Uchumi nchini Korea, Bw. Hwang Seokchae amefurahishwa na namna hospitali ya Mloganzila inavyohakikisha jamii inayowazunguka inapata huduma bora za afya.

“Nimefurahi sana kuitembelea hospitali hii na natumaini ushirikiano huu utazidi kuwa na manufaa hasa kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kutoa Huduma za Afya la Korea (KOFIH) pamoja na Shirika la Ushirikiano wa Kimaendeleo la Korea (KOICA),” amesema Bw. Seokchae. 

Mgeni huyo ametembelea Wodi ya wagonjwa binafsi (Private ward), Kitengo cha Tehama (ICT), Kitengo cha Magonjwa ya Dharura (EMD) pamoja na Radiolojia na kujionea namna wataalam wanavyofanya kazi.