Home Mchanganyiko Tamko la THBUB wakati wa maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu...

Tamko la THBUB wakati wa maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani, Desemba 10, 2019

0

**************************************

Leo Desemba 10, 2019 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB)
inaungana na wadau wa haki za binadamu ulimwenguni kote kuadhimisha miaka
71 ya Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu (Universal Declaration for
Human Rights).

Desemba 10, 1948 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio la
Ulimwengu la Haki za Binadamu ambalo linaainisha haki za msingi za binadamu.
Azimio hili linatoa mwongozo kwa Serikali na jamii duniani kote kuhakikisha
kuwa zinaheshimu, zinalinda na kukuza haki za binadamu kama zilivyoainishwa
katika mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa.

Katika maadhimisho ya mwaka huu kitaifa kauli mbiu yetu inasema: Maadili
katika utumishi wa umma ni nguzo muhimu katika kuimarisha utawala bora na
haki za binadamu.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inatambua kuwa maadili ya
viongozi, watendaji na watumishi katika utumishi wa umma ndiyo muhimili mkuu wa kuzingatia hifadhi ya haki za binadamu na wajibu kwa jamii kwa mujibu wa Katiba na Sheria.

Kwa msingi huo, THBUB inawaasa watumishi wa umma kuzingatia haki za
binadamu na misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yao. Pia
inawahimiza wananchi na watumishi wa umma kuwasilisha malalamiko Tume
pindi waonapo haki zao za msingi zimeingiliwa au kuvunjwa na viongozi au
watendaji katika utumishi wa umma kwa kutumia madaraka kinyume cha Sheria.

Kimataifa maadhimisho haya yamebeba kauli mbiu isemayo: Vijana piganieni
haki za binadamu (Youth standing up for human rights). Kauli mbiu hii
inatambua wajibu na nafasi ya vijana katika kuhakikisha kuwa haki za binadamu
zinaheshimiwa na kufurahiwa na watu wote duniani. Aidha, inawahamasisha
kuzipigania haki hizo pale ambapo hazipatikani.

Hivi sasa duniani kote tunashuhudia vijana wakipaza sauti zao wakipigania haki
mbalimbali, zikiwemo haki ya usawa, haki ya kufanya kazi, haki ya kushiriki
katika kufanya maamuzi na haki nyinginezo nyingi.

Tume inapenda kuwakumbusha wananchi na hususan vijana kutimiza wajibu wao wa kutii na kuheshimu sheria za nchi na kutumia mifumo na njia sahihi katika kudai haki; na kuepuka kutumika na watu wasiolitakia mema taifa letu, ili
kudumisha amani na utulivu wa nchi yetu.

Tanzania inatambua na kuthamini uwezo na mchango wa vijana katika kuleta
maendeleo endelevu ya taifa, na hili linadhihirishwa na kauli maarufu isemayo
‘vijana ni nguvu kazi ya taifa.’ Aidha, zipo jitihada mbalimbali za Serikali
zinazolenga katika masuala ya maendeleo ya vijana nchini; hii ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mifumo, sera, mipango na mikakati inayokidhi mahitaji mbalimbali ya vijana kama vile Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 yenye lengo la kuhakikisha taifa linakuwa na vijana wenye uwezo, wenye ari ya kutosha, wanaowajibika na wanaoshiriki kikamilifu katika nyanja zote za kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaipongeza sana Serikali kwa
jitihada hizi. Lakini pamoja na jitihada hizo, bado zipo changamoto kadhaa
ambazo wadau mbalimbali hususan vijana wanakumbana nazo, zikiwemo
kufahamika kwa mifumo, mikakati, fursa, upatikanaji na utolewaji wa taarifa kwa vijana, upatikanaji wa mikopo, na uelewa mdogo juu ya sera hii ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007.

Hivyo basi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaziomba mamlaka
husika, Serikali na wadau mbalimbali kutoa elimu ya kutosha kuhusu uwepo wa
fursa mbalimbali kwa maendeleo ya vijana na wasimamizi kuhakikisha fursa hizo zinatolewa kwa usawa, kwa vijana wote bila ubaguzi. Na hii itasaidia kuepusha vurugu na ukosefu wa amani na utulivu katika taifa letu.

Aidha, Tume inaendelea kuwahimiza Wananchi kuwasilisha malalamiko yao kwa
taasisi husika na pale wanapoona wametendewa kinyume na sheria, na pale
ambapo wataona kuna usumbufu au malalamiko yao hayashughulikiwi ipasavyo
wasisite kuwasilisha malalamiko kwa kuiandikia Tume au kufika kwenye
mojawapo ya ofisi zake zilizopo Dodoma – Makao Makuu ya Tume (Mtaa wa
Nyerere, Ploti Na. 339 eneo la Kilimani,) au Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) –
jengo la Taaluma la Chuo cha Elimu ya Biashara na Sheria. Pia katika ofisi zake
zilizoko Zanzibar ( Unguja na Pemba), Dar es Salaam, Mwanza na Lindi.