Home Mchanganyiko TAA yasaidia kutokomeza mimba za Utotoni mkoani Tabora

TAA yasaidia kutokomeza mimba za Utotoni mkoani Tabora

0

Mbunge wa Viti Maalum wa Jimbo la Tabora, Mhe. Munde Tambwe
(wenye gauni la kijani na njano) hivi karibuni akiwa na Kaimu Meneja Masoko wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Rose Comino (wa tatu
kushoto) akimwakilisha, Mhandisi Julius Ndyamukama kukabidhi saruji tani 12.5
kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa kike wa Kata mbalimbali za
Tabora.

Kaimu Meneja Masoko wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania
(TAA), Rose Comino (wa pili kushoto) hivi karibuni akimwakilisha, Mhandisi
Julius Ndyamukama akiwa kwenye picha ya pamoja na Mbunge Viti Maalum
(CCM), Mhe. Munde Tambwe (wa tatu kushoto) mara baada ya kukabidhi
msaada wa saruji tani 12.5, kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya watoto wa kike wa shule za sekondari. Wengine pichani ni Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya
Tabora, Joseph Kashushura (kushoto) na Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege
cha Tabora (wapili kulia).

Moja wa Shule ya sekondari ya Kata ya Itonjanda ya Manispaa ya
Tabora, ambayo itajengwa bweni la watoto wa kike ili kuondoa mimba za utotoni. Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) hivi karibuni imetoa msaada wa saruji tani 12.5 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni hayo.

***************************************

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeungana na Mbunge wa Viti
Maalum na Wakazi wa Mkoa wa Tabora kusaidia jitihada zao za kutokomeza mimba za utotoni kwa kutoa msaada wa tani 12.5 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa kike wa shule za sekondari.

 

Akikabidhi saruji hiyo hivi karibuni katika Kata ya Itonjanda, Manispaa ya Tabora, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Julius Ndyamukama, ambayo ni sawa na mifuko 250 ya saruji, Kaimu Meneja wa Biashara wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Rose Comino, amesema TAA, ipo bega kwa bega katika suala zima la kusaidia jamii katika masuala mbalimbali likiwemo la Elimu, ambapo watoto wote ni sawa na wanastahili kupata elimu na sio kukatizwa masomo kutokana na vikwazo mbalimbali zikiwemo mimba za utotoni.

 

Rose amesema Wananchi wa Tabora waungane kwa pamoja kuunga mkono jitihada za Mhe. Mbunge Viti Maalum Munde Tambwe la ujenzi wa mabweni kwa ajili ya watoto wa kike wa shule za sekondari, ambao wanatembea umbali mrefu kwenda shule, ambapo sasa watokomeza mimba za utotoni na kushirikiana kuwabaini wale wote wenye kutenda matendo hayo maovu.

 

“Kwa pamoja tuoneshe jitihada za dhati kwa kuhakikisha watoto wetu wanakuwa sehemu salama mabwenini, ninauhakika wa asilimia 100 kwa 100 tutapata watoto wengi wa kike watakaomaliza shule na kufanya vizuri katika masomo yao,” amesema Rose.

Amesema TAA ni miongoni mwa taasisi ya serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Wakala wa Serikali Na.30 ya mwaka 1997 na kupewa dhamana na Serikali ya kuvisimamia na kuviendesha jumla ya viwanja 58, imekuwa ikitekeleza sera yake ya kurudisha kwa Jamii katika masuala mbalimbali yakiwemo ya elimu.

 

Rose amesema viwanja vya ndege vinatoa fursa mbalimbali za kibiashara zikiwemo za kuendesha migahawa, hoteli, maduka ya bidhaa mbalimbali, usafirishaji wa mizigo ikiwemo mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

 

Pia viwanja vya ndege vimekuwa ni miongoni mwa eneo linalozalisha ajira rasmi na zisizo rasmi, ambazo zinahusisha mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya nchi yenye kutoa huduma katika maeneo ya viwanja vya ndege.

 

Naye Mhe. Tambwe ameushukuru uongozi mzima wa TAA kwa kusaidia jitihada hizo, ambazo anauhakika kwa lengo alilojiwekea ataweza kusaidia ujenzi wa mabweni mengi katika kila kata ya Mkoa wa Tabora.

 

“Naomba ndugu zangu tuunge jitihada hizi nilizoanzisha, na pia kuungana na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kutoa elimu bure, mimi nimezaliwa hapa Tabora na nimeona jinsi gani mabinti zetu wanavyotembea umbali mrefu kwenda na kurudi shule jambo ambalo linachangia kupata vishawishi njiani na kujikuta wanapata mimba za utotoni.” Amesema Mhe. Tambwe.

 

Hatahivyo, amesema mifuko 100 kati ya hiyo 250 itapelekwa kwenye Kata ya Itonjanda, ili ujenzi uanze mara moja, na 150 iliyosalia itapelekwa kwenye shule nyingine.

 

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Itonjanda ameshukuru msaada huu uliotolewa na TAA kwani watoto wamekuwa wakitembea umbali wa Kilometa 10 kwenda shule, na wamekuwa wakiathirika kutokana na kupata mimba.

 

“Tumuunge mkono Rais wetu kwani Tanzania bila elimu haitaienda tuunge jitihada hizi kwani watoto wanakuwa wananawiri sana wanapoingia shule za sekondari, kwani wamekuwa wakipewa fedha ndogo ndogo ambazo zimekuwa zikiwaponza na kujikuta wanapata ujauzito.” Amesema.